KAMBI rasmi ya upinzani bungeni, imetangaza baraza lake la mawaziri
kivuli ambalo Chama cha ACT Wazalendo, chenye mbunge mmoja, Kabwe Zitto,
ndicho hakikuingizwa kwenye baraza hilo. Kiongozi wa kambi hiyo,
Freeman Mbowe alitangaza jana bungeni baraza hilo.
Chadema chenye wabunge wengi katika kambi hiyo, kina mawaziri vivuli
wengi ikilinganishwa na vyama vingine na wakati huo huo, kina wizara
nyingi ambazo kinaongoza peke yake kwa maana ya kuwa na mawaziri na
naibu mawaziri vivuli.
Mawaziri, naibu mawaziri vivuli wa Chadema ni katika Wizara ya Ofisi
ya Rais, Tamisemi, ambayo Waziri Kivuli ni Mbunge wa Moshi Mjini,
Japhary Michael (Chadema) na Naibu wake ni Mbunge wa Ukerewe, Joseph
Mkundi (Chadema).
Wizara ya Fedha na Mipango inaongozwa na wabunge wa Chadema ambao ni
Halima Mdee wa Kawe na Mbunge wa Momba, David Silinde. Kwa upande wa
Wizara ya Nishati na Madini pia inaongozwa na wabunge wote wa Chadema.
Waziri kivuli ni Mbunge wa Kibamba, John Mnyika na Naibu wake ni Mbunge
wa Tarime Vijijini, John Heche.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
inaongozwa na Mbungewa Siha, Dk Godwin Mollel (Chadema) na naibu wake ni
Mbunge wa Viti Maalumu, Zubeda Sakuru (Chadema).
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inaongozwa na wabunge
wa Chadema; ambao ni Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ambaye ni
waziri kivuli akisaidiana na wa Viti Maalumu, Devotha Minja.
Kwa upande wa wizara ya Utumishi, Utawala Bora inaongozwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Ruth Mollel (Chadema) pekee bila naibu.
Mawaziri Chadema kuhusu wizara ambazo mawaziri vivuli ni wa Chadema
na manaibu ni wa vyama vingine, ni Ofisi ya Waziri Mkuu: Sera, Bunge,
Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu inaongozwa na Mbunge wa Bunda Mjini,
Ester Bulaya (Chadema). Bulaya anasaidiana na manaibu ambao wote ni wa
CUF.
Nao ni Mbunge wa Chake Chake, Yusuf Kaiza Makame na Abdallah Maftah wa Mtwara Mjini .
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na
Kimataifa inaongozwa na Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa na Naibu
wake Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Mngwali (CUF).
Mambo ya Ndani ya Nchi amepangiwa Mbunge wa Arusha, Godbless Lema
(Chadema) akisaidiwa na Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdallah Salim (CUF),
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaongozwa na Mbunge wa
Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare (Chadema) na naibu wake ni Mbunge wa
Viti Maalumu, Salma Mwassa (CUF).
Waziri kivuli mwingine ni Suzane Lyimo wa Viti Maalumu anayeongoza
Wizara ya Elimu, Sayansi Teknolojia na Ufundi akisaidiana na Mbunge wa
Mgogoni, Dk Ali Suleiman Yusuf (CUF) ambaye ni naibu.
Wizara ya Katiba na Sheria inaongozwa na Mbunge Singida Mashariki,
Tundu Lissu (Chadema ) akisaidiana na Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolela
(CUF).
Mawaziri wa CUF, Wizara zinazoongozwa na CUF kwa maana ya waziri
kivuli kutoka chama hicho, ni Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na
Mazingira, ambayo Mbunge wa Malindi, Ali Saleh Ali(CUF) anasaidiana na
Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul (Chadema).
CUF imepata pia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambayo Waziri
kivuli ni Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF) na naibu ni Mbunge wa
Viti Maalumu, Dk Immaculate Semesi (Chadema).
Kwa upande wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi laKujenga Taifa, inaongozwa
na Mbunge wa Ole, Juma Hamad Omary (CUF) na naibu wake ni Mbunge wa
Ukonga, Mwita Waitara (Chadema). Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF)
anaongoza wizara ya Maji na Umwagiliaji akisaidiwa na Mbunge wa
Kilombero, Peter Lijualikali (Chadema).
Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR) amepangiwa wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano akisaidiwa na Naibu ambaye ni Mbunge wa Karatu,
Qambalo Qulwi (Chadema). Kiongozi wa Upinzani bungeni, Mbowe aliomba
wote wanaohusika watoe ushirikiano kwa baraza hilo kadri inavyowezekana.
DURU la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara linaanza leo wakati timu 12
zikiwemo za Yanga na Simba kushuka kwenye viwanja tofauti kusaka pointi
tatu muhimu. Hata hivyo, Azam FC inayoshika nafasi ya pili katika
msimamo wa ligi hiyo, leo ilitakiwa kucheza na Prisons ya Mbeya,
haitashuka dimbani kwa sababu inashiriki mashindano ya timu nne nchini
Zambia.
Yanga wenyewe wako kileleni wakiwa na pointi 39 sawa na Azam FC,
lakini wanaongoza kwa uwiano wa tofauti ya magoli, leo watakuwa wageni
wa Coastal Union katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani
mjini Tanga.
Katika mchezo wa raundi ya awali, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao
2-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Yanga watataka kudhihirisha kuwa hawakubahatisha kuifunga Coastal katika
mchezo wa kwanza, huku Wagosi hao wa Kaya nao watataka kudhihirisha wao
sio wanyonge mbele ya mabingwa hao watetezi.
Vijana hao wa Jangwani wakishinda leo watakuwa wamejikusanyia pointi
42 na kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo na kuiacha Azam FC
ikibaki na pointi zake 39 katika nafasi ya pili.
Kwa upande wa Simba, wenyewe katika mchezo wa kwanza dhidi ya African
Sports uliochezwa Mkwakwani, iliibuka na ushindi kiduchi wa bao 1-0,
hivyo na leo itataka kuendeleza ubabe dhidi ya vijana hao wa Tanga.
Simba yenye pointi 33, inazihitaji sana pointi tatu kutoka kwa
African Sports ili angalau izidi kujisogeza katika nafasi ya tatu nyuma
ya Azam katika mbio hizo za ubingwa wa ligi hiyo.
Kwa sasa Simba inafundishwa na Mganda Jackson Mayanja aliyechukua
nafasi ya Muingereza Dylan Kerr aliyetimuliwa licha ya timu hiyo kuwa
katika nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi hiyo.
Mayanja alisema pamoja na ugumu wa mchezo huo, watajitahidi kuibuka
na ushindi ili kuendelea kuzifukuza Yanga na Azam FC zilizoko kileleni.
Coastal Union na African Sports ziko katika nafasi ya 14 na 15 baada ya
kucheza mechi 15 na kuambulia pointi tisa na 10 badala ya kuwa na pointi
45 kutoka katika mechi hizo 15 za duru la kwanza.
Mechi zingine leo ni JKT Ruvu watakuwa wenyeji wa Majina ya Songea,
huku Mtibwa Sugar wakiikaribisha Stand United, wakati Mwadui FC
itaikaribisha Toto African wakati Kagera Sugar watacheza na Mbeya City
na Mgambo JKT watakuwa wenyeji wa Ndanda FC.
Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa Mgambo kuikaribisha Ndanda FC
kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga. Kwa upande wa ufungaji mabao,
Amis Tambwe ndiye anayeongoza hadi duru la kwanza linapomalizika baada
ya kupachika mabao 13 huku Hamisi Kiiza wa Simba akifuatia kwa mabao 10.
SERIKALI imewahakikishia Watanzania kuwa mchakato wa kuanzishwa kwa
Mahakama Maalumu ya mafisadi na wezi, umefikia hatua nzuri. Waziri wa
Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe alisema hayo juzi bungeni mjini
hapa, wakati akichangia Hotuba ya Rais ya Ufunguzi wa Bunge.
Akizungumzia mchakato wa kuanzishwa kwa mahakama hiyo maalumu,
Mwakyembe alisema unakwenda vizuri na utakapokamilika Watanzania
watafahamishwa. “Kiongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, akitoa tamko
lazima litekelezwe.
Kama tunakumbuka Rais, kwa nyakati tofauti kipindi cha kampeni,
aliahidi kuanzisha Mahakama Maalumu ya Mafisadi na Wezi,” alisema
Mwakyembe. Akiizungumzia hotuba ya Rais, Mwakyembe alisema ikiachwa
hotuba ya Mwalimu Nyerere, ya Magufuli pia ni bora na iligusa mioyo ya
Watanzania wenye nia njema na Taifa.
“Wakati rais anatoa hotuba yake iliyokuwa na aya 160, alipigiwa
makofi na vigelegele mara 137, ni zaidi ya asilimia 86, ya Dk Martin
Luther ambaye ni Mmarekani mweusi,” alisema na kuongeza kuwa hatua hiyo,
imewaweka pabaya wapinzani waliokuwa wanapinga kila kitu.
Dk Mwakyembe alisema tatizo ni kwamba kwa hotuba hiyo, yeyote
akijaribu kuipinga, wananchi watamuona wa hovyo. Aliendelea kusema;
“Wamejaribu (upinzani) kutoka kwenye mjadala, kwa hoja tu ya TBC
(Shirika la Utangazaji Tanzania), ili wasiwepo kwenye mjadala, kwani
wakiwepo lazima wataisifia tu.”
January na Tanzania Mpya
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), January Makamba
alisema safari ya kutengeneza Tanzania Mpya, haitakuwa nyepesi na ni
lazima wajaribiwe, watiwe shaka na kukatishwa tamaa kuhusu mwelekeo wao.
Akijibu hoja za wabunge zilizotolewa wakati wa kujadili hotuba hiyo
ya Rais Magufuli ya ufunguzi wa Bunge, aliyoitoa Novemba mwaka jana,
January alisema;“ni kama kutengeneza keki ya mayai, lazima upasue
mayai”.
Aliendelea kusema, “watu wasipate mashaka wala wasiwasi kwamba nchi
inaelekea katika mwelekeo usiofaa. Tulifika mahala tukahitaji Rais wa
namna hii, tumempata na tumuunge mkono.”
Kauli ya Waziri inalenga kujibu kauli za baadhi ya watu, ikiwemo
wabunge wa vyama vya upinzani, ambao hivi karibuni walikosoa kazi ya
‘kutumbua majipu’ inayofanywa na Rais Magufuli pamoja na waziri, wakidai
kwamba haizingatii taratibu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), Utumishi na Utawala Bora, George Simbachawene alisema kazi
ya Rais Magufuli ya kuisuka Serikali haijakamilika, kwani anaendelea kwa
wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi hadi kwa wakuu wa idara,
watakaochujwa kuhakikisha wanaendana ya kaulimbiu yake ya ‘Hapa Kazi
Tu’.
Alisema Tanzania mpya ya Magufuli inayokuja ni ya watu wanaofanya
kazi. Tunataka tuwahakikishie kwamba Rais anaendelea kuisuka serikali na
mtambue kwamba serikali bado haijakamilika, bado tunahitaji wakuu wa
mikoa, wakuu wa wilaya lakini tunakwenda vizuri zaidi tunataka kusuka
wakurugenzi.
“Tunakwenda mbali kusuka mpaka wakuu wa idara, tunataka tuwachuje
vizuri kabisa na siyo kuokotana okotana. Tunataka Tanzania mpya
tukianzia juu tukisema hapa kazi tu basi ni hapa kazi,” alisema.
Hotuba ya Rais Bungeni Akizungumzia Mapambano Dhidi ya Rushwa na
Ufisadi, alipofungua rasmi Bunge mjini Dodoma, Novemba 20, mwaka jana,
2015, Rais Magufuli alisema, “Jambo moja nililolisemea kwa nguvu kubwa
wakati wa kampeni ni mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.
Sikufanya hivyo kwa sababu nilitaka tu kuwarubuni wananchi ili wanipe
kura zao na kunifanya kuwa Rais wao. Nililiongea jambo hili kwa dhati
kabisa, na nilichokisema na kuwaahidi wananchi ndicho hasa
nilichokikusudia. Wananchi wanachukia sana rushwa na ufisadi, na
wamechoshwa na vitendo hivyo.
Mimi pia ninachukia rushwa na ufisadi. Sifurahishwi kabisa na vitendo
vya rushwa na ufisadi vinavyoendelea hapa nchini. Vitendo vya rushwa na
ufisadi vinawanyima haki wananchi na kuitia hasara serikali kwa
mamilioni ya fedha ambazo zingeweza kutumika kwa ajili ya kujenga miradi
ya maendeleo kwa ajili ya watu wetu.”
Magufuli alisema “Mimi nimewaahidi wananchi, na nataka nirejee ahadi
yangu kwao mbele ya Bunge lako tukufu, kwamba nitapambana na rushwa na
ufisadi bila kigugumizi na bila haya yoyote. Dawa ya jipu ni kulitumbua,
na mimi nimejipa kazi ya kuwa mtumbua jipu. Najua kutumbua jipu kuna
maumivu lakini bahati mbaya halina dawa nyingine.
Hivyo ninaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mniombee na
muniunge mkono wakati natumbua majipu haya.” Alieleza kuwa anafahamu
ugumu wa vita aliyoamua kuipigana na anafahamu ugumu na changamoto zake
kwa sababu wanaojihusisha na rushwa, sio watu wadogo wadogo.
Alisema Vitendo vya rushwa na ufisadi vyenye madhara makubwa kwa nchi
na ustawi wa nchi yetu, hutendwa na watu wenye dhamana kubwa za uongozi
na utumishi, ambazo wamezipata kutokana na ridhaa ya watu.
“Katika kushughulikia tatizo hili, nimeahidi kuunda Mahakama ya
Rushwa na Ufisadi. Ni matumaini yangu vyombo husika katika jambo hili
havitanikwamisha,” alisema Magufuli.
WAZIRI wa Fedha, Dk Philip Mpango ameondoa hoja ya Mpango wa Pili wa
Maendeleo ya Taifa kwa kipindi cha miaka mitano 2016/17 mpaka 2020/21
aliyoiwasilisha bungeni jana.
Hatua hiyo ilitokana na mwongozo uliotolewa kwa nyakati tofauti na
wabunge; Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACT Wazalendo) na wa
Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema).
Wabunge hao walisema Waziri amewasilisha hoja kinyume na kanuni za
kudumu za Bunge, zinazosema katika mkutano wa bunge wa kila Oktoba na
Novemba, Serikali inatakiwa kuwasilisha mpango wa maendeleo wa taifa wa
kila mwaka.
“Kutokana na maelezo uliotoa (Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge) na
kwa kutumia kanuni ya hamsini na nane, tano ya kanuni za kudumu za Bunge
toleo la 2016, naomba ruhusu kuondoa hoja niliyoiwasilisha leo (jana)
asubuhi ya Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa kwa kipindi cha miaka
mitano 2016/17 mpaka 2020/21,” alisema Dk Mpango.
Hoja hiyo iliondolewa baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Chenge kutoa
mwongozo na kisha kuahirisha Bunge hadi kesho kutwa. Awali katika
maelezo yao bungeni na nje ya Bunge, wakati wakizungumza na waandishi wa
habari, Zitto na Lissu walisema uwasilishwaji wa hoja ya Waziri Mpango,
umekiuka Katiba. Hata hivyo akitoa mwongozo, Chenge alisema suala hilo
halikukiuka katiba.
“Nimelitafakari sana jambo hili, na baada ya kutafakari hakuna
ukiukwaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.” Alisema kilicholetwa na
serikali ni mchakato wa kushirikisha wawakilishi wa Tanzania ili watoe
maoni, ushauri na mapendekezo yao kuhusu na mpango unaokusudiwa
kutekelezwa na Serikali katika mwaka wa fedha 2020/16/17.
Alisema kitu ambacho wabunge lazima wakubali, ni kwamba kulingana na
Kanuni ya 94 (1), Bunge linapofanya kazi hiyo huwa haliketi kama Bunge,
bali linaketi kama kamati ya mipango. “Hiyo ni dosari ambayo tumeiona,”
alisema na kukiri kwamba hapa ilikuwa ni mpango wa muda mfupi.
Hata hivyo alisema Ibara ya 63 haisemi ni lini huo mpango uletwe.
Alikiri kuwa mpango mfupi unatokana na wa mwaka mitano, ambao hitimisho
lake ni pale waziri atakaposoma mpango wa serikali kwa mwaka unaofuata
wa fedha na jioni yake, Waziri anaposoma bajeti ya serikali.
Akihimiza kuwa Kanuni ya 94 (1) lazima izingatiwe, Chenge alisema,
“Bunge halikuweza kukutana Oktoba na Novemba kama kanuni hiyo inavyotaka
kwa sababu kulikuwa na shughuli kubwa ya uchaguzi.
Alisema Serikali na Bunge hawakuwa na njia nyingine, jambo ambalo
ilikuwa lazima mchakato ufanyike sasa ili Machi 11, serikali iwasilishe
mbele ya wabunge kama ilivyofanyika mwaka jana katika ukumbi wa Mwalimu
Nyerere Dar es Salaam.
“Waziri mwenye dhamana anawasilisha mipango na ukomo wa bajeti.
Wakishawasilisha, katibu wa bunge ndiye anapeleka kwa spika ili aelekeze
ipelekwe kwenye kamati ya bajeti hadi watakapokuja kutoa taarifa,”
alisema.
Kwa mujibu wa kanuni, siku ya kusoma bajeti ya serikali, waziri
anawasilisha hoja yake ya mpango; utekelezaji wa hali ya mwaka jana na
mwaka unaofuata. Hivyo kunakuwa na hoja mbili ambazo hujadiliwa kwa
pamoja; hoja ya mpango na ya bajeti ya serikali.
“Haya ndiyo yanapaswa yafanyike,” alisema na kusihi wabunge kuelewa
kanuni. Baada ya maelezo hayo, Chenge alimuita Waziri mtoa hoja; Waziri
wa Fedha, aombe idhini ya Bunge ya kuondoa hoja. Kabla ya kutoa hoja
hiyo, wabunge walihojiwa, na wote waliridhia.
RAIS John Magufuli amefanya uteuzi wa makatibu tawala wawili wa mikoa
ya Mwanza na Katavi, ili kujaza nafasi za makatibu tawala wa mikoa
hiyo. Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema Dar es Salaam
jana kuwa Rais amemteua Kamishna wa Polisi, Clodwing Mtweve kuwa Katibu
Tawala wa Mkoa wa Mwanza, ambako anakwenda kujaza nafasi iliyoachwa wazi
na Faisal Issa ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.
Kabla ya uteuzi huo, Kamishna Mtweve alikuwa Kamishna wa Fedha na
Utawala wa Jeshi la Polisi Tanzania. Balozi Sefue alisema Rais Magufuli
pia amemteua Kamishna wa Polisi, Paul Chagonja kuwa Katibu Tawala wa
Mkoa wa Katavi, ambako anakwenda kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Madeni
Kipande, ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.
Kabla ya uteuzi huo, Kamishna Chagonja alikuwa Kamishna wa Mafunzo na
Operesheni wa Jeshi la Polisi Tanzania. Aidha, Balozi Ombeni Sefue
alisema Rais Magufuli ameamua kuwateua Makamishna hao wa Polisi, kama
alivyowateua Majenerali wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania kuwa
Makatibu Wakuu wa Wizara, kwa lengo la kujenga nidhamu katika utumishi
wa umma.
Makamishna Clodwing Mtweve na Paul Chagonja pamoja na Mahadhi Juma
Maalim ambaye ameteuliwa kuwa Balozi mpya wa Kuwait, wataapishwa jijini
Dar es Salaam leo saa nne asubuhi.