MBUNGE
wa jimbo la Kilolo Venance Mwamoto ameahidi kuongozana na wazee
wa mji wa Ilula kwenda Dodoma kuonana na waziri mkuu Kassim
Majaliwa ili kumfikishia ahadi ya maji ya Rais Dr John Magufuli kwa
wananchi wa mji mdogo wa Ilula .
Huku
akiwataka wananchi wa Ilula na Nyalumbu kutomchagua mwaka 2020 iwapo
atashindwa kutekeleza ahadi ya maji katika mji huo wa Ilula ndani ya
miaka yake mitano ya ubunge.
Akizungumza
na wananchi wa kata ya Nyalumbu na Ilula wakati wa mikutano yake
ya hadhara ya kuwashukuru wananchi wake kwa kumchagua kuwa mbunge
wa jimbo hilo la Kilolo jana ,Mwamoto alisema kuwa kero ya maji
katika mji wa Ilula imekuwa ya muda murefu jambo ambalo hatataka
kuona wananchi hao wakiendelea kutabika.
Alisema
kuwa kero hiyo ya maji imeanza kuwasumbua wananchi hao toka nchi
ipate uhuru wake mwaka 1961 hadi leo wapo katika mahangaiko ya maji
na baadhi ya viongozi wameendelea kufanya udanganyifu wa mradi huo
kama ambavyo mwaka 2010 viongozi walivyomdanganya aliyekuwa
makamu wa Rais Dr Alli Mohamed Shein kwa kupelekwa kufungua mradi
wa maji ambao viongozi walimdanganya kwa kujaza maji katika tanki
hilo ili azindue mradi huo.
Hivyo
alisema udanganyifu huo hautapewa nafasi katika uongozi wake wa
miaka mitano lazima kero hiyo imalizike na wananchi hao waweze
kupata maji vinginevyo yupo tayari kuongoza wananchi wake kumzuia
waziri wa maji kupita Ilula kwenda jimboni kwake Njombe iwapo wananchi
hao hawatatimiziwa ahadi yao ya maji safi na salama .
Mbunge
huyo alisema katika kikao kijacho cha bunge kinachoanza mwezi ujao
ataomba wananchi wa Ilula na Nyalumbu kumteulia wazee watatu ama
wanne ili kwenda nao bungeni Dodoma kukutana na waziri mkuu ili
kwa ajili ya kumkumbusha ahadi ya Rais ya maji katika mji huo wa Ilula
.
Pia
aliagiza mamlaka ya maji ya mji mdogo wa Ilula kuchunguza vema mradi
wa maji uliopo kama umejengwa kwa kiwango ama chini ya kiwango maana
amesema mradi mdogo uliopo kwa sasa bado umekuwa na kero kubwa ikiwa
ni pamoja na baadhi ya maeneo kuvujisha maji huku akiwataka wananchi
kwa upande wao kutunza miundombinu ya maji.
Mbunge wa Kilolo Bw Venance Mwamoto (kushoto) akisalimiana na mmoja kati ya wazee wa mji wa Ilula aliyetoka kuchota maji
Katika
hatua nyingine mbunge Mwamoto alimshauri meneja wa maji wa IRUWASA
katika mji wa Ilula Teodolah Mvungi kuangalia uwezekano wa kuboresha
kituo cha maji eneo la Ilula ili kiweze kunufaisha wananchi wengi
na kuwa iwapo wataanza uboreshaji kwa upande wake ataunga mkono .