MAMBO makubwa 10 yaliyojitokeza kwenye mjadala wa Bajeti ya Serikali
kwa mwaka wa fedha 2016/17 pamoja na Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka
2015, yatajibiwa na kutolewa ufafanuzi leo na Waziri wa Fedha na
Mipango, Dk Philip Mpango bungeni.
Moja ya mambo hayo ni hoja ya kufuta au kutofuta kodi kwenye kiinua
mgongo cha wabunge. Kabla ya Dk Mpango kutoa ufafanuzi na marekebisho ya
Bajeti Kuu ya Serikali, kama yatakuwepo na hatimaye kupitishwa au
kutopitishwa kwa kupigiwa kura, mawaziri mbalimbali wanatarajiwa pia
kujibu baadhi ya hoja zilizoelekezwa kwenye wizara zao.
Kutokana na mjadala wa bajeti uliochukua takribani wiki nzima,
wabunge walipendekeza kodi na tozo kadhaa kufutwa ili kuwapunguzia
wananchi mzigo, hatua itakayosababisha serikali kuongeza kodi kwenye
baadhi ya vitu kama itakubaliana na hoja za wabunge. Moja ya eneo
linaloweza kukumbwa na ongezeko la kodi kama serikali kama
wanavyopendekeza wabunge ni petroli.
Alipowasilisha Bajeti ya Serikali Juni 8, Waziri Mpango alisema
serikali haikuongeza kodi yoyote kwenye petroli na dizeli ili
kutowaongezea wananchi mzigo na hofu ya kusababisha mfumuko wa bei.
Kiinua mgongo cha wabunge Wawakilishi hao wa wananchi wamekuwa
wakipinga hatua ya serikali kupendekeza kuwakata kodi ya asilimia tano
kwenye kiinua mgongo chao wanacholipwa kila baada ya miaka mitano,
wakidai kitawaumiza kwa kuwa wao hawalipwi pensheni na kwamba fedha
hizo, mbali na kujikimu, zinawasaidia pia katika kuchangia shughuli
mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwenye majimbo yao.
Takwimu zilizopo zinaonesha kwamba mwaka jana Bunge la 10
lilipovunjwa, kila mbunge alilipwa kiinua mgongo cha Sh milioni 230 na
kama wabunge watalipwa kiasi kama hicho mwaka 2020, kila mbunge
atabakiwa na Sh milioni 218.5 baada ya kukatwa kodi hiyo
wanayoilalamikia.
Mbunge wa Nsimbo, Richard Mbogo (CCM), alidai kwamba hatua ya
kuwakata wabunge kodi kwenye kiinua mgongo inapaswa kuangaliwa upya
kwani wabunge wa Tanzania ndio wanaolipwa mshahara mdogo kulinganisha na
wenzao wa Afrika Mashariki.
Alidai kwamba mbunge wa Kenya analipwa Dola za Marekani 11,000,
Rwanda Dola 9,000, Uganda Dola 8,000, Sudan Kusini Dola 7,000, Burundi
Dola 6,000, wakati wabunge wa Tanzania hulipwa Dola 5,000. Wabunge
wanaona pia kama hatua hiyo ni ya kibaguzi wakisema kama serikali
imefikia uamuzi huo katika kusaka mapato zaidi, basi ni vyema kodi ya
kiinua mgongo iende hadi kwa marais, makamu wa rais, mawaziri wakuu,
maspika na naibu spika na wakuu wa mikoa na wilaya.
Mtazamo huu wa wabunge ni tofauti na walio nao wananchi wengi nje ya
Bunge wakiwemo wasomi ambao wanaamini kwamba wabunge ambao wamekuwa
wakiomba sana maendeleo kwenye majimbo yao, wangekuwa wa kwanza kuonesha
utayari wa kuchangia mapato ya serikali kwa kukubali kukatwa kodi hiyo.
Hata hivyo, wapo wabunge kadhaa wa CCM na karibu wote wa upinzani
wamehiari kukatwa kodi kwenye kiinua mgongo chao.
VAT kwenye utalii Suala la pili lililozungumziwa na wabunge wengi ni
kuitaka serikali kuachana na hatua ya kuanzisha Kodi ya Ongezeko la
Thamani (VAT) ya asilimia 18 kwenye huduma za utalii. Wakati
akiwasilisha hotuba yake ya Bajeti, Dk Mpango alisema kwamba kodi hiyo
ipo pia katika nchi za Kenya, Afrika Kusini na Rwanda. Lakini wabunge
katika mjadala walimpa angalizo Waziri kwamba Kenya imeondoa kodi hiyo
na bila shaka sababu ni kujikuta wakipoteza watalii wengi.
Walisema kama serikali haitaondoa kodi hiyo basi itegemee mpango wa
kuongeza watalii zaidi kutofanikiwa kwani wengi watakimbilia maeneo
yatakayoonekana kutokuwa ghali. CAG aongezewe fedha Suala la tatu
lililozua mjadala mkubwa ni hatua ya serikali kuipunguzia fedha ofisi ya
Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kulinganisha na kiwango
kilichoombwa wakisema hatua hiyo itaifanya ofisi hiyo muhimu katika
kupambana na ufisadi kushindwa kutimiza majukumu yake.
Ofisi hiyo iliomba Sh bilioni 68.8 katika mwaka huu wa fedha ili
itekeleze majukumu yake kwa ufanisi lakini katika bajeti inayopendekezwa
imepewa Sh bilioni 32.3 pekee. Wabunge walisema ofisi hiyo ni chombo
muhimu katika kupeleka ushahidi kwenye Mahakama ya Mafisadi
inayotarajiwa kuundwa mwezi ujao hivyo ni lazima serikali ihakikishe
utendaji wake haukwamishwi na uhaba wa fedha.
Wabunge pia waliitaka serikali kuongeza fedha kwenye miradi ya maji
kwani maji ndio kero kubwa inayowasumbua wananchi wengi na hata wakati
wa kampeni, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alikiri kwamba ndio
kilikuwa kilio kikubwa cha wananchi alichokutana nacho. Walitaka
serikali iongeze Sh 50 kwenye petroli kwa ajili ya miradi ya maji
vijijini sawa na ambavyo imekuwa ikifanyika kwenye mkakati wa kupeleka
umeme vijijini ambao kwa kiwango kikubwa umeleta mafanikio.
TRA na kodi ya majengo Lingine lililozua mjadala mkubwa kwenye
mapendekezo ya serikali katika bajeti yake ni kuhamisha jukumu la
ukusanyaji wa kodi za majengo kutoka katika halmashauri na kupelekwa
katika Mamlaka ya Mapato (TRA). Wabunge waliopinga mpango huo walitaja
sababu zaidi wakidai taarifa walizonazo ni kwamba hata mpango wa
majaribio wa TRA kukusanya kodi za majengo katika mkoa wa Dar es Salaam
haukuzaa matunda makubwa.
Waliokubaliana na pendekezo hilo la serikali nao walitoa angalizo
kwamba kama hatua hiyo itachukuliwa ni lazina kuwe na utaratibu
utakaohakikisha kwamba fedha hizo hazichelewi kupewa halmashauri husika
kwa kuwa zimekuwa zikitegemewa sana kwa shughuli mbalimbali. Takwimu za
mikoa masikini Lingine lililowagawa wabunge ni kuhusu takwimu za mikoa
mitano masikini zaidi nchini na mitano yenye ahueni ambapo baadhi ya
wabunge walizitilia mashaka.
Mbunge mmoja alishangaa kuona mkoa wa Mwanza ukiwa miongoni mwa mikoa
mitano masikini wakati taarifa ya Benki Kuu inaonesha kwamba mkoa huo
ni wa pili katika kuipatia Hazina mapato mengi nyuma ya Dar es Salaam.
Akiwasilisha bungeni Taarifa ya Hali ya Uchumi ya Mwaka 2015, Dk
Mpango alitaja mikoa masikini zaidi kuwa ni Kigoma, Geita, Kagera,
Singida na Mwanza huku yenye ahueni ikiwa ni Dar es Salaam, Kilimajaro,
Arusha, Pwani na Manyara.
Kodi miamala ya simu, mitumba Jambo la saba ambalo wawakilishi hao wa
wananchi walitaka serikali iliangalie kwa mapana yake pia ni kodi
kwenye miamala ya simu na benki. Hofu ya wabunge ilikuwa kwamba kama
kodi hiyo itawekwa bila udhibiti wowote, kampuni, hususan za simu
zitahamishia ‘maumivu’ ya kodi hiyo kwa wananchi.
Lingine ambalo wabunge walililalamikia ni Bajeti inayopendekezwa na
serikali kupandisha ushuru wa nguo na viatu vya mitumba kutoka Dola za
Marekani 0.2 mpaka Dola za Marekani 0.4 kwa kilo. Hatua hiyo ambayo ni
sehemu ya makubaliano ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, inalenga
kudhibiti mitumba ikiwa ni sehemu ya kujiandaa kwa kuzuia kabisa
uingiaji wake.