Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akionyesha begi lenye
fomu za kuomba kugombea kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Na Sharon Sauwa, Mwananchi
Waliochukua fomu jana ni Waziri wa Maliasili na
Utalii, Lazaro Nyalandu, kada wa chama hicho, Leonce Mulenda na Ofisa
Mwandamizi mstaafu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Peter Nyalali na kufanya
idadi ya wanaCCM waliokwisha fanya hivyo kufikia 18.
Nyalandu: Ninafahamu changamoto
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Nyalandu
ambaye alisindikizwa na wabunge wa viti maalumu, Mary Chatanda na Martha
Mlata alisema amechukua fomu akifahamu umuhimu wa kuyaendeleza yote
yaliyofanywa na serikali ya awamu ya nne... “Ninafahamu changamoto
zinazotukabili. Nazitazama, naziona hatua ambazo zipo tangu wakati wa
Baba wa Taifa alipomkabidhi kijiti Rais Ali Hassan Mwinyi, Benjamin
Mkapa na Rais Jakaya Kikwete.”
Alisema anafahamu changamoto zinazolikabili Taifa
na anaitazama nchi iendelee kulinda misingi iliyoachwa na waasisi wa
Taifa kwa kuendeleza amani.
Alisema umoja, undugu na mshikamano atakaoulinda, utaifanya Tanzania iwe na nguvu ya kutatua changamoto za sasa na za kesho.
Huku akipigiwa makofi na wapambe wake, Nyalandu
alisema waliambiwa zamani kuwa wazee wanaotawala vyema wanastahili
heshima maradufu.
“Tutaendelea kuwaenzi wazee waliotutawala,
wamekuwa wakitulea katika miji na vijijini, tutaendelea kuwaangalia
vijana na wanawake kwa kuangalia nini ambacho tumefanikiwa katika awamu
hii ya Rais Kikwete. Tutaangalia mageuzi tutakayoyafanya ili kijana wa
Kitanzania aonekane si mzigo,” alisema.
Alisema endapo atafanikiwa kupata nafasi hiyo, serikali yake itajikita katika kuinua uchumi wa nchi.
“Tutajikita katika kuwekeza katika rasilimali
watu, kuwawezesha wananchi kiuchumi… na sisi wenyewe kama Taifa
tutasimama kwa miguu yetu. Tutatembea vichwa vikiwa vimesimama imara
tuishangaze dunia kwa pamoja,” alisema.
Jambo jingine ni kuimarisha vyombo vya ulinzi na
usalama wa nchi kuhakikisha kuwa Taifa linakuwa na uwezo wa kujilinda na
raia wake.
“Tutaendelea kuhakikisha mifumo ya matatizo ikiwa
ni pamoja na magonjwa, tatizo la Ukimwi, mshtuko wa ebola tulioupata
ambao ulitetemesha utalii duniani, changamoto za kigaidi, tutajipanga
kama Taifa na kama umoja kuhakikisha tunakabiliana nazo,” alisema.
Nyalandu alisema njia bora ya kuwawezesha watu ni kuboresha mfumo wa elimu ambao umefanikiwa chini ya Serikali ya Awamu ya Nne.
Alisema endapo atafanikiwa katika safari yake
hiyo ya kuutafuta urais, atahakikisha kila shule ya msingi na sekondari
inakuwa na kitengo cha mafunzo stadi.
Alipoulizwa iwapo chama kingine cha siasa
kitashinda upande wa pili wa Muungano, alisema: “Ni muungano wa mapenzi
ya ndani, ni muungano ambao unazidi tofauti zetu za dini, kabila na
uwepo wa Bara na Visiwani na hali kadhalika, unazidi tofauti zetu za
itikadi za vyama.”
Alisema atashirikiana na viongozi wa Zanzibar katika kuuenzi Muungano wa Tanzania ili uwe ishara ya amani na mshikamano.
Mulenda: Kipaumbele ni elimu bora
Mulenda (41) amechukua fomu ya kuwania kuteuliwa
na chama chake kugombea urais huku akisema kipaumbele chake cha kwanza
ni elimu bora.
Kada huyo ambaye alisindikizwa na watu wasiozidi
sita, alisema kaulimbiu yake ni Serikali sikivu, makini na inayojali
shida za watu.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu ya kuwania
nafasi hiyo katika ofisi za Makao Makuu ya CCM, Mulenda alisema
amejitathmini na kujipima kuwa anaweza kuwa kiongozi wa Tanzania.
Alitaja vipaumbele vingine kuwa ni kuhakikisha CCM inakuwa imara zaidi.
“Kwa upande wa chama nitahakikisha nasimamia kwa
vitendo katiba ya chama, kanuni na taratibu bila kuacha sheria na
miongozo inayoongoza nchi yetu,” alisema.
Alisema atasimamia uamuzi wa vikao na kuhakikisha
unatekelezwa na kupima matokeo kwa kufanya tathmini juu ya malengo
waliyojiwekea.
Mulenda alisema endapo atashinda na CCM ikawa ndicho chama tawala, atakuwa na kazi ya kuisimamia Serikali.
“Ukiona Serikali inafanya vibaya na chama
kinachotawala kinaona sawasawa, basi siku za kukaa madarakani za chama
hicho zinahesabika,” alisema.
Alisema endapo atafanikiwa katika safari yake hiyo, atahakikisha
Serikali yake kupitia ilani ya uchaguzi ya CCM inakuwa sikivu, makini
na inayojali shida za watu.
“Nawahakikishia wananchi kuwa kwa kutambua shida
zao ni dhahiri nitajua wanataka nini na hawataki nini na kwa msingi huo,
Serikali itakayokuwa chini yangu wakati wote tunahakikisha Watanzania
tunawapeleka kule wanakotarajia kwa kutumia uwezo wetu ambao ulijengwa
na waasisi wa Taifa hili,” alisema.
Alisema wazee waliwaambia kuwa nchi ina raslimali
za kutosha na kinachotakiwa ni kujiongoza ili kutumia amani na utulivu
kujenga nchi.