Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Mhe. Lee Nak-yon atafanya ziara ya kikazi
nchini kwa mwaliko wa mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), kuanzia tarehe 21 hadi
23 Julai 2018. Ziara hiyo itakuwa ya kwanza kufanywa na kiongozi wa
ngazi ya juu kutoka Jamhuri ya Korea tangu nchi zetu mbili zianzishe
mahusiano ya kidiplomasia mwaka 1992.
Madhumuni
ya ziara hiyo ni kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa kidiplomasia
kati ya nchi hizo mbili na kufungua zaidi fursa za ushirikiano wa
kibiashara na kiuchumi katika ngazi na sekta mbalimbali. Mhe. Waziri
Mkuu Lee atafuatana na ujumbe mzito wa maafisa wa Serikali, wabunge na
wafanyabiashara wakubwa. Ujumbe wa wafanyabiashara utakaoongozana na
Mhe. Lee unatarajiwa kukutana na wenzao wa Tanzania katika Mkutano wa
Pili wa Jukwaa la Wafanyabiashara uliopangwa kufanyika jijini Dar es
Salaam tarehe 23 Julai 2018. Mkutano wa kwanza ambao ulikuwa na
mafanikio makubwa ulifanyika Seoul mwezi Februari 2018.
Mhe.
Lee Nak-yon atawasili nchini saa kumi na mbili na nusu jioni (12:30) ya
tarehe 21 Julai 2018 na atapokelewa na mwenyeji wake Mhe. Kassim
Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Siku inayofuata, Waziri Mkuu Lee na mwenyeji wake Mhe. Kassim Majaliwa
Majaliwa (Mb.), watafanya mazungumzo rasmi jijini Dar es Salaam na
baadaye watashuhudia uwekaji saini wa mkataba wa kuondoa hitaji la visa
kwa wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za utumishi (diplomatic
and official/service passport). Aidha, Mhe. Lee atakutana na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli
kwa ajili ya kusalimiana.
Jamhuri
ya Korea ni mshirika mkubwa wa maendeleo wa Tanzania ambapo kupitia
Shirika la Kimataifa la Maendeleo (KOICA) na Mfuko wa Ushirikiano wa
Uchumi na Maendeleo (EDCF) yamekuwa yakitoa misaada na mikopo mingi ya
masharti nafuu kwa Tanzania ikiwemo misaada ya fedha katika bajeti,
ujenzi wa miundombinu ya jamii, mafunzo ya muda mfupi na mrefu,
wataalamu mbalimbali wa kujitolea, vifaa na mashine kwa ajili ya sekta
mbalimbali ikiwemo ya afya.
Baadhi
ya miradi ambayo imegharamiwa na Serikali ya Korea ni pamoja na Mradi
wa kuboresha Huduma ya Mama na Mtoto katika Hospitali ya Chanika, Mradi
wa Mfumo wa Usajili wa Meli na Mabaharia kwa Njia ya Mtandao Zanzibar,
Mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Taifa ya Taaluma na Tiba (MUHAS) kampasi
ya Mloganzila na ujenzi wa daraja katika mto Malagarasi.
Vile
vile, Korea ni mshirika mkubwa katika kusaidia maendeleo ya Bara la
Afrika ambapo hivi karibuni katika mkutano wa Sita wa Jukwaa la
Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea na Africa (KOAFEC VI) uliofanyika
mwezi Mei 2018, Busan, Korea ambapo Serikali ya Korea ilitangaza msaada
wa Dola za Marekani bilioni 5 kwa ajili ya Bara la Afrika kwa kipindi
cha mwaka 2018/2020. Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazonufaika na
msaada huo.