ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Alhamisi, 24 Desemba 2015

Mawaziri wapya wanne wateuliwa

RAIS John Magufuli amemalizia kujaza nafasi za uteuzi wa Mawaziri na Naibu Waziri alizobakiza wakati akitangaza Baraza la Mawaziri la Kwanza katika awamu ya tano ya utawala wake.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, Gerson Msigwa kwa vyombo vya habari, Dar es Salaam jana, katika uteuzi wake Rais Magufuli amemteua Profesa Jumanne Maghembe kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.
Aidha, Dk Philip Mpango aliyekuwa Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ameteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango. Amemteua kuwa Mbunge na kumteua pia kuwa Waziri.
Rais Magufuli pia amemtangaza Profesa Makame Mbarawa kuwa Waziri mpya wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, akimhamisha kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Naibu Waziri wa zamani wa Ujenzi, Gerson Lwenge ameteuliwa kuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji.
Aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi ni Dk Joyce Ndalichako ambaye mapema jana aliteuliwa kuwa Mbunge. Dk Ndalichako aliwahi kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza na Mitihani la Taifa (NECTA).
Katika uteuzi wake mwingine, Rais Magufuli amemteua Hamad Masauni kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Waziri wake ni Charles Kitwanga. Rais Magufuli, Desemba 9 mwaka huu alitangaza kuunda wizara 18 zenye mawaziri 19. Mawaziri hao na wizara zao kwenye mabano ni George Simbachawene na Angela Kairuki (Ofisi ya Rais-Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora) wakati Naibu wa wizara hiyo na Selemani Jaffo.
Wengine ni Mwigulu Nchemba (Kilimo, Mifugo na Uvuvi) na Naibu wake ni William ole Nasha, Jenista Mhagama (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Balozi Augustine Mahiga (Mambo ya Nje na Afrika Mashariki). Naibu wake ni Dk Suzan Kolimba.
William Lukuvi (Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi) ambaye Naibu wake ni Angelina Mabula, Ummy Mwalimu (Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto) na Naibu wake ni Dk Hamisi Kigwangalla.
Waziri wa Nishati na Madini ni Profesa Sospeter Muhongo ambaye Naibu wake ameteuliwa Dk Medard Kalemani. Waziri wa Katiba na Sheria ni Dk Harison Mwakyembe na Waziri wa Ulinzi ni Dk Hussein Mwinyi.
Aidha, Nape Nnauye aliteuliwa kuwa Waziri wa Habari na Michezo na Naibu wake ni Anastazia Wambura. January Makamba aliteuliwa Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na Naibu wake ni Luhaga Mpina.
Katika uteuzi wa awali, Rais Magufuli alimteua Charles Mwijage kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Wengine walioteuliwa kuwa Naibu Mawaziri, wakati wizara zao zikisubiri mawaziri kamili ni Edwin Ngonyani (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano), Ashantu Kijaji (Wizara ya Fedha), Ramo Makani (Maliasili na Utalii) na Stella Manyanya (Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi).
Naibu Waziri mwingine ni Isack Kamwela wa Maji na Umwagiliaji. Wakati huo huo, Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Alphayo Kidata ameteuliwa kuwa Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA.
“Mbali ya kukamilisha uteuzi wa Baraza lake la Mawaziri, Rais Magufuli pia amewatakia heri Watanzania wote katika Sikukuu za Maulid, Krismasi na Mwaka Mpya na kuwataka washerehekee kwa amani na utulivu,” ilieleza taarifa hiyo ya Ikulu.

Hakuna maoni: