Asilimia 71 ya wananchi wanaukubali utendaji wa Rais Magufuli tangu
alipoingia madarakani. Kiwango hiki kimeshuka kutoka asilimia 96 mwezi
Juni 2016. Viwango vya kukubalika kwa Rais vinatofautiana katika
makundi mbalimbali:
- Asilimia 68 wenye umri chini ya miaka 30 wanamkubali Rais ikilinganishwa na asilimia 82 wenye umri zaidi ya miaka 50
- Asilimia 75 ya wananchi wenye elimu ya msingi au chini yake wanamkubali Rais ikilinganishwa na asilimia 63 ya wale wenye elimu ya sekondari au zaidi
- Asilimia 75 ya wananchi masikini wanamkubali Rais ikilinganishwa na asilimia 66 ya wananchi matajiri
Viwango vya kukubalika kwa viongozi wengine navyo pia vimeshuka katika kipindi hicho hicho.
- Wabunge: Kukubalika kwa utendaji wa wabunge kumeshuka kutoka asilimia 79 (Juni 2016) hadi asilimia 58 (Aprili 2017).
- Madiwani: Kukubalika kwa utendaji wa madiwani kumeshuka kutoka asilimia 74 (Juni 2016) hadi asilimia 59 (Aprili 2017).
- Wenyeviti wa vijiji/mitaa: Kukubalika kwa utendaji wa wenyeviti wa vijiji/mitaa kumeshuka kutoka asilimia 78 (Juni 2016) hadi asilimia 66 (Aprili 2017).
Matokeo haya yametolewa na Twaweza katika utafiti wake uitwao Matarajio
na matokeo; Vipaumbele, utendaji na siasa nchini Tanzania.
Utafiti huo
unatokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani
Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mikononi.
Matokeo
hayo yanatokana na takwimu zilizokusanywa mwezi Aprili mwaka 2017 kutoka
kwa wahojiwa 1,805 kutoka maeneo mbalimbali Tanzania Bara (Zanzibar
haihusiki kwenye matokeo haya).
Kukubalika kwa vyama vya siasa kunatoa taswira mchanganyiko. Kukubalika
kwa CCM kumeendelea kuimarika, ikiwa ni kati ya asilimia 54 na asilimia
65 kati ya mwaka 2012 na 2017, Baada ya kushuka mwaka 2013 na 2014
ambapo kiwango cha kukubalika kilifikia asilimia 54 kutoka asilimia 65
ya 2012.
Kukubalika kwa CCM kumeendelea kubaki katika kiwango hicho
hicho cha asilimia 62 tangu uchaguzi wa mwaka 2015 na asilimia 63 mwaka
2017. Kukubalika kwa Chadema kumeshuka hadi asilimia 17 mwaka 2017
kutoka asilimia 32 mwaka 2013.
CCM inakubalika zaidi miongoni mwa wazee (asilimia 80), ukilinganisha
na asilimia 55 ya vijana. Wanawake (asilimia 68) wanaikubali CCM kuliko
wanaume (asilimia 58), maeneo ya vijijini (asilimia 66) kuliko maeneo ya
mijini (asilimia 57), na wananchi masikini (asilimia 69) kuliko
matajiri (asilimia 53). Wananchi wenye elimu ya sekondari, elimu ya
ufundi au elimu ya juu wanaikubali CCM kwa asilimia 46.
Kukubalika kwa Chadema kwa ujumla unafuata mtiririko tofauti: ni mkubwa
miongoni mwa vijana, wanaume, watu matajiri na wenye kiwango kikubwa
cha elimu.
Ndani ya kipindi cha miaka miwili tu, vipaumbele vya wananchi
vimebadilika sana. Mwaka 2015, asilimia 34 ya wananchi walitaja
umasikini na uchumi duni kama moja ya vipaumbele vyao vikubwa
ikilinganishwa na asilimia 60 waliotaja masuala hayo mwaka 2017.
Mwaka
2015, ni asilimia 9 waliotaja upungufu wa chakula au njaa kama
kipaumbele chao ikilinganishwa na asilimia 57 mwaka 2017.
Katika kipindi hicho hicho, wasiwasi wa wananchi juu ya huduma za umma na rushwa umepungua.
Asilimia ya wananchi wanaotaja masuala yafuatayo kuwa miongoni mwa changamoto kuu tatu zinazoikabili nchi:
- Afya: asilimia 40 mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 59 mwaka 2015.
- Elimu: asilimia 22 mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 44 mwaka 2015.
- Miundombinu: asilimia 21 mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 32 mwaka 2015.
- Huduma ya maji: asilimia 19 mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 46 mwaka 2015.
- Rushwa: asilimia 10 mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 28 mwaka 2015.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni