Uamuzi
wa Serikali wa kuwafukuza kazi watumishi wanaodaiwa kughushi vyeti,
umezidi kuchukua sura mpya, baada ya watumishi sita wa Halmashauri ya
Kilwa mkoani Lindi kufungwa jela mwaka mmoja kila mmoja kwa kosa la
kughushi vyeti vya kidato cha nne na kujipatia ajira.
Taarifa
nyingine zinasema Katibu Tawala wa Wilaya ya Tandahimba (DAS), Mohamed
Azizi naye ameguswa na sakata la vyeti feki baada ya kutajwa katika
orodha ya watumishi wenye vyeti feki akiwa namba 5356.
Chanzo
cha uhakika kutoka ofisi ya DAS kimesema kuwa, tayari kiongozi huyo
ameshaondoka Mtwara kuelekea Dar es Salaam kupeleka malalamiko yake
katika mamlaka za juu kwamba jina lake limeingizwa kimakosa katika
orodha hiyo.
Taarifa
nyingine kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Vijijini zinasema
zahanati mbili zimefungwa baada ya watumishi wote waliokuwapo kukumbwa
na sakata la vyeti feki.
Madereva
hao, walihukumiwa jana na Mahakama ya Wilaya ya Kilwa, baada ya
kupatikana na hatia ya makosa matatu ya kufoji vyeti vya kidato cha nne.
Hukumu
hiyo, imetolewa na Hakimu wa Mahakama hiyo, Gabriel Ngaeje baada ya
kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.
Madereva waliohukumiwa ni Juma Sungura, Issa Juma Abdurahamani, Abdull Chubi, Dactuce, Ahamadi Selemani na Abdallah Kilolopera.
Kabla
ya kutolewa hukumu hiyo, Hakimu Ngaeje aliwauliza washtakiwa kama wana
sababu zitakazoishawishi mahakama isiwape adhabu kali.
Kila
mmoja kwa wakati wake, aliomba mahakama iwaonee huruma, kwani wana
familia zinazowategemea, hivyo iwapo watapewa adhabu kali kuna hatari ya
kukosa matunzo yao.
Naye
mwanasheria wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),
Emmanuel Camilius aliiomba mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho
kwa watuhumiwa na watu wengine wenye tabia ya aina hiyo ndani ya Mkoa wa
Lindi na Taifa kwa ujumla.
“Tabia
ya aina hii si ya kuifumbia macho, kazi wanazozifanya zinahusu usalama
wa watu, kugushi vyeti kwa ajili ya kujipatia ajira ni hatari,”alisema Camulius.
Hakimu
Ngaeje, akitoa hukumu katika kesi hiyo namba 07/2014, alisema
amesikiliza maombi ya pande zote mbili, hivyo akawahukumu kila mmoja
kifungo cha nje cha miezi (12) kwa kila kosa na kufanya idadi ya miezi
(196).
“Kwa vile adhabu inakwenda pamoja, mtatumikia kifungo cha nje miezi 12,”alisema.
Awali
ilidaiwa mahakamani hapo na mwanasheria Camilius, kuwa watumishi hao
wakijua wanachokifanya ni makosa, walifoji vyeti vya kidato cha nne na
kujipatia ajira kinyume na sheria ya nchi.
Naye
Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF), alisema zahanati mbili katika
Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Vijijini mkoani Lindi, zimefungwa baada
ya watumishi wake kutajwa katika orodha ya watumishi wa umma wenye vyeti
feki.
Bobali
alitoa taarifa hiyo bungeni mjini Dodoma jana, alipokuwa akichangia
bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
kwa mwaka wa fedha 2017/18.
“Mheshimiwa
mwenyekiti, hili suala la vyeti feki limeleta shida katika Halmashauri
ya Wilaya ya Lindi Vijijini kwa sababu kuna zahanati mbili zimefungwa,
baada ya watumishi wake wote kubainika wana vyeti feki.
“Kwa hiyo, namwomba mheshimiwa waziri, achukue hatua haraka,” alisema Bobali wakati alipokuwa akihitimisha mchango wake.
Pamoja
na kusema hayo bungeni, nje ya bunge Bobali alisema a zahanati
zilizofungwa ziko katika Jimbo la Mtama katika Halmashauri ya Wilaya ya
Lindi Vijijini.
“Zahanati
zilizofungwa ni za Mkanga 2 na Sudi ambazo zote ziko pembezoni kabisa
ya mji, kiasi kwamba kitendo cha kuzifunga, kitaathiri mno wananchi.
“Kwa
hiyo, ndiyo maana nilimwomba mheshimiwa waziri afanye kila analoweza
kuhakikisha zinafunguliwa haraka ili kunusuru maisha ya wananchi,”alisema Bobali.
Kwa mujibu wa Bobali, zahanati hizo zilikuwa na watumishi watatu watatu kila moja.
Taarifa zaidi kutoka Lindi, zinasema watumishi 236 wa Serikali wamegundulika kutumia vyeti feki.
Katika sakata hilo, halmashauri za wilaya za Nachingwea na Kilwa zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi
alizitaja wilaya na idaidi ya watumishi kwenye mabano, kuwa ni
Nachingwea (72), Kilwa (53), Ruangwa (45),Lindi Vijijini (25), Ofisi ya
Katibu Tawala (RAS) (23), Manispaa (11) na Liwale (7).
Alisema katika idadi hiyo, idara za afya na elimu zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watumishi wa vyeti feki.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni