ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Alhamisi, 26 Mei 2016

Vigogo wa TCU watumbuliwa

Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma
RAIS John Magufuli amewasimamisha kazi watendaji wakuu wa Kamisheni ya Tume vya Vyuo Vikuu (TCU). Amechukua hatua hiyo baada ya kubainika inadahili wanafunzi wasio na sifa, wakiwemo wenye ufaulu wa daraja la nne, kujiunga na vyuo vikuu na kuwapatia mikopo.
Pia serikali kupitia kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako imetangaza kufanyika kwa udahili upya vyuo vikuu vyote nchini kuondoa wanafunzi wote wasio na sifa. Aidha, imebainika kuwapo wanafunzi hewa wanaotafuna mikopo ya elimu ya juu, jambo ambalo Dk Ndalichako pia ametangaza vita dhidi yao.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Profesa Ndalichako alisema kwa idhini aliyopewa na rais, amewasimamisha kazi mara moja watendaji hao akiwemo Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Yunus Mgaya kwa kushindwa kusimamia kazi za tume akiwa mtendaji mkuu wa taasisi.
Wengine ni Mkurugenzi wa Udhibiti na Ubora, Dk Savius Maronga kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kusimamia ubora na ithibati ya vyuo vikuu. Mkurugenzi wa Udahili, Rose Kiishweko amesimamishwa kwa kushindwa kusimamia udahili wa wanafunzi na kusababisha kudahiliwa wanafunzi wasio na sifa. Mtendaji mwingine aliyesimamishwa ni Kaimu Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka, Kimboka Istambuli.
Walioziba nafasi Waziri Ndalichako alisema ili shughuli za TCU ziendelee, Profesa Eliuter Mwageni ameteuliwa kukaimu nafasi ya katibu mtendaji. Kabla ya uteuzi huo, Profesa Mwageni alikuwa Naibu Makamu Mkuu (Utawala na Fedha) wa Chuo Kikuu cha Ardhi. Aidha Dk Kokubelwa Mollel atakaimu nafasi ya ukurugenzi wa udahili na nyaraka na kabla ya uteuzi wa kukaimu nafasi hiyo, Dk Mollel alikuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Udahili waliofeli St Joseph Alisema kwa muda mrefu, kumekuwa na taarifa za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha St Joseph wanaodahiliwa kutokuwa na sifa. Waziri alisema baada ya ukaguzi kufanyika katika chuo hicho katika Kampasi za Arusha na Songea, kulionekana upungufu mkubwa katika utoaji elimu.
Wanafunzi 489 walibainika kutokuwa na sifa za kusoma chuo kikuu, kwani walikuwa ni wa kidato cha nne waliofaulu daraja la nne huku wengine wakiwa na pointi 32, lakini wakadahiliwa kusomea shahada ya kwanza .
“Mwanafunzi wa kidato cha nne anasoma digrii ya sayansi, mtu kasoma mkondo wa biashara lakini kadahiliwa asomee sayansi na analipiwa mkopo na TCU, si tu hana sifa ya kusoma chuo kikuu, hata cheti cha ualimu hana sifa, hafai hata cheti cha ualimu kupelekwa kwenye digrii,” alisema.
Profesa Ndalichako alisema rais amekuwa akihangaika kutafuta fedha kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu. “Lakini cha kusikitisha, kuna wanafunzi waliofaulu vizuri kidato cha sita wanakosa mikopo, ila wale waliofeli wanaipata mikopo hiyo,” alisema. “Divisheni four (daraja la nne) pointi 34 yuko chuo kikuu, hata ualimu simkubali mtu wa namna hiyo,” alisema.
Alisema baada ya serikali kufunga chuo hicho, wanafunzi hao walihamishiwa vyuo vingine, lakini hata huko walikopelekwa uwezo wao umeonekana kuwa ni mdogo, hali iliyolazimu kuwarudisha madarasa ya nyuma. “Wanafunzi waliotoka St Joseph na kupelekwa Chuo Kikuu cha Dodoma, uwezo wao umeonekana kuwa ni mdogo, ambapo wanafunzi wa mwaka wa pili na wa kwanza wamerudishwa nyuma muhula mmoja huku wale wa mwaka wa tatu wamerudishwa nyuma mwaka moja,” alisema.
Alisema wanachuo wa St Joseph Kampasi ya Songea waliopelekwa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Morogoro, waliokuwa wakisoma mwaka wa nne, wamerudishwa mwaka wa tatu. Aidha, wametengewa muda wa ziada kurekebisha upungufu huo. Alisema pia waliopelekwa vyuo vikuu vingine vya Ruaha na Mkwawa mkoani Iringa, wameonekana kuwa na upungufu pia.
“Kibaya zaidi, hao wanafunzi walikuwa wanapata mikopo, Division four anapata mkopo haki iko wapi? Tulipoona jambo hili si sawa tulichukua hatua tukaieleza bodi ya TCU kusimamisha kazi waliohusika lakini hilo halikufanyika,” alisema.
Alisema kilichoonekana, Mwenyekiti wa TCU, Awadh Mawenya na tume yake, walikataa kuwasimamisha kazi waliohusika. Alisema mwenyekiti wa bodi muda wake uliisha, lakini rais alimuongezea muda mwingine.
“Nimeongea na Rais kaondoa muda alioongezewa mwenyekiti nao unasitishwa,” alisema. Wanafunzi kurejesha fedha Alisema wanafunzi hao 489 ambao walikuwa wanalipiwa na bodi ya mikopo, tayari wameondolewa chuoni na kutakiwa kurejesha fedha walizokopa. “Huo ni mkopo lazima urejeshwe na tumeshatangaza vita kali kwa wanafunzi hewa wanaopata mikopo kutoka elimu ya juu na kazi hiyo imeanza,” alisisitiza.
Wakati huo huo, akijibu maswali bungeni jana, Waziri Ndalichako alisema serikali imejipanga kufanya uhakiki wa viwango vya wanafunzi kujiunga na vyuo vikuu nchini. Alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Mmasi (CCM) aliyetaka kufahamu mkakati wa serikali kupata wanafunzi wenye uwezo, maarifa na tija. Mbunge Mmasi alisema licha ya kuwepo kwa TCU, bado nchi imekuwa ikizalisha wanafunzi wasio na uwezo.
Profesa Ndalichako alisema serikali inajipanga kufanya uhakiki wa vigezo vya kujiunga na vyuo vikuu. Alisema ufafanuzi juu ya hatua hiyo, utatolewa katika hotuba yake ya bajeti itakayosomwa leo.

Magazeti ya Leo Alhamisi ya tarehe 26/05/2016























Jumatano, 25 Mei 2016

Serikali kurejea viwango vya chakula shuleni

Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko, Dodoma
SERIKALI imesema inaendelea kufanya rejeo ya viwango vya chakula shuleni ili kuwezesha wanafunzi wa kidato cha tano na sita kupata elimu bora pamoja na lishe bora.
Aidha imesema serikali imeanza kuwekea miundombinu shule kongwe za kitaifa za kidato cha tano na sita.
Waziri wa Nchi katika ofisi ya Rais,Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jaffo alisema hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma (CUF) aliyetaka kujua mpango wa serikali katika kuhakikisha wanatatua matatizo ya shule za sekondari za kidato cha tano na sita, ikiwemo kupata chakula kisicho na matatizo.
Akijibu swali hilo, Jaffo alisema kwa kutambua changamoto hizo hasa ya chakula serikali inafanya marejeo ya posho kwa kila shule ili kuboresha kiwango cha elimu, ikiwa ni pamoja na shule kongwe kuwekewa miundombinu ya kuwapatia lishe bora.

MAGAZETINI:#Bilioni 15/- kukabiliana na ukosefu wa ajira

Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko, Dodoma
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama amesema serikali imetenga Sh bilioni 15 kwa ajili ya kuongeza ujuzi na kukabiliana na ukosefu wa ajira nchini.
Mhagama alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Josephine Chagula (CCM) aliyetaka kujua mpango wa serikali kuwawezesha vijana wa mkoa wa Geita kuwapatia ujuzi ili waweze kujiajiri na kuajiriwa.
Akijibu swali hilo, Mhagama alisema katika bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu kwenye bajeti yake ya mwaka huu, wametenga fedha hizo ili kuweza kuajiriwa katika viwanda vilivyopo na vitakavyoanzishwa.
Aidha, katika swali hilo la nyongeza, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema kila mkoa una Shirika la viwanda vidogo (Sido) ambalo linatakiwa kutoa elimu ya ujasiriamali bila malipo.
Hivyo alitaka kupeleka vijana ili wapate elimu bure itakayowawezesha kupata ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa.
Katika swali lake la msingi, Chagula alitaka kujua mpango wa Serikali kujenga viwanda vya kusindika mazao katika mkoa wa Geita, kutokana na vijana wengi kukosa ajira na hasa ikizingatiwa sehemu kubwa ya uchumi wa mkoa huo unategemea kilimo.
Akijibu swali hilo, Mwijage alisema kwa kutambua umuhimu wa viwanda katika kuchangia ukuaji wa uchumi nchini, wizara hiyo kupitia makakati unganishi wa Maendeleo ya viwanda kwa lengo la kuhamasisha wananchi na wadau kuwekeza katika kuanzisha viwanda.
Alisema katika mkakati huo unazitaka Mamlaka za serikali za Mitaa na Miji kutenga maeneo ya uwekezaji katika viwanda hadi ngazi ya kata ambayo yatatumika kuanzisha mitaa ya viwanda kwa kutumia malighafi zinazopatikana katika maeneo husika.

MAGAZETINI:# Bunge lawapasha madiwani Misungwi

Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko, Dodoma
BUNGE limekanusha taarifa inayosambazwa katika mitandao ya kijamii na watu wanaodaiwa kuwa ni madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.
Taarifa hiyo inadai kuwa video iliyomuonesha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga akijibu swali bungeni Mei 20 mwaka huu, ilihaririwa na kusambazwa na maafisa wa Bunge.
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Bunge kilitoa taarifa ya ufafanuzi kuhusu madai ya kuhaririwa kwa video hiyo, mjini hapa jana.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa taarifa hizo, si za kweli na zina lengo la kuupotosha umma, kwani ukweli ni kwamba kipindi cha maswali na majibu bungeni, hurushwa moja kwa moja na hupatikana kupitia vituo vyote vya televisheni, vinavyopokea matangazo ya bunge.
Ilisema matangazo hayo, yanaweza pia kurekodiwa na mtu yeyote mwenye uwezo huo popote alipo, kadri anavyoweza kuyapokea matangazo.

MAGAZETINI:#Yanga na TP Mazembe

Imeandikwa na Mwandishi Wetu
KITENDAWILI cha makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC) kiliteguliwa jana, ambapo wawakilishi wa Tanzania katika michuano hiyo Yanga wamepangwa kundi moja na mabingwa wa zamani wa Afrika, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Upangaji wa ratiba hiyo ulifanyika jana mjini Cairo, Misri, ambapo TP Mazembe ni timu yenye umaarufu Tanzania, ambapo nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, ambaye kwa sasa anachezea KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta alitokea timu hiyo kabla ya kwenda Ulaya mwaka huu.
Pia Mazembe ni timu anayochezea Mtanzania mwingine, Thomas Ulimwengu anayechezea pia Taifa Stars na tangu mwaka 2011 ilipokuja nchini kucheza na Simba katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ilitokea kuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki.
Katika droo ya CAF jana mchana, Yanga imepangwa Kundi A na Mazembe, Mo Bejaia ya Algeria na Modeama ya Ghana na ratiba inaonesha mechi za makundi zitaanza Juni 17 mwaka huu. Kwa upande wa Kundi B zipo timu za Kawkab Athletic, Fath Union Sports zote za Morocco, Etoile du Sahel ya Tunisia na Ahly Tripoli ya Libya.
Katika michuano ya Ligi ya Mabingwa, Zesco ya Zambia imepangwa kundi moja na Al Ahly ya Misri, Asec Mimosas ya Ivory Coast na Wac ya Morocco. Kundi B lina timu za Enyimba ya Nigeria, Zamalek ya Misri, Es Setif ya Algeria na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Yanga iliingia makundi ya michuano hiyo baada ya kuitoa Sagrada Esperanca ya Angola kwa jumla ya mabao 2-1, ambapo iliangukia katika kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Shirikisho, baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa 2-1 Alexandria.
Ilianza vizuri Ligi ya Mabingwa kwa kuzitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0, ikishinda 1-0 ugenini na 2-0 nyumbani kabla ya kuitoa na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Kigali na kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
Wakati huo huo, awali jana Kamati ya Maandalizi ya michuano ya klabu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) imeiondoa AS Vita ya DRC kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kosa la kumtumia mchezaji Idrissa Traore hatua za awali akiwa anatumikia adhabu.
Kamati hiyo imefikia uamuzi huo katika kikao chake mjini Cairo, baada ya kupitia malalamiko ya klabu ya Stade Malien ya Mali dhidi ya As Vita juu ya Idrissa Traore.

Magazeti ya Leo tarehe 25/05/2016