Mbunge
wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani maarufu Profesa Majimarefu,
ametoa ruhusa kwa wakazi wa jimbo lake kumwadhibu kwa kumpiga mawe iwapo
atashindwa kutekeleza ahadi alizoahidi wakati wa kampeni za Uchaguzi
Mkuu wa 2015.
Majimarefu
aliyasema hayo wakati akizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mikutano
ya hadhara na wananchi wa Vijiji vya Kwemshai, Ngulu na Mlungui, katika
ziara yake jimboni mwake.
Alisema
licha ya kuwa nje ya nchi kwa matibabu, lakini baada ya afya yake
kuimarika amerejea nchini akiwa tayari kutatua kero za umma.
Aidha, amewaomba wapigakura wake kuendelea kushirikiana naye huku wakimpatia muda kumwezesha kuwatatulia kero hizo.
“Nawashukuru
kwa kuniombea pale nilipokuwa nikiugua, nilikuwa nje ya nchi kwa
matibabu sala zenu zimeniwezesha kuungana nanyi leo," alisema.
Aliwaeleza
wananchi wa Kijiji cha Mlungi kuwa tatizo la maji na umeme viko mbioni
kutatuliwa ndani ya mwaka huu na kwamba wale wanaoeneza maneno kuwa
hakutafanyika kitu wanajidanganya kwa vile mambo yanakwenda sawa.
Majimarefu
alisema katika kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo, ameamua
kumkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mhandisi Robert Gabriel kusimamia
Mfuko wa Jimbo kusaidia miradi.
Katika
hatua nyingine, Majimarefu aliwashukia mahasimu wake wa kisiasa aliodai
wanatumia mbinu chafu kumchafua kuhusu afya yake tangu alipougua na
kwenda kutibiwa nje.
“Kuna
mahasimu wangu wa kisiasa wanapita kila kijiji kuzungumzia afya yangu
kwamba nimepoteza fahamu na kukatwa mguu, siyo kweli myapuuze,”alisema.
Majimarefu alisema wananchi wapuuze uzushi huo usiokuwa na msingi kwani una lengo la kuwavunja moyo kwa manufaa yao ya kisiasa.
Hata
hivyo, alisema kuwa hatavunjika moyo kwa maneno hayo na badala yake
yamekuwa changamoto kwake kutekeleza ahadi zake na hafanyi hayo kwa
lengo la kujipatia umaarufu kama inavyodaiwa na baadhi ya watu ila ni
moja ya utekelezaji wajibu wake kwa wananchi waliomchagua.
Majimarefu
aliwaeleza wananchi hao kuwa wakati wa watu kufanya fitna umekwisha na
uliobaki ni ule wa kusema ukweli akiwahimiza kufanya kazi sambamba na
kulinda rasilimali misitu.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Gabriel, alisema kwamba kazi yake ni
kusimamia rasilimali za umma, hivyo atahakikisha kwamba yale yote
yanayoanzishwa na mbunge huyo anayalinda.