RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ameteua wanasiasa saba kuwa
wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakiwamo watatu waliowania Urais wa
Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa marudio wa Machi 20, mwaka huu.
Hao ni aliyekuwa mgombea wa nafasi ya urais wa chama cha ADC, Hamad
Rashid Mohammed, Said Soud Said aliyewania nafasi ya urais kupitia AFP
Wakulima na Juma Ali Khatib wa ADA-TADEA.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari, wengine
walioteuliwa ni Balozi Ali Karume, Waziri wa zamani wa Fedha na Uchumi
katika Serikali ya Rais mstaafu Dk Salmin Amour, Balozi Amina Salum Ali
pamoja na Mohamed Aboud Mohamed aliyekuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais.
Pia yumo Mouldine Castico ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika hotuba yake ya uzinduzi wa Baraza la Wawakilishi, Rais Shein
aliahidi kuunda serikali itakayovishirikisha vyama vya siasa kwa ajili
ya kuleta maendeleo ya wananchi wote bila ya kujali itikadi za kisiasa.
Rais Dk. John Magufuli leo anatarajia kuondoka nchini kuelekea
Rwanda, ikiwa ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu aapishwe kuingia
madarakani Novemba 5, mwaka jana.
Taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, ilieleza kuwa katika ziara hiyo
Rais Magufuli na mwenyeji wake Rais Paul Kagame wanatarajia kufungua
daraja la kimataifa la Rusumo na kituo cha pamoja cha ukusanyaji ushuru
mpakani, ambacho ni moja ya miradi muhimu iliyoanzishwa kwa hisani ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Miundombinu hiyo ambayo ipo katika mpaka wa Tanzania-Rwanda, ni
muhimu si tu katika kurahisisha mchangamano baina ya nchi hizi mbili,
bali pia kuunganisha zaidi ardhi zisizo na bahari katika mataifa ya
Afrika Mashariki na Kati na Bahari ya Hindi.
Baada ya sherehe ya ufunguzi, viongozi hao wawili wataelekea mjini
Kigali, ambako watafanya mazungumzo pamoja na kuweka shada la maua
kuadhimisha kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Kama mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ziara ya
kwanza ya kigeni ya Rais Magufuli katika eneo hilo pia inaashiria
dhamira yake ya kupanua mchakato wa uchangamano na kuimarisha uhusiano
baina ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Rais Magufuli ambaye staili yake ya kubana matumizi na vita dhidi ya
ufisadi, maarufu kama ‘utumbuaji majipu’ imeteka vyombo vya habari
duniani, ataanza ziara hiyo ya siku mbili kwa kufungua kituo cha mpakani
cha Rusumo.
Baada ya ufunguzi wa kituo hicho cha pamoja cha ukusanyaji ushuru,
ambacho kinaunganisha mataifa haya mawili jirani, atafanya mkutano na
waandishi wa habari akiwa na mwenyeji wake Rais Kagame.
Katika siku yake ya pili ya ziara hiyo ya kikazi kesho, Rais Magufuli
ataungana na Wanyarwanda kote duniani kuadhimisha miaka 22 ya mauaji ya
kimbari dhidi ya Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani.
Siku hiyo ambayo Wanyarandwa huomboleza vifo vya watu zaidi ya
milioni moja vilivyotokea mwaka 1994, wengi wao wakiwa Watutsi, Rais
Magufuli na mwenyeji wake Kagame pamoja na wake zao wataweka mashada ya
maua na kuwasha mishumaa ya kumbukumbu.
Baada ya tukio hilo, Dk. Magufuli ataungana na Wanyarwanda katika
matembezi yajulikanayo kama ‘Walk to Remember’ maalumu kwa kumbukumbu ya
mauaji hayo na kuwasaidia walionusurika kabla ya kuhudhuria mkesha
kwenye Uwanja wa Taifa wa Amahoro mjini Kigali.
Rais Magufuli amekuwa akitumia muda mwingi akiwa Ikulu Dar es Salaam
kwa shughuli za utendaji kazi kwa Serikali yake na alisafiri mara chache
nje ya jiji hilo kwenda mikoa ya Dodoma, Arusha, Mwanza, Morogoro,
Singida na Geita.
WAFAMASIA wawili, mmoja wa hospitali ya
rufaa ya mkoa wa Iringa na mwingine wa hospitali ya wilaya ya Mufindi pamoja na
watuhumiwa wengine wawili waliokuwa viongozi wa kijiji cha Ilula Mwaya wilayani
Kilolo wamefikishwa mahakamani kati ya Januari na Machi mwaka huu wakituhumia
kwa makosa mbalimbali ya rushwa.
Akitoa taarifa ya utendaji kazi ya
kipindi hicho, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa
wa Iringa, Eunice Mmari alisema watuhumiwa hao wanne wamefikishwa mahakamani
kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.
Aliwataja wafamasia hao kuwa ni Lucas
Mwandi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa na Selemani Fulano wa hospitali
ya wilaya ya Mufindi, na Deogratias Vangiliasas aliyekuwa Mwenyekiti wa kijiji
cha Ilula Mwaya na Robert Kisaka aliyekuwa afisa mtendaji wa kijijiji hicho.
Azungumza na wanahabari ofisini kwake
jana, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa
Iringa, Eunice Mmari alisema wafamasia hao wanashitakiwa kupitia kesi namba 53/2016
na kesi namba 39/2016 kwa makosa ya wizi wa mali ya umma wakiwa mtumishi wa
umma kinyume na kifungu cha 270 cha sheria ya kanuni ya adhabu iliyorekebishwa
mwaka 2002.
Kuhusu waliokuwa viongozi wa kijiji
hicho, alisema nao wanashitakiwa kwa makosa ya wizi wa mali za umma kupitia
kesi namba 23/2016, kinyume na sheria hiyo ya rushwa kifungu namba 28, 29, 30
na 31.
Mmari alisema katika kipindi hicho cha
Januari hadi Machi, Takukuru pia imepokea malalamiko 28 ya rushwa na 14 kati
yake yamefunguliwa majadala ya uchunguzi, malalamiko tisa yanafanyiwa uchunguzi
wa awali, huku malalamiko matano yakifungwa baada ya kukosekana kwa ushahidi.
Alikitoa mchanganuo wa mamalamiko hayo
alisema afya iliongoza kwa kuwa na malalamiko saba, serikali za mitaa, vijiji
na kata (6), elimu (3), ardhi (2), sekta binafsi (1), Tanroads (1), Ushirika na
Kilimo (2), Polisi (1), Ujenzi (1) na sekta binafsi (2).
Akizungumzia mwamko wa wakazi wa mkoa wa
Iringa kuyaripoti matukio ya rushwa katika taasisi yao, Mmari alisema; “mwamko
ni mdogo sana ikilinganishwa na mikoa mingine.”
Alisema Takukuru inaamini kuwepo kwa
makosa mengi yanayoangukia katika sheria ya rushwa lakini yemekuwa hayaripotiwi
katika taasisi yao jambo linalowaathiri wananchi wenyewe na uchumi wa Taifa.
Aliwataka wananchi hao kutoa taarifa kwao
wakati wowote wanapokosa huduma baada ya kudaiwa rushwa au pale wanapobaini
miradi ya maendeleo katika maeneo yanayowazunguka inafanywa chini ya kiwango.
Kwa kupitia elimu kwa umma, Mmari alisema
wananchi 4,957 wamepatiwa elimu ya rushwa katika kipindi hicho, wakiwemo
wanafunzi 3,693.
Alisema ofisi yao pia imefanya vikao
vinne vya kujadili dhibiti zilizofanyika ili kuziba mianya ya rushwa katika
usimamizi wa mali za vijiji, zabuni ya ununuzi wa pampu ya kusukuma maji katika
mji wa Mafinga, ajira za vibarua katika mamlaka ya maji Mafinga na taratibu za
kuchukua walimu wa kujitolea shule za msingi za mjini Iringa.
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesisitiza kuwa kitaendelea na juhudi za
kutafuta haki yake kwa njia yoyote, lakini ya amani ambayo itaungwa
mkono na wananchi wa Zanzibar na kwa kuanzia wametangaza kutoitambua
Serikali itakayoundwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad aliwataka wananchi na
wafuasi wa chama hicho kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho alisema
CUF ipo katika juhudi za kutafuta haki wanayodai ilitokana na kushinda
katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana ambao ulifutwa na Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Maalim Seif alisema hayupo tayari kukaa meza moja na Dk Shein kwa ajili ya kutafuta suluhu ya Zanzibar.
“Sipo tayari kukutana na Shein Ikulu kwa ajili ya mazungumzo ya
kuleta amani na utulivu Zanzibar...... nitakutana na yeye kama nani kwa
sababu sisi CUF hatutambui ushindi wa Shein katika uchaguzi wa marudio
pamoja na serikali yake,” alisema Maalim Seif aliyekuwa Makamu wa Kwanza
wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Aidha, Baraza Kuu la CUF limepitisha maazimio ya kuunga mkono uamuzi
wa Marekani kuinyima Tanzania msaada kupitia Shirika la Changamoto za
Milenia (MCC) hivi karibuni.
Kwa upande wake, Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimeipongeza
Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa juhudi zake ikiwemo kuiunga
mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika juhudi zake za kuleta
maendeleo kwa wananchi wake na miradi ya maendeleo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai aliwaambia waandishi
wa habari jana kuwa Serikali ya Watu wa China ni miongoni mwa nchi
marafiki makubwa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara
baada ya nchi mbili kuwa Jamhuri viongozi wake walikuwa marafiki wakubwa
wakitembeleana na kubadilisha wataalamu.
RAIS John Magufuli ameahirisha shamrashamra za maadhimisho ya siku ya
Muungano na hivyo kuwezesha kuokoa zaidi ya Sh bilioni mbili,
alizoagiza zikaanzishe upanuzi wa barabara inayokwenda Uwanja wa Ndege
wa Mwanza.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari kutoka Chato
mkoani Geita ambako Dk Magufuli yuko mapumzikoni nyumbani kwake, Rais
ameelekeza siku hiyo itakuwa ya mapumziko kama kawaida, na Watanzania
waiadhimishe wakiwa majumbani kwao ama katika shughuli zao binafsi.
Sherehe za Muungano huadhimishwa kila Aprili 26 kusherehekea kuzaliwa
kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ilianzishwa Aprili 26, 1964
baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“Kufuatia kuahirishwa kwa shamrashamra hizo, Rais Magufuli ameelekeza
kuwa fedha zilizopangwa kutumika kwa ajili ya kugharamia vinywaji,
vyakula, gwaride, halaiki, burudani mbalimbali na hafla ya usiku ambazo
ni zaidi ya shilingi bilioni mbili, zitumike kuanzisha upanuzi wa
barabara ya “Mwanza - Airport” katika eneo linaloanzia Ghana Quaters
hadi Uwanja wa Ndege wa Mwanza,” ilieleza taarifa ya Ikulu kutoka Chato.
“Barabara hiyo inafanyiwa upanuzi ili kukabiliana na kero ya
msongamano mkubwa wa magari ambao unaathiri shughuli za kila siku za
wananchi,” ilifafanua taarifa hiyo ya Ikulu.
Tangu aingie madarakani, Rais Magufuli alieleza azma ya Serikali yake
ya Awamu ya Tano kubana matumizi na katika hatua alizochukua ni kufuta
safari za nje ya nchi zisizo na tija, mikutano na makongamano, pamoja na
kuahirisha sherehe mbalimbali na kuelekeza fedha zake katika masuala ya
huduma za jamii.
Aliahirisha sherehe za Siku ya Uhuru, Desemba 9, mwaka jana na
kutangaza siku hiyo kuwa ya kufanya usafi nchi nzima ili kukabiliana na
ugonjwa wa kipindupindu katika dhana ile ya Uhuru ni Kazi.
Rais Magufuli aliagiza fedha zilizokuwa zitumike kwa sherehe hizo, Sh
bilioni nne zikatumike kwa ajili ya upanuzi wa Barabara ya Bagamoyo
kutoka Mwenge-Morocco, Dar es Salaam yenye urefu wa kilometa 4.3.
Aidha, Rais Magufuli alisitisha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi
Kitaifa, ambayo yalikuwa yafanyike kitaifa mkoani Singida, Desemba mosi,
mwaka jana.
Badala yake, aliagiza fedha zote ambazo zilitengwa na serikali pamoja
na wahisani mbalimbali kwa ajili ya maadhimisho hayo, zielekezwe
kununua vifaa tiba na vitendanishi. Serikali ilitenga kiasi cha Sh
milioni 18 kwa ajili ya maadhimisho hayo huku kila mshiriki katika
maonesho hayo akichangia kiasi cha Sh 500,000.
Awali Rais Magufuli aliagiza fedha zilizotengwa kwa ajili ya hafla ya
uzinduzi wa Bunge zaidi ya Sh milioni 225, ziende kununulia vitanda kwa
ajili ya wagonjwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu mstaafu wa Kenya, Raila Odinga amerejea
nchini Kenya baada ya kumaliza mapumziko yake ya siku tatu Lubambangwe
katika Kijiji cha Mlimani, Wilaya ya Chato mkoani Geita alikomtembelea
Rais Magufuli aliyepo mapumzikoni.
Akizungumza kwenye Uwanja wa Michezo wa Shule ya Sekondari ya Chato
kabla ya kuruka kwa helikopta, Raila alimshukuru rafiki yake Rais
Magufuli kwa kumpokea na pia aliwashukuru wananchi wa Chato kwa ukarimu
wao kwa wageni.
Pia alisema ana imani kuwa Rais Magufuli ataisaidia Tanzania
kukabiliana na changamoto mbalimbali, ikiwemo umasikini unaowakabili
wananchi wake. “Lakini mimi najua yeye mwenyewe ana maono, anaona mbele
na anajua yale ambayo yanatakiwa yafanyike ili Tanzania iinuke, itoke
katika hali ya ufukara na kuwa katika hali ya maendeleo zaidi,” alisema
Raila.
Raila na mkewe, Mama Ida Odinga waliwasili Chato, Jumamosi iliyopita
kwa mapumziko na kuisalimia familia ya Rais Magufuli ambayo ni familia
rafiki.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameahidi kutoa madawati na
vitabu kwa wanafunzi wa shule tatu za msingi zilizopo Chato, ambao
walijitokeza Uwanja wa Sekondari wa Chato wakati Rais Magufuli akimuaga
mgeni wake Waziri Mkuu mstaafu wa Kenya, Raila Odinga.
kuna mashirika mbalimbali ambayo yameamua kwa namna moja kusaidia jitihada za elimu hasa kwa wafunzi wa kike katika shule za misingi lakini leo tunajiuliza je misaada inayotolewa ina tija kwa wanafunzi wenyewe?
au ndo inasaidia kuwafaidisha baadhi ya wadau waliopo katika mashirika hayo kama wakurugenzi wa mashirika, walimu na viongozi mbalimbali wa shule?
Kupitia maswali haya ndipo tulipoamua kutuma watafiti wetu katika shule mbalimbali hasa katika shule za sekondary za wilaya ya kilolo na kubaini uwepo wa madudu makubwa hasa kwa walimu wanaohusika na utoaji wa pesa mbalimbali kwa wanafunzi waliofadhiliwa na mradi huu wa CAMFED;
- Pesa nyingi zinazotolewa na wafadhili zimebainika kuishia kwa walimu walezi na kile kidogo kinachobaki ndicho wanafunzi hudanganywa kwa kununuliwa daftali au kupewa vifaa vya kujifunzia wafadhiliwa katika mradi huu kutoka shule fulani walisema" ni kwel CAMFED ina tufadhili kwa kutulipia ada na mahitaji mbalimbali ila hapa shuleni kwenu anaefaidi sana ni mwalimu wetu maana mara nyingine huwa wanatulazimisha tusaini hela elfu 80,000/= afu si tunapewa elfu thelathini (30,000/=) tukiuliza wanasema wanakata hela kwaajili ya matumizi ya shule".
mwandishi wetu hakuishia hapo alijaribu kuwadodosa baadhi ya walimu wanaohusika na mradi huo ambao walishindwa kabisa kujieleza na kutoa ushirikiano kwa kudai hayo ni mambo ya kitaasisi" haya ni mambo ya kitasisi sisi kama shule tuna utaratibu wetu wa kutoa pesa ambao humwekea akiba mwanafunzi" alisema mwalimu.
vile vile CAMFED hutoa misaada mbalimbali ya vitabu vya kujifunzia kwa wanafunzi ambavyo mara nyingi hufanya wakuu wa shule watumie vitabu hivyo kana kwamba wametumia bajeti ya shule
Hiyo ni baadhi ya vitabu vilivotolewa na CAMFED kwa shule mbalimbali wilaya ya kilolo
Afisa Miradi wa CAMFED Tanzania, Christina Kyaruzi akizungumza na
baadhi ya wakuu wa shule za sekondari zilizoko katika wilaya ya kilolo
baada ya kukabidhi vitabu katika shule hizo. Kushoto kwake Mwalimu mkuu
wa shule ya Sekondari Ilula
Afisa Miradi wa CAMFED Tanzania, Christina Kyaruzi akionyesha moja ya
vitabu ambavyo amekibadhi kwa shule 22 za wilaya ya Kilolo halfa
zilizofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari Ilula.
Afisa Miradi wa CAMFED Tanzania, Christina Kyaruzi akimkabidhi
Mwenyekiti Huduma za Jamii wa Halmashauri ya wilaya Kilolo, Anna Kulanga
moja ya mfano wa vitabu walivyokabidhi katika shule za sekondari wilaya
ya Njombe.
Afisa Miradi wa CAMFED Tanzania, Christina Kyaruzi akiwa katika picha
ya pamoja na baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari ya Ilula.
Afisa Miradi wa CAMFED Tanzania, Christina Kyaruzi mwenye nguo ya njano
akiwa na walimu wa shule za sekondari zilizopatiwa msaada wa vitabu
kutoka shirika la CAMFED.(Picha zote na Denis Mlowe)
Baadhi ya Maboksi ya Vitabu yaliyokabidhiwa kwa shule 22 zilizoko wilaya ya kilolo.
Na Denis Mlowe,Ilula
Katika kuhakikisha kiwango cha elimu nchini kinakua,shirika lisilo la
Kiserikali la Campaign for Female Education (CAMFED) chini ya mpango
wake kuwasomesha watoto wa kike kilitoa misaada ya vitabu 54,935 kwa
shule 22 za sekondari zilizoko katika wilaya ya Kilolo mkoani Iringa
vyenye thamani ya shilingi milioni 55.
Alipoongea wakati wa halfa ya kukabidhi vitabu iliyofanyika katika Shule
ya Sekondari Ilula mwishoni mwa mwaka juzi mgeni rasmi Mwenyekiti Huduma za
Jamii wa Halmashauri ya wilaya Kilolo, Anna Kulanga alilishukuru shirika
hilo kwa msaada huo kwa kuweza kuwafikia wanafunzi wa shule za Iringa
vijijini.
“Tumefurahi sana kupata vitabu mbalimbali kwani shule ya sekondari za
hapa zina changamoto ya upungufu wa vitabu hasa vya sayansi na
kulifanya somo hilo kuwa na wanafunzi wa chache, lakini hivi sasa
kutokana na msaada wa vitabu vilivyo tolewa vitaongeza ufaulu kwa
wanafunzi wetu kutokana na uwingi wa vitabu wenyewe kwa shule
zilizofaidika na msaada huo” alisema Kulanga
Aliwataka walimu na wanafunzi wavitumie vitabu hivi vizuri kwa
kuvitunza kwa lengo la kutumika kwa muda mrefu wakati wa masomo yao na
kuamini kwamba vitabu vivyo vitaleta ufanisi katika kukuza uelewa wa
mwanafunzi katika matumizi sahihi ya lugha ya kiingereza.
Aidha alisema vitabu hivyo vitumike kwa wanafunzi wote kwa wa shule
husika na kuwaasa wanafunzi wa shule zilizofaidika na msaada huo kuacha
tabia mbaya ya kuuza vitabu na kuwataka walimu wa shule hizo kufatilia
kwa makini wanafunzi wote watakaopatiwa vitabu hivyo.
Naye Mwalimu mkuu aliekuwa wa sekondari ya Irole Laurence Maluka alipongea kwa
niaba ya wakuu wa sekondari 22 zilizofaidika na msaada huo wa vitabu
alisema msaada huo wa vitabu utaweza kuwa saidia wanafunzi kuwa na uweza
wa kujisomea zaidi na kuwawezesha kufaulu hadi kwenda chuo kikuu,kwani
hapo awali kulikuwa na changamoto kubwa katika shule zetu ambapo uwiano
ulikuwa kitabu kimoja wanafunzi 5 lakini kwa sasa ni vitabu 5 kwa
mwanafunzi mmoja.
“Ni jambo la kulishukuru sana shirika la CAMFED kwa msaada huu
utapunguza zaidi, kwa kweli huu ni msaada mkubwa katika kuboresha
taaluma na kuinua ufaulu hivyo tunaomba program hii ya shule zetu
iendelee ili kuwafikiwa wanafunzi wengi zaidi katika wilaya ya Kilolo”
alisema Maluka
Kwa upande wake Afisa Miradi wa CAMFED Tanzania, Christina Kyaruzi
amewataka wanafunzi wa sekondari zote wilaya ya Kilolo mkoani Iringa
kuongeza uwezo wa kujisomea ufaulu wa wanafunzi unaongezeka kupitia
msaada unatolewa na shirika hilo.
Alisema vitabu hivi vitunzwe ili viweze kuwafaidisha wanafunzi wengi
kwa kuwa vitaleta faida kwa wanafunzi wengi zaidi katika kujisomea na
kuwataka walimu wakuu wawapatie wanafunzi kila mmoja vitabu vitano na
kwenda navyo nyumbani hadi amalizapo elimu ya sekodari na kuweza
kuvirudisha.
Alizitaja shule zilizofaidika na msaada huo ni shule ya sekondari Ilula,
Nyalumbu, Mazombe, Irole,Lundamatwe, Selebu, Ngangwe, Uhambingeto,
Lukosi, Mlafi Na Ndekwa.
Shule nyingine ni shule za za sekondari za Mtitu, Kilolo,
Lulanzi,Ukwega, Udzungwa, Dabaga, Kitowo, Mawambala, Masisiwe, Madege na
Makwema.