ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Alhamisi, 16 Februari 2017

ILULA KUNUFAIKA NA KILIMO CHA NYANYA VIWANDA VYAJENGWA

 
KILIO cha wakulima wa nyanya mkoani Iringa hasa katika mji mdogo wa ilula na kidabaga wilayani kilolo  waliokuwa wakikabiliwa na ukosefu wa masoko ya zao hili sasa kinaonekana kupata ufumbuzi kufuatia ujenzi wa viwanda vya kusindika bidhaa za mbogamboga na nyanya  kukamilika. 
Viwanda hivi vipya ambavyo vipo chini ya makampuni mawili tofauti, moja  kampuni ni  Darsh Industries Limited inayozalisha bidhaa maarufu nchini za Redgold kilichojengwa katika Kijiji cha Ugwachanya, Kata ya Mseke, takribani kilometa 12 kutoka Iringa mjini na kingine kimeweza kujengwa katika mji mdogo wa Ilula kata ya ilula kilometer mbili na nusu kutoka ilula mtua na kinatarajia kuanza uzalishaji hivi karibuni.
Kwa mujibu wa mmoja wa maofisa wa
Darsh Industries Limited anayeshughulikia masuala ya ujenzi huo, Pratap, kiwanda hicho kimeanza uzalishaji wake mwezi  Julai mwaka jana.
Pratap alisema kwamba, uzalishaji umeanza kwa  kiwanda hicho kuhitaji jumla ya tani 200 (kilogramu 200,000) za nyanya kwa siku, sawa na kreti 4,500 au magari 20 aina ya Fuso yenye uwezo wa kubeba  tani 10 kila moja.
“Tunahitaji tani 200 kwa siku, ndio uwezo wa kiwanda, na tunawahakikishia wakulima kwamba soko la uhakika litapatikana wala wasiwe na hofu,” alisema Pratap.
Ofisa huyo alisema kwamba, kiwanda kinanunua nyanya za madaraja yote bila kubagua, hivyo hakutakuwa na ‘masalo’ yatakayomwagwa na wakulima wawe na imani kwamba watapata tija kutokana na kilimo hicho.
Aliongeza kusema kwamba, huwa wanapeleka makreti ya kubebea nyanya kwenye vituo vyote vya kukusanyia zao hilo ambavyo vimeteuliwa na kwamba wakulima hawatagharamia usafiri wa kupeleka kiwandani moja ya kituo hicho ni kile kinachopatikana katika soko la TASAF ilula.
“Wakulima kazi yao inakuwa kupeleka nyanya kwenye vituo ambavyo tunakuwa tumepeleka makreti ya kubebea, usafiri utakuwa ni juu ya kiwanda,” alifafanua.
Aidha, alisema kwamba, pamoja na kununua nyanya kwa wakulima, ambayo ni malighafi ya kiwanda hicho, lakini uongozi utatoa huduma za ugani kwa wakulima ukishirikiana na Mradi wa Tanzania Agricultural Productivity (TAPP) pamoja na maofisa ugani wa vijiji na kata husika linakolimwa zao hilo.
Pratap amewataka wakulima kuongeza uzalishaji wa nyanya ili kukidhi mahitaji ya kiwanda pamoja na kujiongezea kipato.
Nyanya, ambalo ndilo zao kuu la biashara mkoani Iringa hasa katika mji mdogo wa ilula na maeneo ya kidabaga, ukiacha mbao zinazotokana na kilimo cha muda mrefu, limekuwa na changamoto kubwa ya masoko, hali inayowafanya wakulima wengi kukata tamaa.
Kikoti.com blog iliwahi kutembelea Tarafa ya Mazombe, hususan Kijiji cha Image ambako kilimo cha nyanya kimeshamiri na kujionea malundo makubwa ya zao hilo yakiwa yametupwa pembeni kutokana na kutofaa kusafirishwa na kwenda kuuzwa.
“Hii ni hasara kubwa, nimekuja na matenga hamsini, lakini inaonekana yametoka thelathini tu, haya malundo yote ni nyanya zilizolainika (masalo) ambazo haziwezi kwenda mahali popote,” alisema musa mlawa, mkulima wa nyanya kutoka Kijiji cha Iyayi, Kata ya Image wilayani Kilolo.
Wakati huo Musa alikuwa ameacha malundo ya nyanya zisizofaa kusafirishwa, ingawa zinafaa kwa matumizi ya nyumbani au hata kwa kusindikwa, hali ambayo alisema inamtia umaskini kwani kungekuwepo na kiwanda walau angepata chochote na kurudisha gharama zake za kilimo.
Mkulima huyo alisema, gharama za shamba lake lenye ukubwa wa ekari moja zilikuwa Sh. 1 milioni na kwamba alipovuna alipata jumla ya matenga 80, lakini matenga 30 yalionekana yameharibika tangu shambani huku mengine 20 yakiharibika wakati alipozifikisha nyanya hizo kwenye soko dogo kando ya Mto Mlowa unaotenganisha kijiji cha Iyayi na Uhominyi katika Kata ya Image.
Bei ya soko ambayo aliikuta kwa siku hiyo ilikuwa Sh. 5,000 tu kwa tenga moja, hivyo kujikuta akiambulia Sh. 150,000 kwa matenga yake 30 ambayo yalionekana yanafaa kusafirishwa.
Musa  ni miongoni mwa wakulima wengi wa Mkoa wa Iringa wanaojishughulisha na zao la nyanya ambao wamekuwa wakipata hasara kila mwaka kutokana na ukosefu wa soko la uhakika.
Inaelezwa kwamba, zaidi ya asilimia 70 ya zao hilo la nyanya inaharibika kutokana na ukosefu wa soko na miundombinu bora, hasa barabara.
Wakulima ndio wanaoathirika zaidi licha ya kutumia gharama kubwa katika kilimo.
Hali hiyo imewafanya wakulima wengi kuendelea kuogelea katika lindi la umaskini, huku wengine wakipunguza ukubwa wa mashamba yao ama kutolima kabisa kutokana na kukosa uwezo wa kuyahudumia. 

Tulipopata nafasi ya kuzungumza na mfanyabiashara wa nyanya, aliiambia blogu hii kwamba nyanya inayoharibika ni kiasi kikubwa zaidi kuliko inayofika sokoni.
“Nyanya ikifika hapa sokoni kutoka shambani kiasi kikubwa inakuwa masalo, hivyo inabidi ichaguliwe na iliyo bora ndiyo inayosafirishwa.
“Kabla ya kufika hapa sokoni mkulima anakuwa ameichambua na kuyaacha masalo shambani, lakini ikishachambuliwa tena hapa, hata kama ana matenga 10, anaweza kujikuta amebaki na manne tu ambayo ndiyo yananunuliwa na sisi wafanyabiashara,” alisema mfanyabiashara huyo.
Pia alisema,  wanapoifikisha nyanya hiyo kwenye masoko makubwa, hasa Dar es Salaam, wanalazimika kuichambua, hivyo kiasi kinachobakia kwa ajili ya matumizi kinakuwa kidogo zaidi ya kilichozalishwa.

Hakuna maoni: