ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Ijumaa, 15 Aprili 2016

TAKUKURU yakabidhiwa Kampuni ya Lugumi


Image result for valentino mlowola
picha :Mkurugenzi Mkuu Takukuru-Valentino Mlowola
Sakata la kampuni ya Lugumi iliyoingia mkataba wa Sh37 bilioni na Jeshi la Polisi wa kufunga mashine za kielektroniki za kuchukua alama za vidole nchi nzima, sasa limetua Takukuru baada ya taasisi ya kupambana na rushwa kuchukua faili lake la usajili.

Kampuni hiyo ilibainika kutotimiza matakwa ya mkataba wake baada ya kufunga mashine 14 tu kati ya 108 ilizotakiwa kufunga, licha ya kulipwa  asilimia 99 ya fedha kwa mujibu wa mkataba.

Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) ya mwaka 2013/14 ndiyo iliyofichua udhaifu huo.

Wakati Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ikitaka nguvu itumike ili Jeshi la Polisi liwasilishe mkataba huo, utata umeibuka katika umiliki wa kampuni hiyo kutokana na kuwepo tuhuma kuwa baadhi ya vigogo wa Polisi na wanasiasa ni wanahisa wa Lugumi Enterprises.

Jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), Frank Kanyusi alisema kuwa Takukuru inashughulikia suala hilo, huku akibainisha kuwa kwa sasa Brela hawana takwimu za kina za kampuni hiyo.

“Kampuni hii ilisajiliwa kihalali na kupewa cheti cha usajili. Ila ninachoweza kukueleza kwa sasa ni kwamba jalada la usajili la Lugumi lipo Takukuru kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” alisema Kinyusi jana.

Kanyusi, ambaye hakutaka kuzungumzia kiundani kuhusu usajili wa kampuni hiyo, alisema: “Waandishi wa habari wamekuwa wakiniuliza maswali mengi kuhusu suala hili ila kwa sasa hali ndiyo hiyo. Jambo hili lipo Takukuru.”

Alisema kwa sasa kampuni zilizosajiliwa na Brela zipo 120,000 na zinakaribia kufika 130,000 na kwamba kampuni lazima zitoe taarifa zake kila mwaka, kinyume na hapo zinaweza kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kufutwa.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Brela zilieleza  kuwa taarifa za usajili wa kampuni hiyo zilitoweka takribani miezi miwili iliyopita.

Mwandishi  alipofika katika ofisi za wakala huyo kwa ajili ya kupata ukweli wa usajili, alielezwa na mmoja wa watumishi ambaye hakutaka jina lake kuwekwa wazi kwamba ni vigumu kupata hilo jalada kwa sababu ya mvutano ulioibuka.

Hata baada ya kufuata taratibu za kupewa jalada hilo kwa ajili ya kupitia masuala mbalimbali, alijibiwa kuwa jalada hilo halionekani ingawa baadaye Kanyusi alisema limechukuliwa na Takukuru.

Sakata la Lugumi liliibuka wiki iliyopita wakati PAC ilipokutana na Jeshi la Polisi kupitia taarifa ya hesabu zao za mwaka 2013/14 zilizokaguliwa na CAG.

Katika hesabu hizo ilibainika kuwa mwaka 2011, Polisi iliingia mkataba na Lugumi kwa ajili ya kufunga mashine hizo katika vituo 108 vya polisi kwa gharama ya Sh 37 bilioni.

Hata hivyo, ilibainika kuwa kampuni hiyo imefunga mitambo hiyo kwenye vituo 14 tu, huku ikilipwa asilimia 99 ya fedha hizo.

Kutokana na ukakasi huo, PAC ambayo ilibaini viashiria vya ufisadi katika mkataba huo, iliagiza watendaji wa Polisi kuwasilisha taarifa za mkataba huo pamoja na vielelezo vyake ili kamati hiyo iweze kuupitia na kujiridhisha.

Lakini hadi sasa Jeshi la Polisi halijawasilisha mkataba huo, jambo ambalo huenda likazua mjadala mkali katika mkutano wa Bunge unaoanza Jumanne ijayo.

Anne kilango malecela atoa ya moyoni

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela, ameibukia kanisani na kutoa ya moyoni, ikiwa siku tano baada ya Rais Dk. John Magufuli kutengua uteuzi wake.

Kilango, Jumatatu wiki hii uteuzi wake ulitenguliwa baada ya Machi 20, mwaka huu, kudai kuwa mkoa wa Shinyanga hauna mtumishi hewa wa serikali hata mmoja.

Hata hivyo, Ikulu ilifanya uchunguzi na kubaini kuwa katika taarifa za awali kuna watumishi hewa 45, huku kazi ya uhakiki ikiendelea katika wilaya za Ushetu na Shinyanga.

Rais Magufuli aliwaagiza wakuu wa mikoa wote, alipokuwa akiwaapisha kuwa wafanya uchunguzi kuhusu uwapo wa watumishi hewa katika mikoa yao na kutoa taarifa.

Kutokana na kutoa taarifa hizo zisizo za kweli, Jumatatu wiki hii, Rais Magufuli alitangaza kutengua uteuzi wake, akiwa amekaa kwenye nafasi hiyo kwa siku 27. Kilango amekuwa mkuu wa mkoa wa 19 tangu kuanzishwa kwa mkoa huo.

Mbali na Kilango, Rais Magufuli pia alimsimamisha kazi Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Abdul Dachi, kutokana na taarifa hizo za kutokuwapo watumishi hewa katika mkoa.

Alivyosema Kanisani
Akiwasalimia waumini wenzake juzi, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria, mjini Shinyanga, baada ya kupewa fursa ya kusema neno, Kilango alisema anamshukuru Mungu kwa kila jambo kwa yote yaliyomtokea.

“Ndugu waumini wenzangu, hili ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu. Hata mtu unapojifungua mtoto akafariki dunia, unamshukuru Mungu kwani hayo ni mapenzi ya Mungu.

"Ukiona mzazi wako kafariki dunia pia, unamshuruku Mungu. Tunao wajibu wa kumshukuru Mungu kwa kila jambo,” alisema kwa maneno mafupi na kisha kuketi, huku akiacha simanzi miongoni mwa waumini wenzake, wakiwamo viongozi wa kanisa.

 
 
 Image result for anne kilango malecela
Alivyoanza Kazi
Mbele ya kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), muda mfupi baada ya kuanza kazi, Kilango alisema Shinyanga ni mkoa wenye changamto nyingi ambazo atazishughulikia, lakini atakuwa akilazimika kukimbia Dar es Salaam kumwona mwenzi wake, Mzee John Malecela ambaye ni mgonjwa, na pindi hali yake ikiimarika wataungana naye mjini Shinyanga.

Hayo aliyasema Machi 22, mbele ya wajumbe wa kikao cha kamati hiyo na Ijumaa Machi 25, alisali kanisani hapo.

Sambamba na hayo, aliahidi kupambana na watumishi wazembe na wale wanaoendekeza rushwa na ufisadi na kurejesha hadhi ya mkoa wa Shinyanga kimaendeleo.

Kilango ambaye yuko mjini Shinyanga, akisubiri kukabidhi ofisi kwa mrithi wake kwa mujibu wa utaratibu, bado anaishi hotelini kwa vile aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Ally Rufunga, hajaondoka katika nyumba ya serikali iliyoko Ikulu ndogo, eneo la Lubaga.

magazeti ya Leo ijumaa ya tarehe 15/04/2016

Magazeti haya yanaletwa kwenu Kwa hisani ya New Mwalimu Education Centre














Jumatano, 13 Aprili 2016

matokeo kati ya yanga na mwaadui

Yanga 2 mwadui1
Azam 1 mtibwa 0

Mrema akumbushia tena ahadi ya kupewa kazi na rais

Image result for agustino mrema
Mwenyekiti wa TLP taifa Dkt. Augustino Lyatonga Mrema amesisistiza ombi lake la kazi kwa kumkumbusha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwamba ampe kazi yoyote amsaidie kibarua kigumu alichonacho cha kuwahudumia wananchi

Dkt. Mrema ameyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na EATV kuhusu miaka 32 ya kifo cha aliyekuwa waziri mkuu wa Tanzania Edward Moringe Sokoine ambaye alihudumu kwenye awamu ya kwanza ya Mwl. Julius Nyerere ambapo alifariki akiwa na cheo cha waziri mkuu tarehe 12.04.1984 kwa ajali ya gari.

''Namkumbuka Sokoine kama mtu wa watu aliyehudumia watu, aliyepambana na ufisadi na magendo .Alikuwa anatenda haki kwa wananchi wote .

"Hata mimi nilipokuwa waziri wa mambo ya ndani na naibu waziri mkuu nilijaribu kufanya kama yeye bahati mbaya sikufanikiwa kama yeye kwa sababu sikuwa waziri mkuu au Rais''- Alisisistiza Mrema.

Kuhusu Mrema kuomba kazi kwa Dkt. Magufuli 
Mrema alisema kwa kutambua rekodi yake ya utendaji kazi wa  Rais Dkt. Magufuli, aliwahimiza wananchi wa Vunjo wamchague kipindi cha kampeni na yeye akampigia kampeni na Rais akawaambia wananchi wa Vunjo kwamba Mrema akikosa ubunge atapangiwa kazi nyingine ndiyo hiyo wananchi wanaulizia.

Aidha Mrema alisema kuna maeneo ambayo yeye anafiti siyo lazima apewe madaraka makubwa 

"Mimi sihitaji ukuu wa mkoa au uwaziri, anipe kazi yoyote na nikionana naye nitamkonyeza maeneo ambayo ninafiti ili nimsaidie kutumbua majipu." Alisema Mrema

Hata hivyo Dkt. Mrema alimpongeza Dkt. Magufuli kwamba ni mtendaji ambaye ameamua bila kusukumwa kupambana na mafisadi na kwamba yeye ni alfa na omega na kazi hiyo ameonyesha kwamba atafanya vizuri kuliko Sokoine na Mrema.

DC, DED Kishapu wamruka Anne Kilango kwa JPM

 Siku moja baada ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango kuvuliwa uongozi kwa kutosema ukweli, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Hawa Ng’humbi ameiruka taarifa ya kutokuwapo kwa watumishi hewa, ambayo amesema ilimshtua alipoiona kwenye televisheni. 
Mkoa wa Shinyanga unaundwa na wilaya tatu ambazo ni Shinyanga, Kishapu na Kahama zinazoundwa na halmashauri sita ambazo ni Kishapu, Manispaa ya Shinyanga, Mji wa Kahama, Ushetu, Msalala na Shinyanga Vijijini. 
Rais John Magufuli juzi alitengua uteuzi wa Kilango, ikiwa ni siku 30 tangu alipotangaza kumteua kwa maelezo kuwa alitoa taarifa isiyo ya kweli kuwa Shinyanga hakuna watumishi hewa kabla ya kujiridhisha.
 Pamoja na Kilango, Rais Magufuli pia alitengua uteuzi wa Katibu Tawala wa Shinyanga, Abdul Dachi, kwa sababu hiyo ya kutoa taarifa za uongo.
 Dk Magufuli alichukua uamuzi huo baada ya kutuma timu mkoani Shinyanga kufanya uhakiki na kubaini kuwa kulikuwa na watumishi hewa 45 katika wilaya moja ya Shinyanga kabla ya kwenda wilaya nyingine za Kahama na Kishapu. 
Akizungumzia sakata hilo jana baada ya uamuzi wa Dk Magufuli, Ng’humbi alisema taarifa za kukosekana watumishi hewa kwenye wilaya yake alizisikia kwenye taarifa ya habari ya televisheni Machi 30 na zilimshtua.
 “Binafsi nilishtuka sana nilipoona ikitangazwa kuwa mkoa mzima wa Shinyanga, hakuna mfanyakazi hewa wakati mimi sikuwa hata nimeona taarifa kutoka wilayani kwangu iliyoandaliwa na uongozi wa halmashauri,” alisema Ng’humbi. 
“Nilijiuliza taarifa imefikaje kwa mkuu wa mkoa bila kupitia kwangu? Kusema kweli nilianza kuifanyia kazi taarifa hiyo na ninatarajia ifikapo Ijumaa nitakamilisha kazi hiyo.” 
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Alphonce Gagambobyaki alisema hadi sasa ofisi yake haijafahamu nani aliyempa mkuu wa mkoa taarifa ya ukaguzi wa wafanyakazi hewa kwa sababu taarifa aliyonayo mezani haijasainiwa.
 “Kuna tatizo la ofisi hii kukaimiwa na zaidi ya watu wanne tangu aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji, Dalikunda Kimulika alipostaafu Februari. Ni vigumu kujua nani alihusika nayo bila kuona saini,” alisema Bagambobyaki. 

Alisema taarifa hiyo inaonekana haikusainiwa kutokana na hofu baada ya watumishi waliobainika kutokuwapo kwenye vituo vyao vya kazi karibu wote kuonekana kuwa na ruhusa maalumu.
“Wakati bado tunajiridhisha kujua ni ruhusa ya aina gani na hawa watumishi wako wapi, ndipo taarifa ilipotangazwa kwamba mkoa hauna watumishi hewa,” alisema.

Hata hivyo, alisema anaamini taarifa sahihi itajulikana baada ya timu maalumu iliyotoka Tamisemi kukamilisha uhakiki wilayani humo jana. 
“Timu ile ya Tamisemi imekwenda mbele zaidi katika uhakiki wake kwa kukagua mtumishi mmoja mmoja hadi vijijini na imekamilisha kazi yake jana,” alisema Bagambobyaki. 

Kuhusu iwapo aliyekuwa mkuu wa mkoa alitumia taarifa zao au la? kaimu mkurugenzi huyo alisema: “Iwapo RC alitumia taarifa zetu au la, hilo siwezi kulisemea kwa sasa.”
Kilango ambaye juzi alisema hakuwa amepata taarifa hivyo asingeweza kuzungumzia kutenguliwa kwake, jana alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kabisa na Dachi akaeleza kuwa ameupokea uamuzi huo kwa kuwa Rais ndiye mteule wake. 
Taarifa ya kutenguliwa kwa watumishi hao wa umma sasa imekuwa kaa la moto kwa wakuu wa wilaya makatibu tawala wao, na wakurugenzi watendaji wa halmashauri za mkoa huo.
Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo za watumishi hewa, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro alisema hawezi kuzungumzia lolote.
“Sisemi lolote na wala sizungumziii mkoa,” alisema na kukata simu ambayo haikupokewa tena. 

Kama ilivyokuwa kwa mkuu wake wa wilaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Shinyanga, Lewis Kalinjuna aligoma kuzungumzia uwezekano wa halmashauri yake kutoa taarifa zilizompotosha Kilango.
“Sitaki kulizungumzia hilo, nawaachia wanaolijua walizungumzie,” alisema Kalinjuna.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Vita Kawawa alikata simu yake mara kadhaa alipopigiwa na baadaye kutuma ujumbe mfupi wa maneno akisema yuko kwenye kikao na kuelekeza atumiwe ujumbe ambao hata alipotumiwa hakujibu.