ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Ijumaa, 5 Mei 2017

Sakata la Vyeti Feki laongeza uhaba wa watumishi katika idara mbalmbali

 
Uamuzi  wa Serikali wa kuwafukuza kazi watumishi wanaodaiwa kughushi vyeti, umezidi kuchukua sura mpya, baada ya watumishi sita wa Halmashauri ya Kilwa mkoani Lindi kufungwa jela mwaka mmoja kila mmoja kwa kosa la kughushi vyeti vya kidato cha nne na kujipatia ajira.

Taarifa nyingine zinasema Katibu Tawala wa Wilaya ya Tandahimba (DAS), Mohamed Azizi naye ameguswa na sakata la vyeti feki baada ya kutajwa katika orodha ya watumishi wenye vyeti feki akiwa namba 5356.

Chanzo cha uhakika kutoka ofisi ya DAS kimesema  kuwa, tayari kiongozi huyo ameshaondoka Mtwara kuelekea Dar es Salaam kupeleka malalamiko yake katika mamlaka za juu kwamba jina lake limeingizwa kimakosa katika orodha hiyo.

Taarifa nyingine kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Vijijini zinasema zahanati mbili zimefungwa baada ya watumishi wote waliokuwapo kukumbwa na sakata la vyeti feki.

Madereva hao, walihukumiwa jana na Mahakama ya Wilaya  ya Kilwa, baada ya kupatikana na hatia ya makosa matatu ya kufoji vyeti vya kidato cha nne.

Hukumu hiyo, imetolewa na Hakimu wa Mahakama hiyo, Gabriel Ngaeje baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

Madereva waliohukumiwa ni Juma Sungura, Issa Juma Abdurahamani, Abdull Chubi, Dactuce, Ahamadi Selemani na Abdallah Kilolopera.

Kabla ya kutolewa hukumu hiyo, Hakimu Ngaeje aliwauliza washtakiwa kama wana sababu zitakazoishawishi mahakama isiwape adhabu kali.

Kila mmoja kwa wakati wake, aliomba mahakama iwaonee huruma, kwani wana familia zinazowategemea, hivyo iwapo watapewa adhabu kali kuna hatari ya kukosa matunzo yao.

Naye mwanasheria wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Emmanuel Camilius aliiomba mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa watuhumiwa na watu wengine wenye tabia ya aina hiyo ndani ya Mkoa wa Lindi na Taifa kwa ujumla.

“Tabia ya aina hii si ya kuifumbia macho, kazi wanazozifanya zinahusu usalama wa watu, kugushi vyeti kwa ajili ya kujipatia ajira ni hatari,”alisema Camulius.

Hakimu Ngaeje, akitoa hukumu katika kesi hiyo namba 07/2014, alisema amesikiliza maombi ya pande zote mbili, hivyo akawahukumu kila mmoja kifungo cha nje cha miezi (12) kwa kila kosa na kufanya idadi ya miezi (196).

“Kwa vile adhabu inakwenda pamoja, mtatumikia kifungo cha nje miezi 12,”alisema.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo na mwanasheria Camilius, kuwa  watumishi hao wakijua wanachokifanya ni makosa, walifoji vyeti vya kidato cha nne na kujipatia ajira kinyume na sheria ya nchi.

Naye Mbunge wa  Mchinga, Hamidu Bobali (CUF), alisema  zahanati mbili katika Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Vijijini mkoani Lindi, zimefungwa baada ya watumishi wake kutajwa katika orodha ya watumishi wa umma wenye vyeti feki.

Bobali alitoa taarifa hiyo bungeni mjini Dodoma  jana, alipokuwa akichangia bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwa mwaka wa fedha 2017/18.

“Mheshimiwa mwenyekiti, hili suala la vyeti feki limeleta shida katika Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Vijijini kwa sababu kuna zahanati mbili zimefungwa, baada ya watumishi wake wote kubainika wana vyeti feki.

“Kwa hiyo, namwomba mheshimiwa waziri, achukue hatua haraka,” alisema Bobali wakati alipokuwa akihitimisha mchango wake.

Pamoja na kusema hayo bungeni, nje ya bunge Bobali alisema a zahanati zilizofungwa ziko katika Jimbo la Mtama katika Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Vijijini.

“Zahanati zilizofungwa ni za Mkanga 2 na Sudi ambazo zote ziko pembezoni kabisa ya mji, kiasi kwamba kitendo cha kuzifunga, kitaathiri mno wananchi.

“Kwa hiyo, ndiyo maana nilimwomba mheshimiwa waziri afanye kila analoweza kuhakikisha zinafunguliwa haraka ili kunusuru maisha ya wananchi,”alisema Bobali.

Kwa mujibu wa Bobali, zahanati hizo zilikuwa na watumishi watatu watatu kila moja.

Taarifa zaidi kutoka Lindi, zinasema watumishi  236 wa Serikali wamegundulika kutumia vyeti feki.

Katika sakata hilo, halmashauri za wilaya za Nachingwea na Kilwa zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Mkoa  wa Lindi, Godfrey Zambi alizitaja wilaya na idaidi ya watumishi kwenye mabano, kuwa ni Nachingwea (72), Kilwa (53), Ruangwa (45),Lindi Vijijini (25), Ofisi ya Katibu Tawala (RAS) (23), Manispaa (11) na Liwale (7).

Alisema  katika idadi hiyo, idara za afya na elimu  zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watumishi wa vyeti feki.

Magazeti ya Leo ijumaa ya tarehe 05/05/2017