Imeandikwa na
Waandishi Wetu
- Imechapishwa: 01 Januari 2016
WAKATI makatibu wakuu wateule na manaibu wao wanaapishwa leo Ikulu
jijini Dar es Salaam, baadhi ya wasomi wamesema uteuzi wao ambao
ameufanya Rais John Magufuli unalenga kuisaidia nchi iweze kuingia
kwenye uchumi wa Viwanda.
Profesa Emrod Elisante wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) alisema
kwamba uteuzi huo ni mzuri kwani umezingatia utaalamu zaidi. Alisema
lazima wizara ziwe na wasimamizi madhubuti ambao wataisaidia nchi kuwa
yenye viwanda.
“Nikiwaangalia watu kama Dk Chamriho (Leonard, Katibu mkuu Uchukuzi)
Profesa Mkenda (Adolf, Katibu mkuu katibu Mkuu Biashara na Uwekezaji)
hawa ni watu makini na ni watendaji wazuri naamini wataisaidia nchi,”
alisema.
Alisema iwapo watapewa malengo na rais, wana uwezo wa kuyatekeleza
hasa kuifanya Tanzania iwe sekta ya viwanda kama alivyoahidi Rais
Magufuli wakati wa kampeni.
Profesa Elisante alisema licha ya nchi kuwa na changamoto mbalimbali
kama za kifedha na rasilimaliwatu, lakini alisema uteuzi huo umejaa
wataalamu ambao wengi wamepelekwa kwenye fani zao.
“Unajua hata waliopita ni wazuri, ila tatizo waliingia kwenye siasa,
Rais Magufuli akiweza kuwadhibiti hawa wasiingie kwenye siasa na
wakafanya kazi yao kwa weledi na kujua malengo ya wizara na nchi naamini
tutachomoka,” alisema.
Naye Mwanaharakati za haki za Binadamu, Onesmo Olengurumwa alisifu
uteuzi wa makatibu wakuu hao kwa maelezo kuwa umewapeleka watu katika
fani walizosomea.
“Mfano Profesa Mchome (Sifuni ambaye ni Katibu mkuu wizara ya katiba
na sheria) yule ni mwanasheria aliyebobea naamini ataisaidia nchi kwa
kutumia taaluma yake,” alisema Olengurumwa.
Alisema kitendo cha Rais Magufuli kujaza wataalamu kama maprofesa na
madaktari katika Serikali yake kunaonesha kuwa anathamini wataalam hao
na angependa kuona wanatumia taaluma yao kuisaidia nchi.
“Utakuta katika wizara kwa mfano ya Madini, kuanzia Waziri hadi
makatibu wakuu ni profesa na daktari, wakikaa pamoja wanaweza kufanya
vizuri lakini pia wanaweza kufanya vibaya,” alisema Olengurumwa.
Alisema dhamira ya rais ni nzuri, hata hivyo alikosoa wingi wa
makatibu wakuu hao hasa uteuzi wa manaibu makatibu wakuu kuwa haukuwa na
maana kwani kila kitengo na idara kina mkurugenzi ambaye kama katibu
mkuu hayupo anaweza kufanya kazi zake.
“Alipunguza baraza la mawaziri tukafurahi, lakini amerudi nyuma kwa
kuleta makatibu wakuu wengi tofauti na alivyotangaza kuwa makatibu wakuu
pia wangepungua, kwa hiyo tuko kule kule,” alisema Olengurumwa.
Naye Katibu Mkuu mteule wa Afya katika wizara ya Afya,Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya amesema ameupokea
uteuzi wake kwa mshituko mkubwa kwa kuwa ni jambo ambalo hakuwahi
kulifikilia.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi yake ya Ukurugenzi wa
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, Dk Ulisubisya alisema uteuzi wake
umekuja kwa ghafla huku akiwa na mipango aliyokuwa amejiwekea ya
kuendeleza hospitali hiyo.
Alisema mawazo yake yote ilikuwa ni kujipanga kuhakikisha anatekeleza
majukumu aliyokuwa ameachiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii majuma mawili yaliyopita, Dk Donan Mbando aliyefanya
ziara ya kushtukiza katika hospitali hiyo.
Dk Ulisubisya alisema agizo lingine lilikuwa kuhakikisha hospitali
hiyo inaanzisha Chuo Kikuu kwa ajili ya kuongezea taaluma kwa madaktari
na kuboresha huduma za dharura na kupunguza foleni kwa wagonjwa, mambo
ambayo tayari alianza kuyafanyia kazi na kuyawekea mikakati.
Wakati huo huo, leo Rais Magufuli anawaapisha makatibu wakuu na
manaibu katibu wakuu wa wizara mbalimbali aliowateua juzi. Kazi ya
kuwaapisha inafanywa leo Ikulu na kwa hatua hiyo, Rais atakuwa
amekamilisha kazi ya kupata watendaji wa ngazi za juu katika wizara
mbalimbali, ambazo ni moja ya vyombo vinavyotegemewa kuleta maendeleo ya
watanzania ikiwa kila mmoja kwa nafasi yake, atatimiza wajibu wake.
Imeandikwa na Shadrack Sagati, Dar na Joachim Nyambo, Mbeya.