KAMA Mzazi inapenda kuanza mwaka huu mpya wa 2016 kwa kuwapongeza
wote waliobahatika kwa mapenzi ya aliyetuumba kuwa hai na salama na
kuendelea kuomba Mungu awalinde kwa mwaka huu tangu mwanzo hadi mwisho
wake.
Tunawajibika kushukuru kwa sababu kuna wenzetu hawakubahatika kuuona
mwaka huu kutokana na sababu mbalimbali zilizo nje ya uwezo wetu. Lakini
kubwa kwa Januari hii ya 2016 ni zawadi ya Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa wazazi na walezi kwa kuanzisha
elimumsingi bila malipo kwa vitendo.
Elimumsingi inajumuisha elimu ya awali,ya msingi na sekondari, kuwa
bure kwa gharama za serikali kwa shule za ngazi hiyo zinazomilikiwa na
serikali ispokuwa shule 11 tu nchi nzima. Hongera sana serikali ya Rais
Magufuli kwa kuishi kwa vitendo.
Kwa mujibu wa waraka wa serikali uliotolewa katikati ya Desemba mwaka
jana, uliainisha wazi majukumu ya serikali katika utekelezaji wa
elimumsingi bila malipo lakini pia ulioanisha majukumu ya wazazi katika
utekelezaji wa jambo hili ili watoto waweze kusoma bila kupata
changamoto zisizo za lazima.
Kama Mzazi nataka kuwakumbusha majukumu ya wazazi na walezi katika
utekelezaji wa jambo hili kwani yale ya serikali, yenyewe inayajua
vilivyo na tayari imeshaanza kutekeleza kwa kutenga fedha za kugharimia
elimu hiyo.
Wazazi na walezi kwa mujibu wa waraka wa serikali wanatakiwa kununua
sare za shule na vifaa vya michezo,vifaa vya kujifunzia ikiwa ni pamoja
na daftari na kalamu, vifaa vya usafi binafsi, chakula kwa wanafunzi wa
kutwa na bweni na gharama za matibabu.
Gharama nyingine kwa wazazi na walezi ni kulipia nauli ya kwenda na
kurudi shule kwa wanafunzi wa kutwa na wanafunzi wa bweni kwa wakati wa
likizo, kununua magodoro, shuka na vifaa vya usafi.
Ili kuhakikisha kwamba hayo yanafanyika bila kuleta manung’uniko kwa
kutumbukiza gharama zisizokuwemo katika orodha hiyo, wazazi na walezi
wanatakiwa kukemea na kutoa taarifa kwa vyombo husika juu ya mienendo
inayokwenda kinyume na utaratibu wa elimumsingi bila malipo.
Kwa uhalisia wake kila mzazi na mlezi anatakiwa kuwa macho kwa kuwa
msimamizi wa utekelezaji wa sera hiyo ya serikali ya elimumsingi bila
malipo huku watoto wakibakiwa na jukumu la kusoma kwa bidii na uwezo
waliojaliwa kwa ajili ya kujipatia ufunguo wa maisha yaani elimu.
Visingizio na figisufigisu zisipewe nafasi katika hili ili tuweze
kunufaika vilivyo.
Visingizio vya watoto kutokwenda shule kwa sababu ya wazazi au walezi
kushindwa kumlipia ada mwanafunzi katika ngazi hizo tatu visipewe
nafasi kama ilivyokuwa kabla ya utaratibu huu mpya. Kila mmoja wetu,
hususan ni wazazi na walezi wajiandae kwa gharama zilizoorodheshwa ili
watoto wetu wote waingie madarasani kwa kazi moja ya kujifunza. Hapa
Kazi Tu sasa!
WAZIRI
wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce
Ndalichako ametoa siku saba kwa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA)
limpe sababu za kubadili mfumo wa utunuku viwango vya ufaulu wa awali(
Division) na kwenda wa wastani wa pointi (GPA) unaotumika sasa Kidato
cha Nne na Sita.
Aidha, ametaka litoe maelezo ya kitaalamu juu ya sababu za kuanzisha
mtihani wa pili kwa watahiniwa wa kujitegemea na kwamba zisipomridhisha,
mwaka huu wasifanyishwe mtihani huo.
Mfumo wa GPA ulianza kutumika kwa wanafunzi waliofanya mtihani wa mwaka
2014 ambao matokeo yao yalitoka mwaka jana.Vile vile mitihani miwili kwa
watahiniwa wa kujitegemea, ilianza mwaka 2014 na 2015.
Ndalichako ambaye aliwahi kuwa Katibu Mtendaji wa baraza hilo kwa miaka
tisa, alitoa maagizo hayo jana ambako pamoja na masuala mengine,
alishuhudia namna alivyojaribiwa na kuletewa vishawishi jambo ambalo
alisema, alilishinda kwa kusimamia taaluma.
Maagizo hayo aliyatoa alipotembelea na kuzungumza na viongozi,
wafanyakazi wa NECTA ambako hakuridhishwa na maelezo yaliyotolewa na
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde.
Alisema tangu alipoteuliwa kuwa Waziri, amepokea malalamiko mengi kutoka
kwa wadau wa elimu na wananchi juu ya mfumo wa sasa wa upangaji matokeo
wa GPA ambao umekuwa haueleweki na kwamba hawakushirikishwa katika
mabadiliko hayo.
“ Nataka nijue sababu za kitaalamu za kubadilisha mfumo wa upangaji wa
matokeo kutoka kwenye ule wa Division (madaraja) kwenda kwenye ule wa
GPA na kama huo mfumo una tija kwa elimu yetu,” alisema.
Awali , Dk Msonde alisema mfumo huo ulipitishwa baada ya vikao kati
yake, Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Baraza la Vyuo vya Ufundi (Nacte) na
Wizara.
Alisema baraza lilitakiwa kuendesha mfumo huo ili kwenda na mifumo
mingine ya elimu ya juu katika kurahisisha udahili wa wanafunzi kwenda
sanjari na mfumo wa serikali mtandao na ajira.
Watahiniwa kujitegemea
Kuhusu uanzishwaji wa mtihani wa pili kwa watahiniwa wa kujitegemea,
Ndalichako alisema, “Nataka sababu za watahiniwa wa kujitegemea kupewa
mtihani wa pili ambao unachukuliwa kama alama upimaji endelevu kwa
mwanafunzi.
“ Kama baraza ambalo ndio wataalamu, mnasema mmeamua kutoa mtihani wa
pili kutokana na kupokea malalamiko ya kufeli na mtihani mgumu, basi
hatuwezi kuendelea nao, nataka nipate sababu za kitaalamu na kama sababu
haziridhisha basi mwaka huu wasifanyishwe mtihani wa pili,” alisema.
Alisema kwa kawaida, mtihani wa pili kwa watahiniwa wa kujitegemea
hauwezi kuwa mbadala wa alama endelevu kwa wanafunzi. Alisema unaongeza
mzigo kwa watahiniwa na gharama za kulipa wasimamizi na wasahihishaji wa
mitihani hiyo.
Ashuhudia alivyojaribiwa
Ndalichako aliwataka viongozi wa baraza hilo kutokukurupuka katika kutoa
uamuzi na kufanya mabadiliko yasiyo na tija kwa taifa. Badala yake,
alisisitiza watumie utaalamu wao kushauri na kukataa maagizo yasiyo na
tija kusaidia katika kuboresha elimu.
Katika hatua nyingine, Ndalichako aliwataka watendaji wa Baraza hilo
kufanya kazi yao kwa umakini na uadilifu na kuepuka vishawishi. “ Baraza
la Mitihani ni sehemu ngumu sana, hasa kutokana na kuhudumia watu na
hasa katika suala zima la mitihani.
"Na ni eneo ambalo lina vishwishi vingi, hata mimi nilijaribiwa kuletewa
vishawishi lakini nilisimama misimamo ya taaluma,” alisema.
Ndalichako pamoja na kuwapongeza Baraza kwa kutoa vyeti mbadala, ametaka kuwa makini katika suala hilo kuzuia udanganyifu.
Alisisitiza watoe tathmini ya kina katika matokeo ya wanafunzi ambayo
yatasaidia wizara kufanya uboreshaji. “Nilipokuwa hapa, kuna wakati
nilikuwa nakosa usingizi linapokuja suala la kutangaza matokeo, unakuta
matokeo ya wanafunzi 30 yote ni mbaya, sasa hapa si kuwa wanafunzi wote
walikuwa hawafundishiki ila kuna tatizo la ziada, na hilo ndio
tunatakiwa kushughulikia,” alisema.
Alisema, “ Nilikuwa naumia sana na ubora wa elimu iliyokuwa ikitolewa
kwa baadhi ya shule, sasa nimepewa kazi ya kuhakikisha elimu inakuwa
bora, tunaondoa watu wa kuchora mazombi na ule wakati wa shule kugeuka
vituo vya kulelea watoto badala ya kutoa elimu umefika mwisho.”
KOCHA wa timu wa Yanga, Hans Van Pluijm amesema kuwa ameridhishwa na
kiwango kinachoendelea kuoneshwa na wachezaji wake katika michuano ya
Kombe la Mapinduzi mjini hapa.
Yanga imetinga hatua ya nusu fainali baada ya kumaliza michezo ya
makundi wakiwa na pointi saba na kushika nafasi ya kwanza katika msimamo
wa kundi A huku Mtibwa Sugar ikishika nafasi ya pili ikiwa na pointi
nne.
Akizungumza baada ya kumaliza mchezo baina yake na Mtibwa, Pluijm
alisema kuwa wachezaji wake wanacheza kwa jinsi alivyowaelekeza.
“Naridhika na kiwango chao hasa kwa vile wanafuata maelekezo yangu na
wanacheza vile ninavyotaka wacheze,”alisema.
Hata hivyo, alisema kuwa mashindano hayo ya Kombe la Mapinduzi ni
mazuri kutokana na kuwa na ushindani ambao unazidi kuongeza uimara wa
timu yake. Katika mchezo huo, Yanga ilishinda mabao 2-1 na mabao yake
yalifungwa na Yussuf Abubakar dakika ya 42 na Mwalimi Busungu dakika ya
82, wakati lile la Mtibwa lilifungwa na Shiza Kichuya katika dakika ya
10. I
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli amemtumia
salamu za pongezi mshambuliaji wa Tanzania anayecheza soka la kulipwa TP
Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mbwana Samatta kwa
kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani.
Magufuli alituma salam hizo jana kupitia Wizara ya Habari, Michezo,
Utamaduni na Sanaa. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa kwa vyombo vya habari, Dk
Magufuli alimtumia salamu za pongezi Waziri wa Wizara hiyo, Nape Nnauye
afikishe salamu zake za pongezi kwa Samatta.
“Rais Magufuli amemtaka Waziri Nnauye amfikishie salamu zake za
pongezi kwa mchezaji huyo, ambaye pia anaichezea TP Mazembe,” imesema
taarifa hiyo ikiongeza kuwa tuzo hiyo imejenga heshima kwa Samatta na
Tanzania.
Katika taarifa hiyo, Magufuli amewasihi wachezaji wa soka wote na
wadau wa mchezo huo kuongeza juhudi kuuendeleza mchezo ili upige hatua
zaidi kimaendeleo. Samatta alitwaa tuzo ya mchezaji bora juzi usiku
iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) katika sherehe
zilizofanyika Abuja, Nigeria.
Mchezaji huyo alikuwa akipambana na wachezaji wengine wawili ambao ni
Robert Kidiaba Muteba (wa TP Mazembe na Congo) na Baghdad Bounedjah
(Algeria & Etoile du Sahel).
Samatta alipata pointi 127, mbele ya mchezaji mwenzake wa TP Mazembe,
kipa Kidiaba wa DRC aliyepata pointi 88, wakati mshambuliaji wa Etoile
du Sahel ya Tunisia na timu ya taifa ya Algeria, Bounedjah alipata
pointi 63.
Mchezaji huyo wa Tanzania ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza
wa Afrika Mashariki kushinda tuzo kubwa ya Afrika. Mafanikio hayo
yamekuja baada ya kuiwezesha Mazembe kutwaa taji la tano la Ligi ya
Mabingwa Afrika, huku akiibuka mfungaji bora kwa mabao yake manane.
Mshambuliaji wa Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang ameshinda tuzo ya
Mwanasoka Bora wa Afrika kwa mara ya kwanza na kumshinda Yaya Toure wa
Man City na Ivory Coast aliyekuwa akisaka tuzo hiyo kwa mara ya tano.
Aubameyang wa Borussia Dortmund ya Ujerumani mwenye umri wa miaka 26,
amewaangusha Toure aliyekuwa anashikilia tuzo hiyo na Andre Ayew wa
Ghana. Amekusanya pointi 143, saba zaidi ya Toure wakati Ayew ameshika
nafasi ya tatu kwa kupata pointi 112.
Wakati huo huo, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal
Malinzi ametoa pia pongezi zake kwa mchezaji huyo. Naye, Kocha wa Yanga,
Hans Pluijm amempongeza Samatta kwa tuzo hiyo akisema kuwa, itawatia
moyo wachezaji wengine wa ndani wa Tanzania kubadilika katika mtizamo wa
kucheza soka la kulipwa.
“Tuzo hiyo itawafanya wachezaji wengine wa Tanzania kucheza katika
kiwango cha juu sio tu katika kujipandisha wao wenyewe, bali kuisaidia
timu ya taifa hasa katika mashindano ya kimataifa,” alisema.
SERIKALI imesema ubomoaji na uondoaji wananchi waishio katika Bonde
la Mto Msimbazi utaendelea kwa utaratibu ambao hautaleta mateso na
usumbufu kwa wananchi. Watakaohusika na uhamishwaji huo, sasa ni wale tu
ambao makazi yao yapo ndani ya bonde, kwenye miteremko ya kuingia
bondeni na kwenye kingo za mto.
Imesisitizwa, awamu hii ya ubomoaji, itajikita katika Bonde la Mto
Msimbazi tu na watakaokuwa na nyaraka halali walizopewa na mamlaka za
umma, zilizowamilikisha na kuwaruhusu kujenga katika bonde hilo,
hawatahamishwa bila kupewa sehemu nyingine za kujenga.
Maamuzi hayo yamefikiwa juzi baada ya mawaziri watatu wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI);
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii.
Mawaziri hao walifanya mkutano wa kutathmini uhamishaji wa wakazi wa
mabondeni katika jiji la Dar es Salaam. Waliamua kuwa watumishi wa umma
waliowamilikisha wakazi maeneo hayo, watachukuliwa hatua za kinidhamu na
kisheria.
Taarifa ya maamuzi hayo ilitolewa jana na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Pia, taarifa hiyo ilisema mawaziri hao wameamua katika siku tatu zijazo,
serikali itaanza kuzoa kifusi na kusafisha maeneo ambapo ubomoaji
umefanyika.
Mawaziri hao walibainisha kuwa serikali itaheshimu amri za mahakama
kuhusu mapingamizi yaliyowekwa na baadhi ya wakazi wa mabondeni, lakini
pia itafuatilia kesi hizo ziishe haraka ili taratibu zinazofuata
zifanyike.
“Serikali itawachukulia hatua za kinidhamu watumishi wake
wanaoendesha zoezi hili kinyume na misingi ya sheria zinazotekelezwa, na
kinyume na misingi ya haki na uwazi, ikiwemo wanaoweka alama za X zaidi
ya mita zilizowekwa kisheria,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, serikali imeanzisha dawati la malalamiko
katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupokea malalamiko
au maswali kuhusu zoezi hilo.
Walisema nyumba na majengo yaliyokuwepo miaka mingi kabla ya kutungwa
kwa sheria zinazotekelezwa katika ubomoaji huo hayatabomolewa,
isipokuwa tu pale maisha ya wakazi yapo hatarini.
Vile vile ilisema wanaoishi katika makazi hayo, watapewa miongozo ya
hatua za kuhifadhi mazingira na kujiokoa na maafa, kwani serikali haina
dhamira ya kubomoa hoteli kubwa za siku nyingi zilizo karibu na fukwe
katika maeneo ya Masaki. Wamiliki wa hoteli hizo, watapewa masharti na
miongozo ya kuhifadhi mazingira kwa mujibu wa Sheria.
Pia, serikali inaweka utaratibu wa karibu zaidi miongoni mwa taasisi
zake ili hatua za utekelezaji wa sheria za nchi, zisiwe chanzo cha
taharuki katika jamii. “Serikali haina dhamira ya kuwatesa wananchi wake
kwa kuwalazimisha kuhama katika makazi yao bila sababu za msingi.
Lakini, pia haiwezi kuruhusu wananchi waendelee kukaa katika maeneo
ambayo ikinyesha mvua kubwa maisha yao yapo hatarini,” ilisisitiza
taarifa hiyo. Itakumbukwa kwamba katika mafuriko ya mwaka 2011, wananchi
49 waishio mabondeni walipoteza maisha.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Hali ya Hewa, mwaka huu
zinatarajiwa kunyesha mvua kubwa kuliko zilizowahi kutokea miaka ya hivi
karibuni. Tathmini ya ubomoaji huo iliyotolewa ripoti kwa mawaziri hao,
ilieleza kuwa hadi sasa wananchi katika nyumba 774 wamehama na nyumba
hizo kubomolewa.
Taarifa hiyo ilieleza pia kwamba kabla ya mkazi kuombwa kuhama,
uhakiki kuhusu uhalali wa makazi anayoishi hufanywa. Kutokana na uhakiki
huo, jumla ya wakazi 20 walikuwa na hati halali za makazi na wakazi 119
walikuwa na leseni za makazi za muda mfupi, hivyo hawakuhamishwa.
Nchi ina kingo za mito na mabonde na maeneo mengi hatarishi, ambamo
watu wanaishi kinyume cha sheria, huku wakiharibu mazingira na
kuhatarisha maisha yao, lakini kutokana na uhaba wa makazi, hali ni
mbaya zaidi katika mabonde ya jiji la Dar es Salaam, hasa bonde la Mto
Msimbazi.
Taarifa hiyo ilisema sababu za kufanya usafishaji wa mabonde na mito
katika jiji la Dar es Salaam na mazingira yanayozunguka, unalenga
kunusuru maisha ya wananchi wanaoishi katika mazingira hatarishi.
Eneo la Bonde la Mto Msimbazi, lilitangazwa ni eneo hatarishi kuishi
binadamu tangu mwaka 1949 na baadaye 1979, hivyo usafishaji huo utapanua
uwezo wa mito ya Dar es Salaam kupitisha maji ya mvua kwa kasi kubwa na
kupunguza uwezekano wa kutokea mafuriko na maafa wakati wa mvua nyingi.
Taarifa hiyo ilisema kabla ya nyumba kubomolewa, taasisi
zinashirikiana kuhakiki iwapo nyumba anayokaa mkazi ina nyaraka za
umiliki na vibali vya ujenzi na iwapo nyaraka hizo zina uhalali wowote.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo nyumba ambazo zimethibitika kuwepo katika
maeneo yasiyostahili, ndizo zinawekwa alama X kuashiria kwamba wakazi
wanapaswa kuhama au kubomolewa, baada ya hapo mkazi hupewa muda wa
kubomoa na kuhama mwenyewe.
“Kutokana na utaratibu huu, sehemu kubwa ya nyumba zinazobomolewa ni
zile ambazo watu wamekwishaamua kubomoa wenyewe, baada ya hapo alama
huwekwa kuonesha mpaka wa bonde,” ilisisitiza taarifa hiyo.
Pia, taarifa hiyo ilieleza kwamba imebainika sehemu kubwa ya wakazi
wa mabondeni ni wapangaji huku wamiliki wanakaa sehemu nyingine salama.
Suala la Mchungaji Rwakatare Taarifa ya mawaziri hao pia ilieleza kuhusu
suala la Mchungaji Getrude Rwakatare.
Ilisema mwanasheria wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira (NEMC) amefukuzwa kazi Januari 6 mwaka huu na taarifa zake
zimekwishafikishwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
kutokana na tuhuma za kufanya udanganyifu kwa niaba ya Baraza, kwa lengo
la kumlinda Mchungaji huyo wa kiroho.
Aidha, Ofisi ya Makamu wa Rais imeshafungua upya kesi mahakamani
kuanzia Desemba 29 mwaka jana, kuomba “makubaliano” kati ya mwanasheria
huyo wa NEMC na Mchungaji Rwakatare, yawekwe pembeni kwa sababu
yalipatikana kwa njia ya udanganyifu.
Taarifa hiyo ilisema Mchungaji Rwakatare amejenga nyumba yake mahali
ambapo amezuia mtiririko wa mto kwa kujaza kifusi ili kupata eneo zaidi
katika eneo la miti ya mikoko, kinyume na sheria tatu muhimu.
Ilielezwa kwamba tangu wakati ujenzi unaanza, jitihada za
kumsimamisha zilifanyika na mamlaka za serikali za mitaa, lakini
ikashindikana kutokana na sababu mbalimbali. NEMC ilipoingilia kati na
kutaka kubomoa nyumba hiyo, Baraza lilishtakiwa mahakamani na wakati
kesi inataka kuanza kusikilizwa, mwanasheria mdogo wa Baraza, yeye
mwenyewe bila kuagizwa wala kuwaarifu wakubwa zake, Mei 11 mwaka jana
aliingia makubaliano na mawakili wa Mchungaji Rwakatare kwa niaba ya
Baraza ya kuondoa kesi hiyo mahakamani na kukubali kwa niaba ya Baraza,
kutombughudhi kabisa Mchungaji Rwakatare.
Ilielezwa kuwa makubaliano hayo yalisajiliwa na Mahakama kama hukumu
Mei 13 mwaka jana, kisha Mwanasheria huyo alificha makubaliano hayo kwa
miezi mitano hadi Oktoba mwaka jana, yalipogundulika na mtumishi
mwingine wa Baraza.
Karakana ya Mradi wa Mabasi Yaendayo kwa Haraka (DART) Taarifa hiyo
ilisema mkutano wa mawaziri hao, ulielezwa kwamba Sheria ya Mazingira
Kifungu 57 (2) inatoa nafasi ya kutolewa ruhusa kwa miradi au shughuli
zenye maslahi ya taifa kufanyika katika maeneo ya mabondeni.
Hivyo, waziri mwenye dhamana ya mazingira anaruhusiwa kutoa miongozo
ya namna ya shughuli hizo, zinavyoweza kufanyika bila kuathiri
mazingira. “Mradi wa DART ulipata kibali hicho na una mkataba na Baraza
la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira kuhusu hatua za hifadhi ya
mazingira, zinazopaswa kutekelezwa katika mradi huo,” ilisema sehemu ya
taarifa hiyo.
Mawaziri walitaka kufahamu hayo kutokana na hoja inayozungumzwa
kwamba wananchi wanaondolewa katika maeneo ya kuishi mabondeni, lakini
mradi wa DART umeachwa.
SERIKALI imesema haitosita kuwafungulia mashtaka na kuwapeleka
mahakamani ifikapo Machi 30, mwaka huu, wazazi ama walezi wote
watakaoshindwa kupeleka watoto wao shuleni ili kupata elimu ya msingi na
sekondari.
Aidha, imepiga marufuku kwa jamii kutumia jina la ‘watoto wa
majumbani’, badala yake waitwe wasaidizi hao ‘wasichana wa kazi’ au
‘vijana wa kazi’. Hayo yalisemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Dar es Salaam jana.
Alisema hayo ili kuhamasisha wazazi na walezi juu ya watoto kujiunga
na shule za msingi na sekondari kwa mwaka huu 2016. Kuhusu kuwafungulia
wazazi mashtaka, alisema serikali inaamini kuwa ikiwa inataka kujenga
taifa lililoelimika ni lazima kuwekeza kwenye elimu, hivyo ni wajibu wa
kila anayehusika kuhakikisha anatimiza wajibu wake.
“Elimu ndio njia bora ya kuwajengea watoto wetu msingi imara wa
maisha yao…serikali haitosita kuchukua hatua za kisheria kwa wazazi au
walezi ambao watazembea, kumficha, kumtorosha au kuzuia mtoto kuanza
masomo ya shule za msingi na sekondari,” alisema Ummy.
Alisema serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
itawafungulia mashtaka na kuwapeleka mahakamani wazazi na walezi wote
watakaoshindwa kutimiza wajibu wao wa kuwapeleka watoto shule, kwani
hata Sheria ya Mtoto Namba 2 ya mwaka 2009 Kifungu cha 8, inaelekeza
kuwa ni wajibu wa mzazi kuhakikisha mtoto anapata elimu.
Waziri Ummy alisema Kifungu cha 14 kinatamka kuwa ni kosa la jinai,
kushindwa kutimiza wajibu huo na adhabu yake ni faini isiyozidi Sh
milioni 5 na kifungo kisichozidi miezi 6; au vyote kwa pamoja.
Alisema pia wazazi na walezi, wahakikishe kuwa watoto wanaoendelea na
masomo ya shule ya msingi na sekondari, wanahudhuria masomo yao kwa
ufanisi, kwa kuwa serikali haitarajii kuendelea kuona utoro wa watoto
shuleni kutokana na sababu zinazoweza kuepukika.
Kuhusu kuwepo kwa mwitikio mkubwa wa watoto wanaoanza masomo,
alisisitiza kuwa wazazi, walezi na jamii kuhakikisha kila mtoto mwenye
umri wa kuanza elimu ya msingi yaani darasa la kwanza na elimu ya awali,
kujiunga na shule kwa muda uliopangwa na kuhudhuria masomo ipasavyo.
Kuhusu kuwepo kwa michango mbalimbali katika baadhi ya shule wakati
huu wa maandalizi ya shule, alisema serikali imeshatoa mwongozo stahiki.
Waziri huyo alisisitiza kwamba sio ada peke yake iliyofutwa, bali hata
michango yote na tayari serikali imekwishatoa fedha za kugharimia elimu
bure na zimekwishapelekwa katika shule zote nchini.
Kwa ujumla, walimu wakuu hawatakiwi kutoza mchango wa aina yoyote,
kama vile ya ulinzi, maji, umeme, uzio, fagio, jembe, ndoo na mingineyo,
kwani fedha za kugharimia elimu ya bure zitatumika pia kwenye masuala
hayo yote
Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amefanya uteuzi wa Makatibu wakuu na Manaibu Katibu wakuu wa wizara mbalimbali.
Aidha,
Dkt Magufuli pia amemteua Eliakimu Maswi kuwa Kaimu Naibu Kamishna wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na kutengua uteuzi wa Naibu Kamishina
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Lusekelo Mwaseba.
Miongoni mwa Makatibu walioteuliwa ni pamoja na nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi, ambaye amebaki Balozi Ombeni Sefue.
Baadhi
ya Makatibu waku hao waliochaguliwa ni pamoja na Mhandisi Mussa
Iyombewa ameteuliwa katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa, Ofisi ya Makamu wa Rais anakuwa Mbaraka A. Wakili.
Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano waliochaguliwa ni Mhandisi Joseph.
Nyamuhanga (Katibu Mkuu – Ujenzi), Dokta Leonard Chamuliho (Katibu Mkuu -
Uchukuzi) na Profesa Faustine R. Kamuzora (Katibu Mkuu - Mawasiliano).
Wizara
ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ni Dokta Yamungu Kayandabira,
Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi ni Maimuna Tarishi.
Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wanakuwa ni Dokta
Mpoki Ulisubisya atakayesimamia Afya na Sihaba Nkinga - Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Wizara ya Nishati na Madini ni Profesa Justus W. Ntalikwa, Wizara ya Mambo ya Ndani ni Jaji Meja Jenerali Projest A. Rwegasira.
Wizara
ya Fedha na Mipango anabaki kuwa Dokta Silvacius Likwelile , Wizara ya
Mambo ya Nje, Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa ni Dkt Aziz Mlima.
Huku Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa akiteuliwa Job D.
Masima.