Baraza la Mitihani Tanzania limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne 2015 ambapo ufaulu umeshuka kwa 1.85% toka 69.75% mwaka 2014 hadi 67.91% mwaka 2015.
SERIKALI ya India imeiomba radhi serikali ya Tanzania, kufuatia
kudhalilishwa na kupigwa kwa wanafunzi wa Tanzania wanaosoma nchini
humo.
Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika, Kikanda na Uhusiano wa
Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga, aliliambia Bunge, jana, mjini hapa,
wakati akitoa taarifa ya serikali kuhusu hatua zilizochukuliwa serikali
ya India kufuatia tukio hilo.
Alisema tayari serikali ya India, imewachukulia hatua wote waliohusika na tukio hilo na wamefikishwa mahakamani.
Balozi Mahiga alisema serikali ya India, imeagiza kuwa wanafunzi wa
Watanzania wapewe ulinzi maalumu kwenye maeneo wanakoishi na
wasindikizwe wanapokwenda masomoni.
Aidha alisema serikali ya India ilimtaka balozi wa Tanzania afuatane
na maofisa waandamizi, wa Wizara ya Mambo ya Nje ya India kwenda
Bangalore ili kukutana na wanafunzi wa Tanzania na wengine wa Afrika
kufanya mikutano na wanafunzi hao.
Balozi Mahiga alisema tukio hilo lilitokea baada ya uendeshaji mbaya
wa gari uliofanywa na mwanafunzi kutoka Sudan ambaye aligonga pikipiki
tatu na baada ya hapo kumgonga mama wa kihindi aliyekufa papo hapo.
Alisema baada ya tukio hilo, mwanafunzi huyo alikimbia na wananchi
waliokuwa jirani walichoma gari lake moto na kwamba baada ya muda
lilitokea gari lingine likiwa na wanafunzi wanne Watanzania akiwemo
msichana mmoja.
Balozi Mahiga alisema wananchi hao walilisimamisha gari hilo na
kuwatoa nje wanafunzi hao ambapo mwanafunzi wa kike alivuliwa nguo na
kutembezwa mitaani uchi, huku wanaume wakipigwa sehemu mbalimbali za
miili yao na gari lao lilichomwa moto.
“Katika gari hilo kulikuwa na simu zao na document (nyaraka) mbalimbali ambazo ziliteketea,” alisema.
Alisema baada ya muda, polisi walifika lakini walishindwa kutoa
ushirikiano ingawa waliwachukuwa na kuwapeleka hospitali. Balozi Mahiga
alisema, “Kule hospitali walionekana wana majeraha makubwa, walitibiwa
lakini ikabidi waondoke kwa sababu walikuwa hawana fedha za kutosha za
kugharamia matibabu”.
Alisema baada ya hapo, Balozi wa Tanzania aliyeko India aliandika
dokezo la kidiplomasia kwa serikali ya India kulaani kitendo hicho na
kuitaka serikali ya India, ichukue hatua za kisheria na za haraka katika
kupeleleza tukio hilo.
KAMBI rasmi ya upinzani bungeni, imetangaza baraza lake la mawaziri
kivuli ambalo Chama cha ACT Wazalendo, chenye mbunge mmoja, Kabwe Zitto,
ndicho hakikuingizwa kwenye baraza hilo. Kiongozi wa kambi hiyo,
Freeman Mbowe alitangaza jana bungeni baraza hilo.
Chadema chenye wabunge wengi katika kambi hiyo, kina mawaziri vivuli
wengi ikilinganishwa na vyama vingine na wakati huo huo, kina wizara
nyingi ambazo kinaongoza peke yake kwa maana ya kuwa na mawaziri na
naibu mawaziri vivuli.
Mawaziri, naibu mawaziri vivuli wa Chadema ni katika Wizara ya Ofisi
ya Rais, Tamisemi, ambayo Waziri Kivuli ni Mbunge wa Moshi Mjini,
Japhary Michael (Chadema) na Naibu wake ni Mbunge wa Ukerewe, Joseph
Mkundi (Chadema).
Wizara ya Fedha na Mipango inaongozwa na wabunge wa Chadema ambao ni
Halima Mdee wa Kawe na Mbunge wa Momba, David Silinde. Kwa upande wa
Wizara ya Nishati na Madini pia inaongozwa na wabunge wote wa Chadema.
Waziri kivuli ni Mbunge wa Kibamba, John Mnyika na Naibu wake ni Mbunge
wa Tarime Vijijini, John Heche.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
inaongozwa na Mbungewa Siha, Dk Godwin Mollel (Chadema) na naibu wake ni
Mbunge wa Viti Maalumu, Zubeda Sakuru (Chadema).
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inaongozwa na wabunge
wa Chadema; ambao ni Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ambaye ni
waziri kivuli akisaidiana na wa Viti Maalumu, Devotha Minja.
Kwa upande wa wizara ya Utumishi, Utawala Bora inaongozwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Ruth Mollel (Chadema) pekee bila naibu.
Mawaziri Chadema kuhusu wizara ambazo mawaziri vivuli ni wa Chadema
na manaibu ni wa vyama vingine, ni Ofisi ya Waziri Mkuu: Sera, Bunge,
Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu inaongozwa na Mbunge wa Bunda Mjini,
Ester Bulaya (Chadema). Bulaya anasaidiana na manaibu ambao wote ni wa
CUF.
Nao ni Mbunge wa Chake Chake, Yusuf Kaiza Makame na Abdallah Maftah wa Mtwara Mjini .
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na
Kimataifa inaongozwa na Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa na Naibu
wake Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Mngwali (CUF).
Mambo ya Ndani ya Nchi amepangiwa Mbunge wa Arusha, Godbless Lema
(Chadema) akisaidiwa na Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdallah Salim (CUF),
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaongozwa na Mbunge wa
Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare (Chadema) na naibu wake ni Mbunge wa
Viti Maalumu, Salma Mwassa (CUF).
Waziri kivuli mwingine ni Suzane Lyimo wa Viti Maalumu anayeongoza
Wizara ya Elimu, Sayansi Teknolojia na Ufundi akisaidiana na Mbunge wa
Mgogoni, Dk Ali Suleiman Yusuf (CUF) ambaye ni naibu.
Wizara ya Katiba na Sheria inaongozwa na Mbunge Singida Mashariki,
Tundu Lissu (Chadema ) akisaidiana na Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolela
(CUF).
Mawaziri wa CUF, Wizara zinazoongozwa na CUF kwa maana ya waziri
kivuli kutoka chama hicho, ni Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na
Mazingira, ambayo Mbunge wa Malindi, Ali Saleh Ali(CUF) anasaidiana na
Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul (Chadema).
CUF imepata pia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambayo Waziri
kivuli ni Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF) na naibu ni Mbunge wa
Viti Maalumu, Dk Immaculate Semesi (Chadema).
Kwa upande wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi laKujenga Taifa, inaongozwa
na Mbunge wa Ole, Juma Hamad Omary (CUF) na naibu wake ni Mbunge wa
Ukonga, Mwita Waitara (Chadema). Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF)
anaongoza wizara ya Maji na Umwagiliaji akisaidiwa na Mbunge wa
Kilombero, Peter Lijualikali (Chadema).
Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR) amepangiwa wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano akisaidiwa na Naibu ambaye ni Mbunge wa Karatu,
Qambalo Qulwi (Chadema). Kiongozi wa Upinzani bungeni, Mbowe aliomba
wote wanaohusika watoe ushirikiano kwa baraza hilo kadri inavyowezekana.
DURU la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara linaanza leo wakati timu 12
zikiwemo za Yanga na Simba kushuka kwenye viwanja tofauti kusaka pointi
tatu muhimu. Hata hivyo, Azam FC inayoshika nafasi ya pili katika
msimamo wa ligi hiyo, leo ilitakiwa kucheza na Prisons ya Mbeya,
haitashuka dimbani kwa sababu inashiriki mashindano ya timu nne nchini
Zambia.
Yanga wenyewe wako kileleni wakiwa na pointi 39 sawa na Azam FC,
lakini wanaongoza kwa uwiano wa tofauti ya magoli, leo watakuwa wageni
wa Coastal Union katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani
mjini Tanga.
Katika mchezo wa raundi ya awali, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao
2-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Yanga watataka kudhihirisha kuwa hawakubahatisha kuifunga Coastal katika
mchezo wa kwanza, huku Wagosi hao wa Kaya nao watataka kudhihirisha wao
sio wanyonge mbele ya mabingwa hao watetezi.
Vijana hao wa Jangwani wakishinda leo watakuwa wamejikusanyia pointi
42 na kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo na kuiacha Azam FC
ikibaki na pointi zake 39 katika nafasi ya pili.
Kwa upande wa Simba, wenyewe katika mchezo wa kwanza dhidi ya African
Sports uliochezwa Mkwakwani, iliibuka na ushindi kiduchi wa bao 1-0,
hivyo na leo itataka kuendeleza ubabe dhidi ya vijana hao wa Tanga.
Simba yenye pointi 33, inazihitaji sana pointi tatu kutoka kwa
African Sports ili angalau izidi kujisogeza katika nafasi ya tatu nyuma
ya Azam katika mbio hizo za ubingwa wa ligi hiyo.
Kwa sasa Simba inafundishwa na Mganda Jackson Mayanja aliyechukua
nafasi ya Muingereza Dylan Kerr aliyetimuliwa licha ya timu hiyo kuwa
katika nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi hiyo.
Mayanja alisema pamoja na ugumu wa mchezo huo, watajitahidi kuibuka
na ushindi ili kuendelea kuzifukuza Yanga na Azam FC zilizoko kileleni.
Coastal Union na African Sports ziko katika nafasi ya 14 na 15 baada ya
kucheza mechi 15 na kuambulia pointi tisa na 10 badala ya kuwa na pointi
45 kutoka katika mechi hizo 15 za duru la kwanza.
Mechi zingine leo ni JKT Ruvu watakuwa wenyeji wa Majina ya Songea,
huku Mtibwa Sugar wakiikaribisha Stand United, wakati Mwadui FC
itaikaribisha Toto African wakati Kagera Sugar watacheza na Mbeya City
na Mgambo JKT watakuwa wenyeji wa Ndanda FC.
Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa Mgambo kuikaribisha Ndanda FC
kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga. Kwa upande wa ufungaji mabao,
Amis Tambwe ndiye anayeongoza hadi duru la kwanza linapomalizika baada
ya kupachika mabao 13 huku Hamisi Kiiza wa Simba akifuatia kwa mabao 10.
SERIKALI imewahakikishia Watanzania kuwa mchakato wa kuanzishwa kwa
Mahakama Maalumu ya mafisadi na wezi, umefikia hatua nzuri. Waziri wa
Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe alisema hayo juzi bungeni mjini
hapa, wakati akichangia Hotuba ya Rais ya Ufunguzi wa Bunge.
Akizungumzia mchakato wa kuanzishwa kwa mahakama hiyo maalumu,
Mwakyembe alisema unakwenda vizuri na utakapokamilika Watanzania
watafahamishwa. “Kiongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, akitoa tamko
lazima litekelezwe.
Kama tunakumbuka Rais, kwa nyakati tofauti kipindi cha kampeni,
aliahidi kuanzisha Mahakama Maalumu ya Mafisadi na Wezi,” alisema
Mwakyembe. Akiizungumzia hotuba ya Rais, Mwakyembe alisema ikiachwa
hotuba ya Mwalimu Nyerere, ya Magufuli pia ni bora na iligusa mioyo ya
Watanzania wenye nia njema na Taifa.
“Wakati rais anatoa hotuba yake iliyokuwa na aya 160, alipigiwa
makofi na vigelegele mara 137, ni zaidi ya asilimia 86, ya Dk Martin
Luther ambaye ni Mmarekani mweusi,” alisema na kuongeza kuwa hatua hiyo,
imewaweka pabaya wapinzani waliokuwa wanapinga kila kitu.
Dk Mwakyembe alisema tatizo ni kwamba kwa hotuba hiyo, yeyote
akijaribu kuipinga, wananchi watamuona wa hovyo. Aliendelea kusema;
“Wamejaribu (upinzani) kutoka kwenye mjadala, kwa hoja tu ya TBC
(Shirika la Utangazaji Tanzania), ili wasiwepo kwenye mjadala, kwani
wakiwepo lazima wataisifia tu.”
January na Tanzania Mpya
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), January Makamba
alisema safari ya kutengeneza Tanzania Mpya, haitakuwa nyepesi na ni
lazima wajaribiwe, watiwe shaka na kukatishwa tamaa kuhusu mwelekeo wao.
Akijibu hoja za wabunge zilizotolewa wakati wa kujadili hotuba hiyo
ya Rais Magufuli ya ufunguzi wa Bunge, aliyoitoa Novemba mwaka jana,
January alisema;“ni kama kutengeneza keki ya mayai, lazima upasue
mayai”.
Aliendelea kusema, “watu wasipate mashaka wala wasiwasi kwamba nchi
inaelekea katika mwelekeo usiofaa. Tulifika mahala tukahitaji Rais wa
namna hii, tumempata na tumuunge mkono.”
Kauli ya Waziri inalenga kujibu kauli za baadhi ya watu, ikiwemo
wabunge wa vyama vya upinzani, ambao hivi karibuni walikosoa kazi ya
‘kutumbua majipu’ inayofanywa na Rais Magufuli pamoja na waziri, wakidai
kwamba haizingatii taratibu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), Utumishi na Utawala Bora, George Simbachawene alisema kazi
ya Rais Magufuli ya kuisuka Serikali haijakamilika, kwani anaendelea kwa
wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi hadi kwa wakuu wa idara,
watakaochujwa kuhakikisha wanaendana ya kaulimbiu yake ya ‘Hapa Kazi
Tu’.
Alisema Tanzania mpya ya Magufuli inayokuja ni ya watu wanaofanya
kazi. Tunataka tuwahakikishie kwamba Rais anaendelea kuisuka serikali na
mtambue kwamba serikali bado haijakamilika, bado tunahitaji wakuu wa
mikoa, wakuu wa wilaya lakini tunakwenda vizuri zaidi tunataka kusuka
wakurugenzi.
“Tunakwenda mbali kusuka mpaka wakuu wa idara, tunataka tuwachuje
vizuri kabisa na siyo kuokotana okotana. Tunataka Tanzania mpya
tukianzia juu tukisema hapa kazi tu basi ni hapa kazi,” alisema.
Hotuba ya Rais Bungeni Akizungumzia Mapambano Dhidi ya Rushwa na
Ufisadi, alipofungua rasmi Bunge mjini Dodoma, Novemba 20, mwaka jana,
2015, Rais Magufuli alisema, “Jambo moja nililolisemea kwa nguvu kubwa
wakati wa kampeni ni mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.
Sikufanya hivyo kwa sababu nilitaka tu kuwarubuni wananchi ili wanipe
kura zao na kunifanya kuwa Rais wao. Nililiongea jambo hili kwa dhati
kabisa, na nilichokisema na kuwaahidi wananchi ndicho hasa
nilichokikusudia. Wananchi wanachukia sana rushwa na ufisadi, na
wamechoshwa na vitendo hivyo.
Mimi pia ninachukia rushwa na ufisadi. Sifurahishwi kabisa na vitendo
vya rushwa na ufisadi vinavyoendelea hapa nchini. Vitendo vya rushwa na
ufisadi vinawanyima haki wananchi na kuitia hasara serikali kwa
mamilioni ya fedha ambazo zingeweza kutumika kwa ajili ya kujenga miradi
ya maendeleo kwa ajili ya watu wetu.”
Magufuli alisema “Mimi nimewaahidi wananchi, na nataka nirejee ahadi
yangu kwao mbele ya Bunge lako tukufu, kwamba nitapambana na rushwa na
ufisadi bila kigugumizi na bila haya yoyote. Dawa ya jipu ni kulitumbua,
na mimi nimejipa kazi ya kuwa mtumbua jipu. Najua kutumbua jipu kuna
maumivu lakini bahati mbaya halina dawa nyingine.
Hivyo ninaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mniombee na
muniunge mkono wakati natumbua majipu haya.” Alieleza kuwa anafahamu
ugumu wa vita aliyoamua kuipigana na anafahamu ugumu na changamoto zake
kwa sababu wanaojihusisha na rushwa, sio watu wadogo wadogo.
Alisema Vitendo vya rushwa na ufisadi vyenye madhara makubwa kwa nchi
na ustawi wa nchi yetu, hutendwa na watu wenye dhamana kubwa za uongozi
na utumishi, ambazo wamezipata kutokana na ridhaa ya watu.
“Katika kushughulikia tatizo hili, nimeahidi kuunda Mahakama ya
Rushwa na Ufisadi. Ni matumaini yangu vyombo husika katika jambo hili
havitanikwamisha,” alisema Magufuli.