ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumatatu, 26 Septemba 2016

Msajili: Sikumrudishia Lipumba uenyekiti CUF, Kajirudisha Mwenyewe Kinyemela

Wakati  wanasiasa na wasomi wakimnyooshea kidole Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi (pichani) kwa uamuzi wake wa kumtambua aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, mwenyewe ameibuka na kusema kuwa hatua yake hiyo haikulenga kumrudishia msomi huyo nafasi yake ya uenyekiti.

Jaji Mutungi  jana alisema kuwa alichofanya ni kukishauri chama hicho kuhusu mgogoro uliokuwa ukikisonga na Lipumba aliamua kutumia ushauri huo kurudi mwenyewe kwenye nafasi yake hiyo kinyemela.

Kauli hiyo ya Jaji Mutungi imekuja siku mbili tangu alipotoa waraka unaoelezwa kumtambua Profesa Lipumba kama kiongozi halali wa CUF licha ya kuandika barua ya kujiuzulu Agosti 6, mwaka jana akipinga vyama vinavyounda Ukawa kumpa fursa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kugombea urais.

“Isome barua yangu…, mimi nimeamua watu waijadili umenielewa? Ni vizuri wanavyoijadili, ila nilitarajia waijadili kwa tija sio kwa hasira,” alisema Jaji Mutungi.

Alipoulizwa kuhusu polisi kumsaidia Profesa Lipumba kuingia katika makao makuu ya CUF kwa mtutu alisema: “Hizo ni taratibu ambazo (polisi) wanatumia kwa kuzingatia sheria nyingine za nchi.”

Juni mwaka huu, Profesa Lipumba alimwandikia barua Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kutengua barua yake ya kujiuzulu na kutaka arejee kwenye kiti chake, uamuzi uliozusha mtafaruku huku Mkutano Mkuu wa chama hicho ulioketi Agosti 21 ukiridhia kujiuzulu kwake licha ya kuwa ulivunjika.

“Barua yangu inajieleza sina haja ya kuichambua. Nimekujibu baada ya kuona mjadala huo (katika mitandao) nilitegemea (waliomtukana) wawashauri CUF cha kufanya badala ya kuanza kunitukana,” alisema Jaji Mutungi.

“Sasa huko mahakamani wanakotaka kwenda kama mahakama ikiamua kama Mutungi alivyoshauri huko nako watatukana pia?” alihoji.

Wanasiasa na wasomi 
Mwenyekiti wa Chama cha Kijamii (CCK), Constatine Akitanda alisema alichofanya msajili ni kupandikiza zogo ndani ya CUF jambo ambalo linasikitisha.

Akitanda alisema ndani ya CUF kuna bundi ambaye alikuwa anasumbua watu ila msajili ameongezea mgogoro huo na kuwa alichokifanya si sawa kwa mujibu wa mamlaka yake.

“Unajua hii nchi inachezewa sana hivi mtu anajiuzulu mwenyewe halafu anaamua kurejea mwenyewe bila kufuata taratibu ni aibu, lakini nadhani kuna mkono wa mtu,’ alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira alisema anachokiona ndani ya CUF ni uwepo wa biashara haramu ambayo inaweza kuua chama hicho.

Alisema ni wakati mwafaka kwa wafanyabiashara haramu hao wakajulikana katika pande zote kwani ni aibu kuvumilia kasoro hizo zitawale vyama vya siasa.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Dominata Rwechungura alisema migogoro ndani ya vyama vya siasa ipo, hivyo ni jukumu la CUF kutatua ili kurejesha amani na upendo kati yao.

Mwenyekiti wa Chama cha United People Democratic Party (UPDP), Fahimu Dovutwa alisema kinachotokea ni msiba unaoacha pengo ndani ya CUF na vyama vya siasa nchini.

Dovutwa alisema pia pengo la mwasisi wa CUF, marehemu Shaban Mloo linaonekana na kuwataka wazee wa chama hicho kukaa ili kukinusuru chama. 
“Huu ni msiba katika siasa za Tanzania, naomba CUF watafute wazee wao ili waweze kusuluhisha hali hiyo kwa maslahi ya chama chao kwani pengo la Mloo linaonekana,” alisema.

Katibu wa Habari na Uenezi wa NCCR Mageuzi, David Kafulila alisema mgogoro wa CUF unaweza kutolewa uamuzi na mahakama pekee kwa kuwa msajili hana mamlaka ya kufanya alichokifanya. Kafulila alisema msajili anapaswa kushauri kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na si kama alivyoelekeza kwani anaongeza mgogoro zaidi.

Mwenyekiti wa ADC, Hamad Rashid alishauri CUF kutumia vikao kumaliza tofauti zao, huku akibainisha kuwa ndani ya chama hicho kuna viashiria vya udikteta na usultani.

Mbunge wa Tandahimba CUF, Katani Katani alisema kwa sasa wamethibitisha jinsi Lipumba anavyotumika kwani pamoja na Jeshi la Polisi kukataza maandamano, wafuasi wa Lipumba waliandamana bila kuzuiwa.

Alisema haiwezekani chama kikaendeshwa kwa ajenda za watu wachache ambao wanatumikia matumbo yao na makundi yao na si chama.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Kitivo cha Sheria, Dk. Onesmo Kyauke alisema msajili anakosea na kuwataka CUF wakimbilie mahakamani kupata haki.

Credit: Jamboleo

Hakuna maoni: