Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold
Corporation ambayo ni mmiliki mkubwa wa kampuni ya Acacia Mining
Limited Prof. John L. Thornton na kukubaliana kuwa kampuni hiyo ipo
tayari kufanya mazungumzo na Serikali ya Tanzania ili kulipa fedha
ambazo Tanzania imezipoteza kutokana na kampuni hiyo kuendesha shughuli
zake hapa nchini.
Prof.
John L. Thornton ambaye amesafiri kwa ndege binafsi kutoka nchini
Canada hadi Tanzania amekutana na Mhe. Rais Magufuli leo Juni 14, 2017
Ikulu Jijini Dar es Salaam na mazungumzo yao yamehudhuriwa na Balozi wa
Canada hapa nchini Mhe. Ian Myles na Waziri wa Sheria na Katiba Mhe.
Prof. Palamagamba Kabudi.
Baada
ya Mazungumzo hayo Prof. John L. Thornton amesema kampuni yake ipo
tayari kufanya mazungumzo na Tanzania yatakayozingatia maslahi ya pande
zote mbili na pia ipo tayari kulipa fedha zote ambazo inapaswa kulipa
kwa Tanzania.
Kwa
upande wake Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali inakaribisha mazungumzo
hayo na itaunda jopo la wataalamu watakaofanya majadiliano na kampuni
ya Barrick Gold Corporation ili kufikia makubaliano ya kulipwa fedha
zinazodaiwa na namna kampuni hiyo itakavyoendesha shughuli zake nchini
maslahi ya pande zote mbili.
Mhe.
Rais Magufuli amesema pamoja na kukubali kulipa fedha zinazodaiwa Prof.
John L. Thornton amekubali kushirikiana na Tanzania kujenga mtambo wa
kuchenjulia dhahabu (smelter) hapa nchini.
Wakati
huo huo, Mhe. Rais Magufuli amevionya vyombo vya habari vinavyowataja
Marais wastaafu Mhe. Benjamin William Mkapa na Mhe. Jakaya Mrisho
Kikwete na kuwahusisha na taarifa za kamati mbili za uchunguzi wa madini
yaliyo katika makontena yenye mchanga wa madini (Makinikia) ambao
ripoti zimekabidhiwa kwake na kamati hizo.
“Nimesoma
ripoti zote mbili hakuna mahali ambapo Mzee Mkapa na Mzee Kikwete
wametajwa, vyombo vya habari viache kuwachafua hawa wazee, wamefanya
kazi kubwa ya kulitumikia Taifa letu, viwaache wapumzike” amesema Mhe.
Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
14 Juni, 2017
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni