Jumanne, 21 Juni 2016
Jumatatu, 20 Juni 2016
Majibu 10 ya Bajeti yasubiriwa bungeni leo
MAMBO makubwa 10 yaliyojitokeza kwenye mjadala wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17 pamoja na Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2015, yatajibiwa na kutolewa ufafanuzi leo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango bungeni.
Moja ya mambo hayo ni hoja ya kufuta au kutofuta kodi kwenye kiinua mgongo cha wabunge. Kabla ya Dk Mpango kutoa ufafanuzi na marekebisho ya Bajeti Kuu ya Serikali, kama yatakuwepo na hatimaye kupitishwa au kutopitishwa kwa kupigiwa kura, mawaziri mbalimbali wanatarajiwa pia kujibu baadhi ya hoja zilizoelekezwa kwenye wizara zao.
Kutokana na mjadala wa bajeti uliochukua takribani wiki nzima, wabunge walipendekeza kodi na tozo kadhaa kufutwa ili kuwapunguzia wananchi mzigo, hatua itakayosababisha serikali kuongeza kodi kwenye baadhi ya vitu kama itakubaliana na hoja za wabunge. Moja ya eneo linaloweza kukumbwa na ongezeko la kodi kama serikali kama wanavyopendekeza wabunge ni petroli.
Alipowasilisha Bajeti ya Serikali Juni 8, Waziri Mpango alisema serikali haikuongeza kodi yoyote kwenye petroli na dizeli ili kutowaongezea wananchi mzigo na hofu ya kusababisha mfumuko wa bei.
Kiinua mgongo cha wabunge Wawakilishi hao wa wananchi wamekuwa wakipinga hatua ya serikali kupendekeza kuwakata kodi ya asilimia tano kwenye kiinua mgongo chao wanacholipwa kila baada ya miaka mitano, wakidai kitawaumiza kwa kuwa wao hawalipwi pensheni na kwamba fedha hizo, mbali na kujikimu, zinawasaidia pia katika kuchangia shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwenye majimbo yao.
Takwimu zilizopo zinaonesha kwamba mwaka jana Bunge la 10 lilipovunjwa, kila mbunge alilipwa kiinua mgongo cha Sh milioni 230 na kama wabunge watalipwa kiasi kama hicho mwaka 2020, kila mbunge atabakiwa na Sh milioni 218.5 baada ya kukatwa kodi hiyo wanayoilalamikia.
Mbunge wa Nsimbo, Richard Mbogo (CCM), alidai kwamba hatua ya kuwakata wabunge kodi kwenye kiinua mgongo inapaswa kuangaliwa upya kwani wabunge wa Tanzania ndio wanaolipwa mshahara mdogo kulinganisha na wenzao wa Afrika Mashariki.
Alidai kwamba mbunge wa Kenya analipwa Dola za Marekani 11,000, Rwanda Dola 9,000, Uganda Dola 8,000, Sudan Kusini Dola 7,000, Burundi Dola 6,000, wakati wabunge wa Tanzania hulipwa Dola 5,000. Wabunge wanaona pia kama hatua hiyo ni ya kibaguzi wakisema kama serikali imefikia uamuzi huo katika kusaka mapato zaidi, basi ni vyema kodi ya kiinua mgongo iende hadi kwa marais, makamu wa rais, mawaziri wakuu, maspika na naibu spika na wakuu wa mikoa na wilaya.
Mtazamo huu wa wabunge ni tofauti na walio nao wananchi wengi nje ya Bunge wakiwemo wasomi ambao wanaamini kwamba wabunge ambao wamekuwa wakiomba sana maendeleo kwenye majimbo yao, wangekuwa wa kwanza kuonesha utayari wa kuchangia mapato ya serikali kwa kukubali kukatwa kodi hiyo. Hata hivyo, wapo wabunge kadhaa wa CCM na karibu wote wa upinzani wamehiari kukatwa kodi kwenye kiinua mgongo chao.
VAT kwenye utalii Suala la pili lililozungumziwa na wabunge wengi ni kuitaka serikali kuachana na hatua ya kuanzisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya asilimia 18 kwenye huduma za utalii. Wakati akiwasilisha hotuba yake ya Bajeti, Dk Mpango alisema kwamba kodi hiyo ipo pia katika nchi za Kenya, Afrika Kusini na Rwanda. Lakini wabunge katika mjadala walimpa angalizo Waziri kwamba Kenya imeondoa kodi hiyo na bila shaka sababu ni kujikuta wakipoteza watalii wengi.
Walisema kama serikali haitaondoa kodi hiyo basi itegemee mpango wa kuongeza watalii zaidi kutofanikiwa kwani wengi watakimbilia maeneo yatakayoonekana kutokuwa ghali. CAG aongezewe fedha Suala la tatu lililozua mjadala mkubwa ni hatua ya serikali kuipunguzia fedha ofisi ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kulinganisha na kiwango kilichoombwa wakisema hatua hiyo itaifanya ofisi hiyo muhimu katika kupambana na ufisadi kushindwa kutimiza majukumu yake.
Ofisi hiyo iliomba Sh bilioni 68.8 katika mwaka huu wa fedha ili itekeleze majukumu yake kwa ufanisi lakini katika bajeti inayopendekezwa imepewa Sh bilioni 32.3 pekee. Wabunge walisema ofisi hiyo ni chombo muhimu katika kupeleka ushahidi kwenye Mahakama ya Mafisadi inayotarajiwa kuundwa mwezi ujao hivyo ni lazima serikali ihakikishe utendaji wake haukwamishwi na uhaba wa fedha.
Wabunge pia waliitaka serikali kuongeza fedha kwenye miradi ya maji kwani maji ndio kero kubwa inayowasumbua wananchi wengi na hata wakati wa kampeni, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alikiri kwamba ndio kilikuwa kilio kikubwa cha wananchi alichokutana nacho. Walitaka serikali iongeze Sh 50 kwenye petroli kwa ajili ya miradi ya maji vijijini sawa na ambavyo imekuwa ikifanyika kwenye mkakati wa kupeleka umeme vijijini ambao kwa kiwango kikubwa umeleta mafanikio.
TRA na kodi ya majengo Lingine lililozua mjadala mkubwa kwenye mapendekezo ya serikali katika bajeti yake ni kuhamisha jukumu la ukusanyaji wa kodi za majengo kutoka katika halmashauri na kupelekwa katika Mamlaka ya Mapato (TRA). Wabunge waliopinga mpango huo walitaja sababu zaidi wakidai taarifa walizonazo ni kwamba hata mpango wa majaribio wa TRA kukusanya kodi za majengo katika mkoa wa Dar es Salaam haukuzaa matunda makubwa.
Waliokubaliana na pendekezo hilo la serikali nao walitoa angalizo kwamba kama hatua hiyo itachukuliwa ni lazina kuwe na utaratibu utakaohakikisha kwamba fedha hizo hazichelewi kupewa halmashauri husika kwa kuwa zimekuwa zikitegemewa sana kwa shughuli mbalimbali. Takwimu za mikoa masikini Lingine lililowagawa wabunge ni kuhusu takwimu za mikoa mitano masikini zaidi nchini na mitano yenye ahueni ambapo baadhi ya wabunge walizitilia mashaka.
Mbunge mmoja alishangaa kuona mkoa wa Mwanza ukiwa miongoni mwa mikoa mitano masikini wakati taarifa ya Benki Kuu inaonesha kwamba mkoa huo ni wa pili katika kuipatia Hazina mapato mengi nyuma ya Dar es Salaam.
Akiwasilisha bungeni Taarifa ya Hali ya Uchumi ya Mwaka 2015, Dk Mpango alitaja mikoa masikini zaidi kuwa ni Kigoma, Geita, Kagera, Singida na Mwanza huku yenye ahueni ikiwa ni Dar es Salaam, Kilimajaro, Arusha, Pwani na Manyara.
Kodi miamala ya simu, mitumba Jambo la saba ambalo wawakilishi hao wa wananchi walitaka serikali iliangalie kwa mapana yake pia ni kodi kwenye miamala ya simu na benki. Hofu ya wabunge ilikuwa kwamba kama kodi hiyo itawekwa bila udhibiti wowote, kampuni, hususan za simu zitahamishia ‘maumivu’ ya kodi hiyo kwa wananchi.
Lingine ambalo wabunge walililalamikia ni Bajeti inayopendekezwa na serikali kupandisha ushuru wa nguo na viatu vya mitumba kutoka Dola za Marekani 0.2 mpaka Dola za Marekani 0.4 kwa kilo. Hatua hiyo ambayo ni sehemu ya makubaliano ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, inalenga kudhibiti mitumba ikiwa ni sehemu ya kujiandaa kwa kuzuia kabisa uingiaji wake.
Kubenea Amshitaki Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson
Wakati
Kamati ya Haki, Maadili na Madara ya Bunge imepokea mashtaka dhidi ya
Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, mbunge mwingine wa upinzani
ameamua kumshtaki kiongozi huyo kwenye Kamati ya Kanuni ya Bunge.
Mbunge
wa kwanza kumshtaki Dk Tulia, alikuwa Mbunge wa Simanjiro (Chadema),
James ole Millya aliyewasilisha kusudio lake kwa Spika wa Bunge hilo,
Job Ndugai mashtaka sita na tayari yamewasilishwa kwenye kamati husika.
Mbunge
wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea alitangaza jana uamuzi wake wa
kumshtaki Dk Tulia, ambaye ndiye anayeliongoza Bunge kwa sasa.
Dk Tulia atakuwa na kesi mbili, Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka na kwenye Kamati ya Kanuni.
Dk
Tulia anakuwa Naibu Spika wa kwanza tangu kuanza Bunge linalojumuisha
wabunge wa upinzani, kushtakiwa kwa madai ya kukiuka kanuni na taratibu
za Bunge.
Kubenea
alisema ameamua kumshtaki Dk Tulia katika kamati hiyo akidai kuwa
alivunja kanuni na taratibu wakati akiwasilisha malalamiko ya Waziri wa
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi kwenye Kamati ya
Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuwa mbunge huyo alisema uongo
bungeni.
Akizungumza
na wanahabari, mbunge huyo alisema hakuridhishwa na hatua ya Dk Tulia
aliyoifanya Mei 13 na kwamba tayari alishawasilisha barua yake yenye
hoja tano za mapungufu ya kikanuni kwa Katibu wa Bunge, Dk Thomas
Kashililah tangu Ijumaa iliyopita.
Kubenea
alieleza kuwa Dk Tulia alitumia kanuni ya 71 kupokea malalamiko ya Dk
Mwinyi kinyume na utaratibu kwa kuwa kanuni hiyo huruhusu watu wasio
wabunge kupeleka malalamiko yao kwa Spika, iwapo masuala yaliyojadiliwa
bungeni yamewaathiri.
Alisema
wakati akichangia hoja ya wizara hiyo Mei 10, alimtaka Dk Mwinyi aeleze
juu ya kuwapo kwa mkataba baina ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na
Kampuni ya Heinan Guoji Industry & Investment Limited na kama upo
haoni kama kuna mgongano wa masilahi kutokana na kushiriki kumjengea
nyumba yake.
Hata
hivyo, alidai hakuna mbunge aliyesimama kudai hoja hiyo ilikuwa ya
uongo kama kanuni ya 63(3) inavyotaka, badala yake siku tatu baadaye
alitakiwa kufuta bungeni jambo ambalo anaona Dk Tulia hakumtendea haki.
“Naibu
Spika wakati akitoa mwongozo wa Spika alinukuu sehemu tu ya maelezo
yangu jambo lilipotosha misingi na mantiki ya mchango wangu bungeni
hivyo kuashiria alikuwa na nia mbaya dhidi yangu,” alisema Kubenea na kuongeza: “Hata
nilipoomba kufanya hivyo siku aliposoma mwongozo na kunipa nafasi ya
kufuta maneno yangu au kuyathibitisha, alikataa na endapo angezingatia
mchango wangu wote angetenda haki.”
Katika
barua hiyo, Kubenea amelalamika kuwa wakati Dk Tulia anapokea
malalamiko kutoka kwa Dk Mwinyi hakumpelekea nakala ili kurahisisha
utetezi wake.
Pia,
alieleza kuwa Naibu Spika aliamua kimakosa kuwasilisha tuhuma dhidi
yake kwenye kamati hiyo bila kuzingatia maelezo aliyowasilisha kwake na
vielelezo huku akijua Waziri huyo wa ulinzi alikiuka kanuni ya 63 (3) na
64(2).
Kubenea
alisema anaiomba Kamati ya Kanuni yenye nguvu kuliko Spika kusimamisha
mchakato unaoendelea kufanywa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya
Bunge juu ya suala lake hadi pale itakapofanya uamuzi iwapo ilifuata
kanuni ama la.
Katika
barua hiyo, Kubenea anamuomba Dk Kashililah amjulishe Spika ili aweze
kuitisha kikao cha Kamati ya Kanuni kwa mujibu wa kanuni ya 5(5) ili
kuona kama kulikuwa na uhalali wa shauri lake na anaamini Katibu huyo wa
Bunge atamtendea haki.
Kubenea
alishahojiwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge Alhamisi
iliyopita na kueleza kuwa alikubali kufanya hivyo kwa kuwa kamati hiyo
ina nguvu kubwa ya kikanuni ikiwamo kukamatwa.
Kubenea
alisema hana wasiwasi na aliyoyasema ila anataka haki itendeke kwa
kufuata kanuni na hadi sasa ana vielelezo vya kutosha kuhusu suala lake.
Dk Kashililah alieleza jana kuwa hawezi kuzungumzia kwa kina jambo hilo kwa kuwa taratibu zote za kufuata zinafahamika.
“Inawezekana
ameandika, lakini mpaka ifike tuipokee. Mimi nilikuwepo Ijumaa hadi saa
tano usiku sikuiona. Huenda ipo njiani ikifika tutaipokea na
tutaifanyia kazi,” alisema Kashililah.
Serikali Yasitisha Ajira Zote Kwa Muda
SERIKALI imesitisha ajira zote, kama njia ya kukabiliana na wimbi la watumishi hewa.
Kutokana
na uamuzi huo hivi sasa hakuna nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa
Serikali na wakala zake pamoja na utoaji wa vibali wa likizo ya bila
malipo.
Katibu
Mkuu Utumishi, Dk. Laurean Ndumbaro, jana alisema kuwa Serikali
imesitisha kwa muda utoaji wa ajira, ili kupitia upya muundo wa Serikali
na taasisi zake.
Alisema
utekelezaji wa mkakati huo utakwenda sambamba na kusitisha kwa muda
utoaji wa vibali vya ajira zote mbadala pamoja na uidhinishaji wa ajira
hizo zilizopo Sekreterieti ya Ajira katika utumishi wa umma na kwenye
mfumo wa taarifa za kiutumishi.
“Ni
kweli tumesitisha kwa muda ili kupitia mfumo wa Serikali na hata
kuangalia ulipaji wa mishahara kama upo katika malipo stahiki.
“…na
hili litakwenda sambamba na hata kusitishwa malipo ya mishahara
yanayotokana na upandishwaji wa vyeo kwa watumishi. Tukimaliza zoezi
hili ndipo tunaweza kuanza kutoa ajira za Serikali,” alisema Dk. Ndumbaro.
Alisema
muundo mpya wa utumishi wa Serikali unakwenda sambamba na uhakiki wa
malipo ya mishahara, hivyo ni lazima ujue ni nani unayemlipa kuliko
ilivyo sasa.
Kwa
mujibu wa maelekezo hayo uhamisho na uidhinishaji katika mfumo wa
watumishi ambao wamehamishwa kutoka kwa mwajiri mmoja kwenda kwa mwajiri
mwingine ambao atalipwa mshahara mkubwa kuliko ule wa sasa pia
utaangaliwa kwa lengo la kupata taarifa sahihi za mtumishi husika.
“Baada
ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki watumishi pamoja na tathmini ya
muundo wa Serikali na taasisi zake, wote wataarifiwa ni lini utekelezaji
utaendelea,” alisema.
Taarifa
kutoka maeneo mbalimbali nchini, zinaarifu kuwa maelekezo hayo
yalitolewa Juni 13, mwaka huu na kusambazwa katika maeneo mbalimbali
ikiwemo kwa makatibu wakuu wote, makatibu tawala wa mikoa, kwa wakuu wa
idara za Serikali zinazojitegemea.
Waliotakiwa
kutekeleza maelekeo hayo ya Serikali ni wakurugenzi wote wa majiji,
manispaa na miji, wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya,
watendaji wa taasisi za umma na watendaji wa wakala za Serikali kwa
upande wa Tanzania Bara.
Kamatakamata
Wiki iliyopita vyombo vya dola vilianza kuwatia mbaroni watumishi hewa kwa kuwafuata na pingu majumbani.
Hatua
hiyo imetajwa kuwa ni mkakati wa Serikali ya awamu ya tano chini ya
Rais Dk. John Magufuli, kuanza kupambana na watendaji ambao wamekuwa
wakiisababishia hasara Serikali ya kulipa mamilioni ya shilingi kwa
watumishi hewa.
Kutokana
na uamuzi huo ambapo mtumishi mmoja wa moja za Mkoa wa Kigoma,
alifuatwa na askari wa polisi na kutiwa mbaroni nyumbani kwao Ubungo
Kibangu jijini Dar e Salaam.
Tukio
hilo la aina yake lilitokea mchana wa juzi na kuibua hisia miongoni mwa
majirani ambao waalisema kuwa, askari hao walifika nyumbani kwao na
mtumishi huyo na kumfunga pingu mikono na miguuni na kuondoka naye.
Kutokana
na hekaheka hiyo ya watumishi hewa, taarifa kutoka wilayani Nyasa
mkoani Ruvuma, zilidai kuwa walimu watano wastaafu nao walikamatwa na
polisi kwa madai ya kupokea mishara hewa.Mbali na walimu hao pia
alikuwepo muuguzi mmoja.
Hivi
karibuni akizungumza Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki,
alisema Serikali imewaondoa jumla ya watumishi 12,246 kwenye mfumo wa
malipo ya mishahara kwa sababu mbalimbali, ikiwemo umri wa kustaafu kwa
lazima, kufukuzwa kazi, vifo na kumalizika kwa mikataba.
Waziri Kairuki alisema kuondolewa kwa watumishi hao kumeokoa Sh bilioni 25 ambazo zingelipwa kwa watumishi hao.
Alisema
kuwa fedha hizo zingepotea endapo watumishi wasingeondolewa kwenye
mfumo, ikilinganishwa na watumishi 10, 295 walioondolewa kwenye mfumo
kuanzia Machi 15 hadi Aprili 30 mwaka huu.
Alisema pia kuwa watumishi hewa 1,951 wameongezeka ikiwa ni pamoja na Sh bilioni 1.8.
Alifafanua
kuwa ofisi hiyo ilitoa maelekezo kwa Makatibu Wakuu, Wakuu wa taasisi
za umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa, kuwasilisha taarifa ya
watumishi hewa ifikapo Juni 10, mwaka huu.
Chanzo: Mtanzania
Jumapili, 19 Juni 2016
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)