Hali
ya ulinzi imeimarishwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)
alikolazwa mfanyabiashara Yusuf Manji baada ya kuugua ghafla akiwa
polisi alikokuwa akihojiwa.
Manji
aliyekuwa akihojiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini hapa
alipelekwa hospitalini hapo juzi jioni akiwa ndani ya gari la wagonjwa
aina ya Toyota Land Cruiser lenye nembo ya Shirika la Umoja wa Mataifa
la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) huku gari lake aina ya Range Rover
likifuata kwa nyuma.
Askari
wenye sare na wengine wakiwa na mavazi ya kiraia nje ya wodi aliyolazwa
mwenyekiti huyo wa klabu maarufu nchini ya Yanga walionekana
wakiimarisha ulinzi.
Ilipofika saa 4:13 asubuhi mfanyabiashara huyo alitoka kwenye chumba hicho na kuongozwa kuelekea upande mwingine wa jengo hilo.
Akiwa amevalia nguo za wagonjwa zenye rangi ya kijani, Manji alitembea taratibu kuelekea upande aliokuwa akielekezwa.
Alipoulizwa
kuhusu uwapo wa Manji hospitalini hapo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI,
Profesa Mohamed Janabi alisema hawezi kuzungumzia taarifa za mgonjwa.
Februari
8, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alitoa orodha ya watu
65, akiwamo Manji ambao aliwataka wafike Polisi kwa ajili ya mahojiano
kuhusu masuala ya dawa za kulevya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni