ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Ijumaa, 22 Julai 2016

Kikwete Akata Mzizi wa Fitina....Awapiga Kijembe Waliodhani CCM Itakufa

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais mstaafu Jakaya Kikwete, amekata mzizi wa fitna kwa kutangaza rasmi kuwa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM, utakaofanyika mjini Dodoma kesho utafanya kazi moja tu ya kumchagua Rais John Magufuli kuwa Mwenyekiti mpya wa chama hicho.

Kikwete alisema hayo alipofungua kikao cha Kamati Kuu ya CCM kwenye ukumbi wa White House, makao makuu ya CCM, mjini hapa jana. Kauli hiyo ya Kikwete inamaliza minong’ono ya muda kuwa hapangekuwa na kupokezana kijiti katika mkutano huo.

Pia kauli hiyo imezima madai kwamba kungekuwa na mchujo katika uchaguzi wa Mwenyekiti, ambapo majina hadi matano yangependekezwa na Kamati Kuu na kupelekwa katika Halmashauri Kuu ambayo ingekata mawili na kupeleka matatu kwenye Mkutano Mkuu Maalumu, ili yapigiwe kura kumchagua Mwenyekiti.

“Ajenda yetu kubwa leo (jana) ni moja tu; nayo ni kupendekeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ili nayo Halmashauri Kuu ya Taifa ipendekeze kwa Mkutano Mkuu wa CCM ili achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa CCM,” alisema Kikwete kwenye ufunguzi huo wa Kamati Kuu, akitumia dakika tano tu, kisha wajumbe wakaendelea na ajenda. Rais Magufuli alichaguliwa kuongoza Tanzania Oktoba mwaka jana.

Katika hotuba yake hiyo ya jana, Kikwete aliwajia juu ‘wafitini’ walioombea chama hicho kife katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Alisema “Wapo watu walidhani CCM ingekufa na walishajiandaa na salamu za rambirambi. Walidhani wataibuka. Hawakuibuka na hawataibuka kamwe.” 
Kikwete aliwaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa kilikuwa kikao chake cha mwisho cha Kamati Kuu, kauli iliyobainisha wazi kuwa anang’atuka kumwachia kijiti Rais Magufuli kuongoza chama.

Alisema amekuwa Mwenyekiti wa Chama kwa miaka 10, hivyo aliwashukuru wajumbe wa Kamati Kuu kwa kumsaidia katika kipindi chote hicho huku akisisitiza; “Bila msaada wenu CCM isingekuwa imara kama ilivyo hivi leo.”
 
Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Rais Magufuli alikuwa akifahamika kama Tingatinga na kwenye mikutano kadhaa, Rais mstaafu Kikwete aliweza kumuita kwa jina hilo.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa CCM, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete jana alikagua ukumbi wa mikutano wa CCM na kuoneshwa sehemu mbalimbali ambapo alisema ameridhika na maandalizi ya mkutano kwamba yanaenda vyema.

Maeneo mengine aliyotembelea ni mabanda ya mama na baba lishe, sehemu za kutolea huduma za Benki na mabanda ya maonesho ya wajasiriamali.

Katika ziara hiyo aliambatana na Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana, makamu Mwenyekiti Bara, Phillip Mangula, waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Nape Nnauye, msemaji wa CCM Christopher Ole sendeka, naibu katibu mkuu wa CCM Bara Rajab Luhwavi na wajumbe wa Kamati Kuu Pindi Chana na Mohamed Seif Khatib. Wajumbe wa mkutano Mkuu maalum wa CCm walianza kuwasili jana na wengine wengi wanatarajiwa leo.
ADVATISMENT   kikoti education centre
KIKOTI EDUCATION CENTRE (K.E.C)
MAHALI: ILULA MADIZINI KARIBU MAJENGO YA KANISA KATORIKI

Mzazi/Mlezi wa ……………………………………………….kikoti education centre inapenda kukutarifu

Magazeti ya Leo ijumaa ya tarehe 22/07/2016



















ADVATISMENT   kikoti education centre
KIKOTI EDUCATION CENTRE (K.E.C)
MAHALI: ILULA MADIZINI KARIBU MAJENGO YA KANISA KATORIKI

Mzazi/Mlezi wa ……………………………………………….kikoti education centre inapenda kukutarifu

Alhamisi, 21 Julai 2016

Lowassa atoa ya moyoni

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEh3EW61OzPNqE0abzqWF5bYKTg2z_AvkeJaBHIeJOlQlxdh1C6VIBc0tmEZz4gQYYPw3qcdBLsXLZM0rnAAFBAsNC-pPSb1Fly5_BuCFWywhnXMMPP4OUAxzdgW5m__7yd7-p_57ax9Bqo/s1600/1.jpgALIYEKUWA mgombea urais kupitia mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa amewataka vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumlinda Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kama nyuki wanavyomlinda malkia wao.

Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alitoa kauli hiyo wakati akifungua kikao cha Kamati ya Utendaji ya Baraza la Vijana (Bavicha) jijini Dar es Salaam jana.

Waziri mkuu huyo wa zamani, pamoja na mambo mengine aliwataka vijana wa chama hicho kuacha vita vya ndani kwa ndani na badala yake washikamane na kuwang’ang’ania viongozi wanaowaongoza.

“Tuache vita vya ndani kwa ndani, Mbowe ndiye mwenyekiti wetu wa chama…tumlinde kama nyuki wanavyomlinda malkia wao. Mtu akishakuwa kiongozi tumg’ang’anie,”alisema Lowassa.

Lowassa ambaye alijiunga na upinzani mwishoni mwa mwaka jana alisema kumekuwapo na kawaida ya kuibuka kwa makundi uchaguzi unapomalizika.

Azungumzia uchumi
Katika mkutano huo, Lowassa pia alizungumzia uchumi ambapo alisema hivi sasa maisha ya Watanzania walio wengi hayana uhakika, huku matumaini kidogo yakielekezwa kwa watu wachache.

“Binadamu anaishi kwa matumaini, lakini mambo yanayoendelea hapa nchini hayatoi matumaini hayo…hali ya uchumi inakwenda vibaya sana, kuna rafiki yangu mmoja ana msamiati wake anasema maisha ni pasua kichwa hivi sasa kwa sababu hayana uhakika,” alisema Lowassa.

Aidha Lowassa alieleza kusikitishwa kwake kwa baadhi ya watu kuacha kuzikana kwa sababu ya siasa ambapo alisema hayo ni mambo ya ovyo.

Ajivunia vijana
Katika hotuba yake hiyo, Lowassa aliwapongeza Bavicha kwa kutii maelekezo ya Mbowe kuhusu kusitisha uamuzi wao wa kwenda Dodoma kuzuia Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Niwapongeze kwa kutii maelekezo ya mwenyekiti wetu, najua haikuwa rahisi, mlikuwa mmeshajipanga lakini maelekezo ya mwenyekiti ni mazuri, vitu vingine si lazima uende mbali sana ni kama kwenye simu kwamba ‘message sent’ mlifikisha ujumbe mahsusi hata kama hawakubaliani lakini ujumbe umefika.

“Wala msione aibu mnachofanya, vijana mngefanya tofauti ningeshangaa, nyie ndio chachu ya mabadiliko lazima mje na kitu kipya na mawazo mapya, ninyi ni jeshi la chama.

“Kwa uzoefu wangu CCM lazima watakwenda kumtambulisha mwenyekiti wao mpya katika Uwanja wa  Jamhuri mjini Dodoma, hivyo wananchi wenyewe wataangalia na kupima kama Chadema wanazuiwa kwa nini wapinzani wazuiwe, waachane wapate tabu kujieleza kwa umma” alisema Lowassa huku akishangiliwa.

Kuhusu uteuzi uliofanywa na Rais John Magufuli hivi karibuni, Lowassa aliuponda na kusema ni wa kibaguzi kwa sababu umewatenga vijana wa vyama vya upinzani.

“Kama wewe ni CCM utakuwa mkuu wa wilaya, mkoa na hata mkurugenzi wa halmashauri lakini hali ni tofauti kwa vijana wa upinzani, wanabaguliwa utadhani si Watanzania.

“Hili ni jambo la kutafakari na kukemea kwa sabu ajira ni tatizo hapa nchini, lakini hata hizo chache zinatoka kwa kubaguana pamoja na jitihada zote lakini hazisaidii,”alisema.

Msako vyuoni wanasa wanafunzi hewa 139

Image result for ndalichako

WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, amesema operesheni ya uhakiki wa wanafunzi hewa wanaopatiwa mikopo imeanza kuonesha mafanikio, kwani wanafunzi hewa wameanza kubainika.
Akizungumza baada ya kufungua Maonesho ya 11 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) jana, alisema uchunguzi wa awali umebaini wanafunzi hewa 139 katika vyuo vitano vilivyofanyiwa uhakiki.
“Tunaendelea kuhakiki na tayari tumehakiki vyuo vitano ambapo wanafunzi hewa 139 walibainika kati yao wamo marehemu, walioacha shule, waliosimamishwa shule na waliohamishwa,” alisema bila kuvitaja vyuo hivyo kwa maelezo kuwa, taarifa haijawa kamili.
Aidha, alisema katika jitihada za kuboresha elimu inayotolewa nchini wizara hiyo inafanya mapitio ya Sheria ya Vyuo Vikuu ili itoe fursa kuchukulia hatua vyuo vya kitapeli. Alisema kupitia sheria hiyo, serikali itaanzisha mfumo wa kuratibu na kudhibiti uanzishwaji wa vyuo kwa lengo la kuwabana wanaoanzisha vyuo kwa lengo la utapeli.
Hivi karibuni, Rais John Magufuli aliwasimamisha kazi watendaji wakuu wa Kamisheni ya Tume vya Vyuo Vikuu (TCU) baada ya kubainika kamisheni hiyo inadahili wanafunzi wasio na sifa, wakiwemo wenye ufaulu wa daraja la nne, kujiunga na vyuo vikuu na kuwapatia mikopo.
Serikali pia ilibaini uwepo wa wanafunzi hewa wanaotafuna mikopo ya elimu ya juu, jambo lililosababisha Profesa Ndalichako kutangaza vita dhidi yao na kuanza operesheni ya uhakiki katika vyuo vyote vikuu nchini.
Aliungwa mkono na Rais John Magufuli aliyetangaza kuwa serikali yake imejipanga kumaliza makosa yote yaliyojitokeza huko nyuma, ikiwemo tatizo la watumishi na wanafunzi hewa lililoibuka hivi karibuni.
Profesa Ndalichako alianza kuchukua hatua kwa kusimamisha kazi viongozi wanne waandamizi kwa tuhuma za kudahili wanafunzi wasio na sifa.
Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya TCU, Awadh Mawenya naye alisimamishwa kazi kwa kosa la kushindwa kuwachukulia hatua watumishi waliodahili wanafunzi hao wasio na sifa.
Profesa Ndalichako alichukua hatua hizo baada ya TCU kudahili wanafunzi 489 waliopata daraja la 4.32 katika mitihani yao ya kidato cha nne lakini walijiunga na chuo kikuu na kupatiwa mikopo yenye thamani ya Sh milioni 784.
ADVATISMENT   kikoti education centre
KIKOTI EDUCATION CENTRE (K.E.C)
MAHALI: ILULA MADIZINI KARIBU MAJENGO YA KANISA KATORIKI

Mzazi/Mlezi wa ……………………………………………….kikoti education centre inapenda kukutarifu

Serikali kupaisha zaidi udahili vyuo vikuu



Imeandikwa na Mwandishi Wetu

SERIKALI imesema katika kutekeleza Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo (FYDP II) kwenye sekta ya elimu, imepanga kuleta mageuzi ya elimu kwa kuhakikisha inaongeza udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka asilimia 3.3 ya sasa hadi kufikia asilimia 6.9 ifikapo mwaka 2020.
Mkakati huo unalenga kuimarisha kiwango cha ubora wa elimu inayotolewa nchini ili kupata wahitimu wenye uwezo wa kuwajibika katika maeneo yao ya kazi na kutengeneza ajira, hivyo kuiwezesha Serikali kufikia lengo la Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
Hatua hiyo, imetokana na ukweli kuwa pamoja na nchi kuwa na idadi kubwa ya watu inayoongezeka mwaka hadi mwaka, bado takwimu zinaonesha udahili wa wanafunzi katika vyuo vya elimu ya juu ni mdogo katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jangwa la Sahara.
Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako wakati akifungua Maonesho ya 11 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia.
Alisema katika mwaka wa masomo 2015/2016 jumla ya wanafunzi 224,080 ndio waliodahiliwa, sawa na asilimia 3.3. Alisema kiwango hicho hakijafikia wastani wa chini uliowekwa na nchi za Jangwa la Sahara wa asilimia sita.
Aliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo sasa ni wakati wa Watanzania kuwekeza kwa nguvu zote katika elimu ili kuongeza fursa na usawa kama sharti la kufikia malengo ya taifa ifikapo mwaka 2025.
Alisema kupitia mpango huo, moja ya mageuzi katika mfumo wa elimu yanayotarajiwa pamoja na kuongeza udahili wa wanafunzi kujiunga na elimu ya juu ni kuhakikisha asilimia 56 ya wahitimu ifikapo mwaka 2020 ni wale waliobobea katika fani za sayansi na uhandisi.
Profesa Ndalichako alisema; “Ni kweli kuwa kwa sasa idadi ya vyuo na wanafunzi wanaodahiliwa imeongezeka kuliko miaka ya nyuma, lakini kitendo cha wanafunzi hao kupokea shahada pekee hakitoshi. Lazima vyuo hivi vihakikishe elimu wanayoitoa inawawezesha wahitimu hawa kufanikiwa katika maisha yao ya baadaye.”
ADVATISMENT   kikoti education centre
KIKOTI EDUCATION CENTRE (K.E.C)
MAHALI: ILULA MADIZINI KARIBU MAJENGO YA KANISA KATORIKI

Mzazi/Mlezi wa ……………………………………………….kikoti education centre inapenda kukutarifu

Kinana atoa Masharti Endapo Rais Magufuli Atamhitaji Aendelee Kuwa Katibu Mkuu wa CCM

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ametoa neno endapo Rais John Magufuli atamhitaji kuendelea na wadhifa huo, huku akibainisha kuwa amekutana na changamoto nyingi katika nafasi hiyo kiasi kwamba wakati mwingine alikata tamaa.


Mwanasiasa huyo maarufu ndani ya CCM na nchini, anatarajiwa kuhitimisha uongozi wake wiki hii wakati Mwenyekiti mpya wa CCM Taifa, Rais John Magufuli atakapokabidhiwa uenyekiti huo na kuunda Sekretarieti yake mpya ambayo haijulikani kama itaongozwa tena na Kanali huyo wa zamani wa Jeshi.

Akizungumza jana na waandishi wa habari baada ya kukagua Ukumbi wa Mkutano Maalumu wa CCM utakaofanyika keshokutwa Jumamosi, Kinana ambaye amekuwa katika nafasi hiyo kwa miaka mitatu na nusu, alisema aliombwa katika nafasi hiyo baada ya kuwa aliamua kustaafu, lakini akakumbana na changamoto mbalimbali.

CCM kuwa mbali na wananchi 
Alisema kuna wakati aliona kama vile chama kiliacha kwenda kwa wananchi na kwamba hakikuwa karibu sana nao.

“Ninyi ni mashahidi, ikabidi kubuni utaratibu mzuri wa kwenda kwa wananchi ili chama kiwe karibu na wananchi, kiwasikilize na kuwa sauti ya wananchi kifuatilie matatizo yao kisimamie utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi,” alisema Kinana na kuongeza kuwa katika kufanya hivyo amekuwa akiwasiliana na Rais na Waziri Mkuu kwa ajili ya matatizo kutatuliwa.

“Changamoto ya pili ya kuimarisha umoja na mshikamano ndani ya chama, hapo nyuma kulikuwa na misukosuko kidogo ya umoja na mshikamano, kushutumiana na kulaumiana,” alisema na kuongeza kuwa kazi nyingine aliyofanya ni kuimarisha umoja ndani ya chama, kushirikiana na viongozi wenzake kuhakikisha chama kinajitahidi kwa kadri ya uwezo wake kurejea katika misingi yake ya awali katika maeneo ya uadilifu, uwajibikaji na utendaji kazi kwa ufanisi.

Azuiwa ziarani
Kinana alisema amekwenda wilaya zote, majimbo, mikoa na nusu ya kata za nchi na amesafiri zaidi ya kilometa 192,000, kufanya mikutano zaidi ya 3,700 ya aina mbalimbali ya ndani na nje na haikuwa kazi rahisi
 “Changamoto nilizokutana nazo ambazo lazima nikiri ni pale nilipotaka wakati mwingine kufanya ziara kwenye maeneo fulani fulani niliambiwa ni hatarishi siwezi kwenda kwa hiyo ilibidi nibishane na viongozi na watendaji wakuu wa serikali…nikasema hapana nimeamua kwenda lazima niende,” alisema Kinana.

Katibu huyo akitoa mfano alisema kuna wakati aliamua kutoka kwa boti kutoka Nyamisati wilayani Rufiji kwenda Mafia, viongozi wa Mkoa wa Pwani walifikiri si njia salama ya kusafiri na kumpelekea ujumbe asisafiri kwa boti, bali asafiri kwa ndege, lakini alisema hapana ataondoka kwa boti.

“Walichofanya wakakaa kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na wakaniandikia barua rasmi kwamba tunakushauri usisafiri kwa boti safiri kwa ndege kwa maana nyingine walikuwa wanajivua lawama kwa yatakayotokea, lakini vile vile kunitisha kidogo kwamba si salama zaidi nikawasisitiza hapana,” alieleza Kinana.

Ashitakiwa kwa JK
“Baadaye Rais mstaafu Kikwete alikuwa Msoga, viongozi wa Mkoa wa Pwani wakaenda kumwambia tumezungumza na Katibu Mkuu wako naona hasikii tumemuandikia barua ya kumuomba asisafiri na boti hasikii, Rais akaandika meseji ndefu sana…nikamjibu rais nakuheshimu mamlaka yako ni makubwa si vizuri nikakukatalia, lakini niruhusu nikukatalie kwa sababu hata wananchi wanaosafiri kwenye boti hii wanahatarisha maisha yao, ni vizuri na mimi nikahatarisha maisha yangu hata kidogo… akaniambia nimekuelewa endelea,” alibainisha.

Alisema zipo changamoto nyingi sana nyingine, kwa mfano Mbambabay kwenda Kyela, mkuu wa mkoa akamuambia boti haifai kusafiri akasema mara haiwezi kusafiri imeharibika.

“Nikazungumza na Mwakyembe akapeleka mafundi wakatengeneza, safari haikuwa rahisi, lakini changamoto zilikuwa nyingi sana, kwingine Lupingu kule ni gari moja tu ndio inayoshuka chini hakuna kupishana magari nikaambiwa nisiende nikasema nina kwenda,” alisema na kuongeza kuwa kulikuwa na ubishi mwingi wakati mwingine alionekana mtu mmoja kidogo ambaye hasikilizi ushauri sana.

Pia nyingine zinazotokana na changamoto za wananchi kutolipwa mazao yao kwa wakati, mbolea kutofika kwa wakati, halmashauri kutopata fedha za maendeleo kwa wakati, watumishi wa umma wanaohamishwa kwenda vijijini hawaendi vijijini kwenda kuwahudumia wananchi, tatizo kubwa la migogoro kati ya wakulima na wafugaji kati ya wananchi na hifadhi za taifa.

“Ndio maana mnaniona siku hizi nimenyamaza kwa sababu yale yote niliyokuwa nikiyaombea yanafanyika, umangimeza haupo watu wachape kazi wawahudumie wananchi, uadilifu unapigwa vita, rushwa inapigwa vita, uwajibikaji na uadilifu unahimizwa, utendaji kazi unatakiwa na hayo yasipofanyika mtu anaondolewa mara moja,” alifafanua Kinana ambaye kuanzia mwaka 2014 hadi mwanzoni mwa mwaka jana alitembea kote nchini akikisafisha chama chake na kuibana serikali.

Kurejea kwake CCM
“Yalitokea mazingira ambayo niliombwa na viongozi wastaafu na viongozi wa chama kuniomba niwe mtendaji mkuu wa chama chetu. Si nafasi ambayo niliipenda, bali niliitwa na nikakalishwa wakanisihi na mimi nikakubali sababu ni wito na kwa kuwa ni watu ninaowaheshimu na wana dhamana kubwa kwenye nchi yetu, nikakubali kufanya kazi hiyo,” alisema Kinana akizungumzia jinsi alivyoteuliwa kushika nafasi hiyo.

Alisema amekuwepo katika uongozi ndani ya chama kwa muda mrefu (miaka 25) ndani ya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa, na alihisi ni wakati muafaka wa kung’atuka.

“Mwanasiasa mzuri ni yule anayejua wakati wa kuingia na wakati wa kutoka. Ni wakati mzuri wa kung’atuka kuachia waingie wenye umri wa kati na umri wa vijana kuachia waongoze chama na kuwaamini,” alieleza.

Alisema moja ya mambo ambayo walikubaliana wakati ule akajitahidi kukiimarisha chama, kusimamia na kumsaidia mwenyekiti kusimamia mchakato wa kuwapata wagombea kwenye nafasi zote za Urais, Ubunge na Udiwani. Pia alijitahidi kuendesha shughuli za kampeni na uchaguzi na utakamalizika.

“Uchaguzi umekwisha niruhusiwe kupumzika, na wote waliafiki na kukubali sasa muda umefika kwa hiyo nimewakumbusha yale tuliyokubaliana muda wake umefika sasa wengine wakaniuliza hivi ndivyo tulivyokubaliana nikawaambia wazee hamjawa wazee kiasi cha kusahau ndio haya tuliyokubaliana,” alieleza.

Akiombwa na JPM
Alipoulizwa kama akiombwa na Rais Magufuli aendelee kwa Katibu Mkuu, Kinana alisema, “Niseme hajasema, hatujazungumza hilo, likitokea tutaangalia, tutakaa naye kikao kama akiniomba, tutakuwa na kikao na mazungumzo muda utakapofika kama nilivyokuwa na mazungumzo na kikao kama kwa wale walioniomba mwaka 2012.”

Waliokisaliti chama
Akizungumzia walioisaliti CCM katika Uchaguzi Mkuu mwaka jana, mtendaji huyo wa CCM alisema msaliti yeyote adhabu yake ni mbaya sana, hata kwenye chama cha siasa.

“Kwenye CCM wapo watu walioyumba, kulikuwa na wimbi kubwa mwaka jana, watu waliyumba hivi kidogo wakakaa mguu upande huku hawapo na kule hawapo, wako ambao sio tu waliyumba, bali walikiuka maadili na hawakushiriki kwenye shughuli za kampeni,” alisema.

Pia alisema wapo ambao hawakushiriki, hawakusaidia na wakasaidia upinzani na kila mtu atakuwa na adhabu yake kulingana na makosa yake.

“Kama mmekuwa mkifuatilia kuna waliochukuliwa hatua ngazi za wilaya na mikoa. Kwa mfano, Shinyanga 123 walichukuliwa hatua. Wapo wanaotakiwa kuchukuliwa hatua kwenye ngazi za juu, sasa jambo moja mtu yeyote kabla ya kuchukuliwa hatua lazima aelezwe mashtaka yake, apewe fursa ya kusikilizwa, kwa hiyo hawa wote watasomewa mashtaka, watasikiliza na kupewa adhabu kwa kadri itakavyostahili, lakini hatua zitachukuliwa mara baada ya Mkutano Mkuu kumalizika,” alieleza.
ADVATISMENT   kikoti education centre
KIKOTI EDUCATION CENTRE (K.E.C)
MAHALI: ILULA MADIZINI KARIBU MAJENGO YA KANISA KATORIKI

Mzazi/Mlezi wa ……………………………………………….kikoti education centre inapenda kukutarifu

Magazeti ya Leo Alhamisi ya tarehe 21/07/2016
















ADVATISMENT   kikoti education centre
KIKOTI EDUCATION CENTRE (K.E.C)
MAHALI: ILULA MADIZINI KARIBU MAJENGO YA KANISA KATORIKI

Mzazi/Mlezi wa ……………………………………………….kikoti education centre inapenda kukutarifu