WAKUU wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa
nchini wameagizwa kujiandaa kuwapokea vizuri wanafunzi waliochaguliwa
kujiunga na kidato cha tano na kuwaandalia chakula wanafunzi wa bweni
kabla shule hazijafunguliwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, George Simbachawene alisema hayo jana mjini hapa
wakati akizungumzia maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha tano
mwaka 2016 kwenye shule mbalimbali walizopangiwa.
Wanafunzi hao wanatakiwa kuripoti shule walizopangiwa Julai 11, mwaka
huu. Alisema ni vizuri kwa watendaji hao kujipanga ili wanafunzi
wanapofika kwenye shule walizopangiwa wakute mazingira mazuri. Alisema
wanafunzi hao wamepangwa katika shule 329 zote za kidato cha tano na
sita nchini, na kati ya hizo 50 ni mpya.
Simbachawene alisema wanafunzi wa awamu ya kwanza waliopangwa
kujiunga na kidato cha tano ni 65,720 kati ya 90,248 na awamu ya pili
inasubiri nafasi zitakazojitokeza kutokana na wanafunzi watakaoacha
kuripoti kwa kupelekwa na wazazi wao kwenye shule za binafsi.
Alisema chimbuko la kuanzisha shule mpya za kidato cha tano 50
imetokana na maombi ya mikoa kwenye maeneo yao ili kuendana na lengo la
serikali la kuongeza shule za kidato cha tano na sita hapa nchini.
Alisema wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa mamlaka za serikali
za mitaa wana wajibu wa kuzihudumia shule hizo kwa karibu, na pia
kuhakikisha miundombinu yote inakamilika ikiwemo mabweni, madarasa,
vyoo, maabara, samani, huduma za maji na umeme.
Wakati huo huo, Waziri Simbachawene amesema kuanzia sasa shule zote
za serikali zifungwe na kufunguliwa siku moja tofauti na sasa kila shule
imejiwekea utaratibu wake.
OFISI ya Rais, Menejimenti ya Utumioshi wa Umma na Utawala Bora
imejaza nafasi zilizokuwa wazi za Makatibu Tawala wa Wilaya (Ma-DAS)
katika wilaya mbalimbali nchini.
Kujazwa kwa nafasi hizo kumetokana na sababu mbalimbali ikiwemo
baadhi ya Ma-DAS kustaafu, kufariki pamoja na kupoteza sifa za kuendelea
kuwa makatibu tawala wa wilaya hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Angellah Kairuki alisema, baadhi ya wilaya zimeachwa wazi ambapo uteuzi
wa Ma-DAS utafanyika baadaye kwa ajili ya kujaza nafasi hizo.
Kairuki alizitaja wilaya hizo na mikoa yake kwenye mabano kuwa ni
Newala (Lindi), Makete (Njombe) pamoja na Kisarawe iliyopo mkoa wa
Pwani.
“Makatibu ambao waliokuwepo wataendelea na kazi kama kawaida lakini
kwa wale wapya walioteuliwa wafike ofisi za Utumishi wakiwa na CV
(wasifu zao pamoja na nakala za vyeti vyao,” alisema Kairuki.
Ma-DAS walioteuliwa na Wilaya na Mikoa yao kwenye mabano ni David
Mwakiposa (Arusha), Amos Siyantemi (Monduli), Adam Mzee (Arumeru), Abas
Kayanda (Karatu), Lamuel Kileo (Ngorongoro) na Toba Nguvila (Longido,
Arusha).
Kwa mkoa wa Dar es Salaam walioteuliwa ni Edward Mpogoro (Ilala),
Omary Mhando (Kigamboni), Mtela Mwampamba (Ubungo), Hashimu Komba
(Temeke) na Gift Msuya (Kinondoni). Dodoma walioteuliwa ni Kasilda Mgeni
(Bahi), Athanasia Kabuyanja (Mpwapwa), Juliana Kilasara (Chamwino),
Audiphace Mushi (Kongwa), Winnie Kijazi (Kondoa), Jasinta Mboneko
(Dodoma) na Ally Chilukile (Chemba).
Geita walioteuliwa ni Thomas Dime (Geita), Paul Cheyo (Bukombe),
Eliasi Makory (Chato), Reuben Mwelezi (Nyang’wale) na Christopher Bahali
(Mbogwe). Iringa ni Allan Mwella (Mufindi), Joseph Chitika (Iringa) na
Yusuph Msawanga (Kilolo).
Katavi ni Epaphras Tenganamba (Mlele), Mahija Nyembo (Mpanda) na
Mwashitete Geogrey (Tanganyika). Kagera ni Gread Ndyamukama (Bukoba),
Joel Mwakabibi (Biharamulo), Josephat Tibaijuka (Ngara), Mwakasyege
Richard (Muleba), Godfrey Kasekenya (Misenyi), Weka Ng’olo (Karagwe) na
Haji Godigodi (Kyerwa).
Kigoma ni Muguha Muguha (Kasulu), Kwame Daftari (Kigoma), Ayubu
Sebabili (Kibondo), Zainab Mbunda (Kakonko), Upendo Marango (Uvinza) na
Peter Masindi (Buhigwe).
Kilimanjaro ni Heri James (Hai), Abubakari Asenga (Rombo), Mabenga
magonera (Same), Yusufu Kasuka (Mwanga), Leornad Maufi (Moshi) na
Nicodemus John (Siha).
Lindi ni Thomas Safari (Lindi), Lameck Lusesa (Liwale), Athanas
Hongoli (Kilwa), Husna Sekiboko (Nachingwea) na Twaha Mpembenwe
(Ruangwa). Manyara ni Ndaki Mhuli (Kiteto), Zuwena Omary (Simanjiro),
Mkumbo Barnabas (Hanang), Cade Mshamu (Babati) na Samuel Gunzar (Mbulu).
Mara ni (Justin Manko (Musoma), Masalu Kasasila (Bunda), John Mahinya
(Tarime), Cosmas Qamara (Serengeti), Mirumbe Daudi (Rorya) na Credo
Lugalila (Butiama). Mbeya ni Anold Mkwawa (Mbeya), Moses mashaka
(Rungwe), Ezekia Kilemile (Mbarali), Sostenes Mayoka (Chunya) na Godfrey
Kawacha (Kyela).
Morogoro ni Alfred Shayo (Morogoro), Michael Maganga (Mvomero),
Stanslaus Nyanga (kilosa), Linno Mwageni (Kilombero), Abraham Mwaikwila
(Ulanga/ Mahenge) na adam bibangamba (Gairo). Mtawara ni Teoford Ndomba
(Mtwara), Benaya Kapinga (Masasi), Azizi Fakili (Tandahimba) na Michael
Matomola (Nanyumbu).
Mwanza ni Kazeri Japhet (Misungwi), Solomon Ngiliule (Magu), Andrea
Ng’hwani (Kwimba), Allan Muhina (Sengerema), Yonas Alfred (Nyamagana),
Focus Majumbi (Ukerewe) na Tryphone Mkorokoti (Ilemela). Njombe ni
Joseph Chota (Njombe), Stephen Ulaya (Ludewa) na Edward Manga
(Wanging’ombe).
Pwani ni Erica Yegella (Bagamoyo), Sozi Ngate (Kibaha), Gilbert
Sandagila (Mafia), Severine Lalika (Mkuranga) na Maria Katemana
(Rufiji).
Rukwa ni Festo Chonya (Nkasi), Christina Nzera (Sumbawanga) na Juma Seph Kalambo.
Ruvuma ni Aden Nchimbi (Namtumbo), Gilbert Sinya (Mbinga), Ghaibu
Lingo (Tunduru), Pendo Daniel (Songea) na Richard Mbambe (Nyasa).
Simiyu ni Albert Tuihwa (Bariadi), Rutaremwa Rutangumirwa (Maswa),
Chele Ndaki (Meatu), Helman Tesha (Itilima) na Sebastian Masanja
(Busega). Shinyanga ni Timonth Ndaya (Kaham), Shadrack Kengese ()
Kishapu) na Boniface Chambi (Shinyanga).
Singida ni Pius Songoma (Iramba), Deusdedith Duncun (Manyoni), Wilson
Shimo (Singida), Flora Yongolo (Ikungi) na Omar Kipanga (Mkalama).
Songwe ni Johari Samizi (Songwe), Mary Marco (Ileje), Tusibetege Tengela (Mbozi) na Mathias Felix (Momba).
Tabora ni (Sweetbert Nkuba (Tabora), Moses Pesha (Uyui), Paschal
Byemelwa (Urambo), Godslove Kawiche (Igunga), Onesmo Kisoka (Nzega),
Renatus Mahimbali (Sikonge) na Jones Likuda (Kaliua).
Tanga ni Veronika Kinyemi (Lushoto), Mariagrace Kallega (Korogwe),
John Mahali (Handeni), Faiza Salim (Tanga), Desderia Haule (Muheza),
Ebene Mabuga (Pangani), Joseph Sura (Mkinga) na Philis Nyimbi (Kilindi).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), George Simbachawene amesema wanaendelea kukusanya takwimu za
madawati mikoa yote nchini ambazo zitabainisha mkoa wa kwanza hadi wa
mwisho katika kufanikisha kampeni hiyo na hatua zitakazochukuliwa kwa
walioshindwa.
Alisema hayo jana mjini hapa wakati akikabidhiwa hundi ya Sh milioni
900 kwa ajili ya utengenezaji wa madawati nchini iliyotolewa na Benki ya
NMB.
Alisema tatizo la uhaba wa madawati lilikuwepo tangu awamu zilizopita
za uongozi wa nchi, hata hivyo tatizo hilo liliongezeka mwaka huu
kutokana na serikali kuanza kutekeleza utoaji wa elimu ya msingi bila
malipo.
Aliongeza kuwa, utekelezaji huo ulihamasisha wazazi na jamii kwa
ujumla kuwaandikisha watoto wengi kuanza darasa la awali na darasa la
kwanza, hivyo idadi kubwa ya uandikishaji imeongeza upungufu wa madawati
uliokuwepo.
Waziri huyo alisema Januari mwaka huu, watoto waliotegemewa kuanza
darasa la kwanza walikuwa milioni moja, lakini walioandikishwa walifikia
milioni 1.3.
“Tunaendelea kukusanya takwimu za madawati na tutajua wa kwanza hadi
wa mwisho na hatua zitakazochukuliwa kwa walioshindwa,” alisema na
kuongeza kuwa pamoja na hayo, sasa wanaelekeza nguvu kwenye kukabiliana
na upungufu wa vyumba vya madarasa, kwani vilivyopo havitoshi.
Alisema katika shule za msingi kuna upungufu wa vyumba vya madarasa
127,799 sawa na asilimia 54 kati ya vyumba 236,092 vinavyohitajika huku
kwa upande wa sekondari kuna upungufu wa vyumba 10,636 (asilimia 23.7).
Aidha, Simbachawene ameishukuru NMB kwa kuitikia mwito wa Serikali ya
Rais, Dk John Magufuli kwa kuchangia Sh milioni 900 za kununulia
madawati. Naye Ofisa Mkuu wa Fedha wa benki hiyo, Waziri Barnabas
alisema sera yao ni kutoa asilimia moja ya mapato yao kwa ajili ya
shughuli za kijamii.
MBUNGE wa Mwibara, Kangi Lugola, anayekabiliwa na mashtaka ya kuomba
rushwa ya Sh milioni 30, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu itoe
onyo kwa kitendo cha upande wa Jamhuri kuahirisha kesi mara kwa mara.
Licha ya Lugola, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mbunge wa
Mvomero, Ahmad Saddiq (53) na wa Lupa, Victor Mwambalaswa (63).
Lugola alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Thomas Simba, baada ya
Wakili wa Serikali, Dennis Lekayo kuahirisha kesi hiyo kwa kuwa
waendesha mashitaka katika kesi hiyo hawapo.
Awali, Wakili Lekayo alidai, kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kuwasomea
washtakiwa maelezo ya awali lakini aliomba ipangiwe tarehe nyingine kwa
kuwa mawakili hawapo.
Lugola aliomba Mahakama ikemee tabia hiyo kwa kuwa ofisi ya waendesha
mashitaka ina watu wengi hivyo ingeweza kutoa wengine kwa ajili ya
kuwasomea maelezo ya awali. Aliendelea kudai kuwa, kitendo cha
kuahirisha kesi hiyo mara kwa mara, kinawanyima haki yao ya msingi ya
kufanya shughuli za kibunge.
“Kwa kuwa imekuwa kawaida washtakiwa wanapokuwa watoro, Mahakama
inawaita ili wathibitishe, kwa nini hawajafika na wakati mwingine
wanachukuliwa hatua hivyo naomba mahakama itoe onyo kwa upande wa
Jamhuri,” alidai Lugola.
Baada ya maelezo hayo Wakili Lekayo aliiomba Mahakama iwawie radhi na
kuahidi watafanya haraka kesi iendelee. Hakimu Simba alisema hoja ya
mshtakiwa ni ya msingi kwani kama mwendesha mashitaka aliondoka,
alitakiwa alete wengine. Aliwataka wasirudie kufanya hivyo.
Kesi imeahirishwa hadi Julai 12 mwaka huu kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.
Wabunge hao wanadaiwa wakiwa wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali
za Mitaa, waliomba na kushawishi kupewa rushwa ya Sh milioni 30 kutoka
kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Gairo, Mbwana Magotta kama
kishawishi cha kutoa mapendekezo ya hati safi kwa halmashau
TAASISI
ya Maridhiano inatarajia kuwasilisha ujumbe kwa Spika wa Bunge Job
Ndugai kuomba kuyakutanisha makundi mawili yanayosigana bungeni ili
kuleta muafaka wenye tija kwa taifa.
Mwenyekiti wa taasisi hiyo Sheikh
Sadick Godigodi jana alisema kumeguka kwa Bunge kunakosababishwa na Kambi ya
Upinzani kuona inaonewa na maamuzi ya Naibu Spika, Dk. Tulia Akson
kunahitaji viongozi wa dini kuingilia kati na kupata suluhu.
"Tunatarajia
katika Bunge lijalo litakaloanza Septemba kuwasilisha ujumbe kwa Spika
ili tupewe nafasi ya kutatua mgogoro huu kwa maana wabunge wote
wanatakiwa kuwepo bungeni kuwakilisha matatizo ya wananchi," alisema
Sheikh Godigodi.
"Haiwezekani kundi moja likawa nje na jingine likaendelea, tunahitaji maridhiano ya pande zote mbili za muhimili huo.”
Kambi ya Upinzani Bungeni ilisusia vikao vya Bunge la Bajeti kwa zaidi ya siku 70 kupinga kile kilichoita kuburuzwa na
Naibu Spika katika uendeshaji wa chombo hicho cha kutunga sheria.
Kambi hiyo, ilianza kutoka nje Mei 30 baada ya Naibu Sika kukataa hoja ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua
Nassari
(Chadema), ya kutaka Bunge likatize shughuli zake na kujadili hoja ya
kufukuzwa kwa wanafunzi zaidi ya 700 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
Ingawa
kitendo hicho cha Naibu Spika kiliwaudhi wabunge wa chama tawala (CCM)
na Upinzani, kambi hiyo haikurudi ndani mpaka Bunge lilipoahirishwa na
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katikati ya wiki iliyopita.
Mshauri
wa mambo ya kisheria na kidiplomasia wa taasisi hiyo ya Maridhiano,
Agustino Matefu alisema mbali na kusuluhisha migogoro chochezi ya kidini
kwa kutoa elimu sahihi kwa umma, pia wamejikita katika kusuluhisha
migogoro sugu kati ya wakulima na wafugaji nchini.
“Tumetoa
mchango mkubwa wa kuleta suluhu ya migogoro ya ardhi baina ya wafugaji
na wakulima mkoani Morogoro katika wilaya za Mvomero, Kilombero na
Kilosa (na) ndio maana watanzania wanaona hali ni kama sasa imekuwa
shwari,” alisema Matefu.
Matefu alisema wamepata mualiko rasmi kwa
uongozi wa Mkoa wa Iringa na wanatarajia kwenda huko baada ya uzinduzi
rasmi wa taasisi hiyo utakaofanyika Julai 13 jijini Dar es Salaam.
Katibu
wa taasisi hiyo, Mchungaji Oswald Mlay alisema kuwa uzinduzi na
utambulisho wa taasisi hiyo utaendana na utoaji tuzo ya amani kwa
viongozi na watu mbalimbali waliojitoa kuhamasisha udumishwaji wa amani
nchini.
Wanaotarajiwa kupewa tuzo ni Mama Maria Nyerere kwa niaba
ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere ambae atatunukiwa tuzo ya Amani
uasisi wa amani ya taifa.