Mkuu
wa mkoa wa Dar es Salaam amedaiwa kuwatishia kuwafunga jela miezi 6 au
kuwapa tuhuma za dawa za kulevya bila kupitia mahakamani wafanyakazi wa
kituo cha utangazaji cha Clouds kwa kukataa kurusha habari aliyoitaka.
Hayo
yamebainika katika ripoti ya uchunguzi wa tukio la mkuu huyo wa mkoa
kuvamia katika kituo cha utangazaji cha Clouds akiwa na askari wenye
silaha, ripoti ambayo pia imependekeza mamlaka husika kumchukulia hatua
za kinidhamu.
Akiwasilisha
ripoti hiyo kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo mbele ya
wanahabari katika ukumbi wa Habari Maelezo jijini Dar es Salaam,
Mwakilishi wa Kamati ya uchunguzi Deodatusi Balile amesema kamati hiyo
haikuweza kumpata Paul Makonda kwa ajili ya mahojiano.
Akitaja
mambo yaliyobainika katika sakata hilo, Balile amesema kamati hiyo
iliyohoji watu mbalimbali wakiwemo wafanyakazi 14 wa kituo cha Clouds,
imejiridhisha pasipo shaka kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul
Makonda alivamia katika kituo hicho saa 4:30 usiku wa Machi 17 akiwa
anaendesha gari yenye namba za usajili T553 BFH.
Amesema
uchunguzi wa kamati umebaini kuwa sababu ya uvamizi huo ni habari
iliyodaiwa kumuhusu mwanamke aliyedai kuzaa na Mchungaji Josephati
Gwajima ambapo alitaka habari hiyo iruke kwenye kipindi..
Pia
kamati hiyo imethibitisha kuwa Makonda na askari waliingia hadi katika
vyumba ambavyo hawakupaswa kuingia, na waliingia hadi kwenye studio
ambayo inarusha matangazo na kutoa vitisho kwa watangazaji, waandaji na
wafanyakazi wengine, kiasi cha baadhi yao kuagua vilio.
“Vitisho
hivyo ni askari wenye silaha za moto, kuingia ndani ya studio kibabe
wakiwa na silaha za moto, Makonda aliwatisha usiku huo kwamba
angewafunga jela miezi sita, pia angewakagua watangazaji wa kipindi kama
wanahusika na dawa za kulevya, au kuwabana wadhamini wa kipindi na
pengine kuwaingiza kwenye orodha ya wahusika wa dawa za kulevya endapo
wangeendelea na msimamo wao” Amesema Balile
Pia
amesema kamati imebaini kuingiliwa kwa uhuru wa habari kinyume cha
sheria kwa kulazimisha kutangazwa kwa habari isiyokidhi vigezo.
Kuhusu
wafanyakazi kupigwa, Balile amesema kamati hiyo haikuona uthibitisho
wowote kuwa kuna watu walipigwa, isipokuwa wapo waliolia kutokana na
vitisho vya kupelekwa jela miezi 6.
Kamati
hiyo imetoa mapendekezo manne ikiwa ni pamoja kumtaka Makonda aombe
radhi kwa tasnia ya habari, kumtaka Waziri kuwasilisha malalamiko kwa
mamlaka yake ya uteuzi ili hatua zichukuliwe, vyombo vya dola vianzishe
uchunguzi wa ndani dhidi ya askari walioingia.
Amesema
kamati hiyo ilijiridhisha kuwa Makonda hakuwa tayari kuhojiwa wala
kutumia fursa ya kujieleza jambo ambalo hata hivyo halikuathiri
uchunguzi wa kamati hiyo.
"Tulianza
kwa kumpigia simu, lakini hakupokea, tukaamua kumpelekea ujumbe
hakuujibu, tukatumia wasaidizi, wakatutaka tufike ofisini kwake,
tulifanya hivyo, tulifika lakini ilielezwa kuwa ana mgeni, ulipofika
muda akatuita, tukaelekezwa kupita ngazi za mbele lakini yeye akapita
mlango wa nyuma akaondoka. Tukaambiwa tumsubiri, tukasubiri lakini
baadaye tukaambiwa amepata shughuli nyingine kwa hiyo hataweza kurejea
ofisini". Amesema Balile
Mara
baada ya kupokea ripoti hiyo, Waziri Nape amesema ataifikisha katika
mamlaka husika kwa ajili ya hatua kuchukuliwa huku akiwataka wanahabari
kuendelea kuwa na imani na serikali katika kulinda uhuru wa habari.
"Juu
yangu kuna Waziri Mkuu, kuna Makamu wa Rais na kuna Rais, nitawakabidhi
ripoti hii, nawaomba wanahabari, tuendelee kuwa watulivu, Rais wetu
Magufuli ana nia njema na tasnia ya habari na ndiyo maana akaipitisha
haraka sheria inayoipa hadhi tasnia hii... Wakati mwingine madhaifu
yakitokea kwa mtendaji mmoja mmoja, yasiwe tope kwa serikali
nzima....Mimi nitaipeleka taarifa kwa wenzangu, wataiangalia na litakuwa
ni funzo kwa watu wengine" Amehitimisha Waziri Nape