ILULA IRINGA TANZANIA

ILULA IRINGA TANZANIA
KIKOTI.COM BLOG - ILULA IRINGA TANZANIA / 0769694963 .......................................

Jumatano, 31 Agosti 2016

KAULI 10 NZITO ZA MHE.MBOWE

Image may contain: 4 people , outdoor
1.“Tunajua uamuzi huu utawaumiza sana wafuasi wetu, na uamuzi huu umeniumiza sana hata mimi mwenyewe, lakini ni nani miongoni mwa viongozi wetu na wanachama wetu ambaye anaweza kuombwa kuahirisha jambo na viongozi wa madhebu na dini zote hapa nchini na akawakatalia?”
2.“Polisi na Serikali wajue kuwa, hatuahirishi maandamano na mikutano yetu kwa sababu ya mazoezi, risasi au mabomu ya polisi. Hatuahirishi kwasababu ya usafi wao, wanaofanya kesho na wala hatuahirishi kwasababu ya ndege za kijeshi zinazoruka, ila tumeamua kuwaheshimu viongozi wetu dini.”
3.“Tunawaomba wanachama wetu, wapenzi wetu na wapenda demokrasia kote nchini watusamehe na wakubali kuwapa viongozi wa dini hizi wiki tatu, watafute suluhu kwa kuonana na Rais na ikishindikana, hatutarudi nyuma. Tutaingia barabarani.”
4.“Tangu tulipotangaza operesheni Ukuta, jumla ya wanachama na viongozi wetu 230 katika maeneo mbalimbali wamekamatwa na kushitakiwa kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo uchochezi na jumla ya viongozi na wanachama wetu 28 wapo rumande mpaka sasa pasipo sababu za msingi.”
5.“Haikuwa rahisi sisi kufikia uamuzi huu, hatukuwa tayari kurudi nyuma. Lakini viongozi wa dini na taasisi zinazoheshimika hapa nchini wametusihi. Mpaka Mama Maria Nyerere ameongea na Mheshimiwa Lowassa na kutuomba tuahirishe ili watafute suluhu ya suala hili.”
6.“Hatuogopi mabomu wala risasi za polisi, tuna uwezo wa kuandamana kwasababu tunazo mbinu za kufanikisha mipango yetu. Juzi polisi walitukamata na kuzuia kikao cha Kamati Kuu ila jana tumekifanya na wala hawajui tumefanyia wapi na saa ngapi.”
7.“Wakati tukifanya harakati hizi, tunaendelea pia kufungua kesi sehemu mbalimbali. Tundu Lissu na jopo lake tayari wameandaa mashitaka 15 ili tuweze kuyafungua katika mahakama zetu hapa nchini. Tutadai haki mahakamani na tutaidai barabarani.”
8.“Inasikitisha sana kuona taifa lina rais anayeomba watu wamuombee kila siku, ‘Niombeeni jamani’, lakini amekuwa akijaribu kuwakwepa viongozi wa dini kila wanapotaka kumuona ili kuzungumza naye kuhusu amri haramu ya kuzuia mikutano ya hadhara.”
9.“Viongozi wa dini walituomba wiki mbili au tatu ili wafanye mazungumzo na Rais Magufuli, sisi tumewapa mwezi mzima kabisa, ili wasake suluhu ili sisi kama vyama vya siasa tupewe haki yetu ya kisheria na kikatiba. Ikishindikana hakika sisi hatutarudi nyuma.
10.“Salum Mwalimu bado yupo rumande kwasababu za hovyo, Polisi wamekataa kumpeleka mahakamani leo wanadai wapo ‘busy’ eti wanazuia maandamano ya UVCCM, yalipangwa kufanyika leo. Sisi wote ni wafungwa watarajiwa lakini hatutarudi nyuma.

Upinzani waahirisha maandamano Tanzania(Ukuta)

 Viongozi wa upinzani wakati wa kikao na wanahabari Dar es Salaam
Muungano wa vyama vya upinzani nchini Tanzania umeahirisha maandamano ya kitaifa ambayo yalikuwa yamepangiwa kufanyika kesho.
Viongozi wa upinzani, akiwemo Edward Lowassa wa Chadema, wametangaza hatua hiyo kwenye kikao na wanahabari Dar es Salaam.
Wamesema wameahirisha maandamano hayo kwa kipindi cha mwezi mmoja baada ya kusikia ombi la viongozi wa kidini na wadau wengine waliowaomba kukumbatia na kuyapa muda mazungumzo.

Taarifa Toka IKULU : Rais Magufuli atengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 31 Agosti, 2016 amemteua Bw. Doto M. James kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Kabla ya uteuzi huo Bw. Doto M. James alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango (Sera).

Bw. Doto M. James ataapishwa kesho tarehe 01 Septemba, 2016 saa 2:45 Asubuhi Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Kufuatia uteuzi huo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Servacius Likwelile atapangiwa kazi nyingine.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
31 Agosti, 2016

Makusanyo Kodi za Simu Yapanda Maradufu

Sheria ya Fedha ya Mwaka 2016 iliyopitishwa kuhusu utozaji ushuru kwenye ada ya kutuma na kupokea fedha kwenye miamala ya benki na simu, imeanza kuzaa matunda kutokana na ongezeko la mapato lililoanza kushuhudiwa kutoka kampuni za simu.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iliyokutana jana na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), iliambiwa kutokana na sheria hiyo iliyopitishwa Bunge baada ya kupitisha bajeti ya mwaka huu, mwezi uliopita serikali imeshuhudia ongezeko kubwa la mapato, yaliyotolewa na kampuni za simu.

Taarifa hiyo ilitolewa jana kwenye Kamati ya Kudumu ya Miundombinu, imeonesha Kampuni ya Vodacom ilikuwa ikitoa kodi ya ushuru wa bidhaa kwa fedha zinazotumwa kwa wastani wa Sh milioni 360 kwa mwezi, lakini baada ya mabadiliko ya sheria, Julai pekee mwaka huu imelipa Sh bilioni 1.9.

Mwakilishi wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Godwin Barongo aliiambia kamati hiyo kuwa kwa upande wa Kampuni ya Tigo, walikuwa wanatoa wastani wa Sh milioni 250 kwa mwezi, lakini sasa wametoa Sh bilioni 1.48.

Barongo ambaye ni Meneja Msaidizi, Kitengo cha Walipa Kodi Wakubwa TRA alikuwa akizungumzia namna Mtambo Maalumu wa Kusimamia Mawasiliano na Udhibiti wa Mapato yatokanayo na Simu (TTMS) unaosimamiwa na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) ulivyowezesha kufanikisha ukusanyaji mapato.

“Pamoja na mabadiliko ya sheria yaliyoanza mwezi Julai mwaka huu, kampuni za simu zilikuwa zikitoza transfer, lakini sheria ilikuwa haigusi kwenye kutoa, Baada ya hiyo, tuligundua kuwa sasa kamisheni nyingi zilipelekwa kwenye kutoa kwa sababu hakuna tozo na kwenye transfer zinapungua,” alisema Barongo.

Aliendelea kusema, “Kwa hiyo mabadiliko haya ya sheria ya sasa hivi ambayo tunatoza kwenye kuweka na kutoa, yametusaidia.” 
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso alisisitiza kuwa wabunge wanategemea Wizara ya Miundombinu kupitia sekta ya mawasiliano, ichangie mapato mengi kwa serikali.

Baada ya Bunge kupitisha mabadiliko ya sheria ya fedha yaliyopitisha utozaji kodi ya ushuru wa bidhaa katika miamala ya benki na simu za mkononi, ulijitokeza mjadala ambao baadhi ya watu walidai ushuru huo utaathiri wateja wa kampuni za simu na benki.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alifafanua kwamba serikali imeamua kutoza ushuru kwenye ada ya kutuma na kupokea fedha au vyote kwa kadri itakavyotozwa akisisitiza kwamba utalipwa na benki na kampuni na si mtumiaji au mpokeaji wa fedha katika miamala itakayofanyika

Lowassa Aandika Waraka Mzito Kuhusu Oparesheni UKUTA

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa ameandika barua kuhusu operesheni ya chama chake iliyopewa jina la Ukuta na jinsi ambavyo jeshi la Polisi na Serikali lilivyopanga ‘kuubomoa’.

Katika waraka huo, Lowassa ameeleza kuwa ameamua kushika kalamu na kuandika masikitiko yake kuhusu hali ya amani nchini akidai Serikali imekata mkono wa amani.

Ameeleza kuwa Serikali imekandamiza upinzani na demokrasia na ndio chanzo cha wao kuanzisha UKUTA kupinga ukandamizaji huo.

“Binafsi nafurahishwa na kutiwa moyo na jinsi watanzania walivyoipokea Operesheni hii, pamoja na vitisho vya dola,” ameandika. “Siku zote sisi Chadema na Ukawa kwa ujumla ni wenye kulitakia amani na utulivu Taifa letu. Maandamano haya ya Septemba 1 ni ya amani, lakini vitendo vya jeshi la polisi vimewapa wasiwasi Watanzania,” Lowassa ameongeza.

Katika andiko hilo, Lowassa amedai kuwa amekuwa akipigiwa simu na viongozi wastaafu pamoja na watu mashuhuri wakimshauri kushawishi wakae na Serikali kuzungumza ili kuepusha taifa kujiingiza katika machafuko. Aliongeza kuwa kukutana na Rais John Magufuli katika Jubilee ya miaka 50 ya ndoa ya Rais Mstaafu, Benjamini Mkapa ni sehemu ya juhudi hizo.

“Nyote ni mashahidi wa tukio la kukutana na Rais Magufuli katika Jubilei ya miaka 50 ya ndoa ya mzee Mkapa. Ulikuwa ni mwanzo wa juhudi zetu za kuwanyooshea mkono wa amani. Lakini tunashangazwa wenzetu hawako tayari kuupokea mkono huo,” ameandika.

Aliongeza kuwa katika kikao cha juzi cha ndani cha chama hicho kilichofanyika katika Hotel ya Giraffe jijini Dar es Salaam walipanga kuzungumzia jinsi ya kuunyosha zaidi mkono wa amani lakini Jeshi la Polisi ‘liliukata’.

“Kitendo kile kwangu binafsi kimezidi kuniimarisha na kunipa nguvu zaidi ya kudai demokrasia na kuheshimu katiba ambayo viongozi wetu waliapa kuifuata na kuitetea,” unasomeka waraka wa Waziri Mkuu wa zamani, Lowassa.

Magazeti ya Leo jumatano ya tarehe 31/08/2017
















Jumanne, 30 Agosti 2016

Lowassa, Mbowe Watakiwa Kuripoti Polisi Leo

Viongozi waandamizi wa Chadema akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa jana walikamatwa na Jeshi la Polisi wakati wakiwa katika kikao cha ndani katika Hoteli ya Giraffe mkoani Dar es Salam

Lowassa, ambaye alikaa kituoni hapo kwa takribani saa tatu anaweza kuwa kiongozi wa kwanza aliyewahi kushika nafasi ya Waziri Mkuu kuhojiwa na polisi.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu aliwataja viongozi wengine waliokamatwa kuwa ni Mwenyekiti, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika na Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Said Issa.

Mara baada ya kukamatwa, walipelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi ambako baadhi ya wajumbe na wabunge waliwafuata na kuwasubiri nje ya kituo hicho kujua hatima yao. 
Viongozi hao walionekana wakiingia Polisi saa 10.30 jioni na kutoka saa 1.25 usiku, jambo ambalo liliwafanya wakae kituoni hapo kwa saa tatu. 
Lissu alisema polisi walivamia kikao hicho kilichokuwa na wajumbe 170, wakiwamo baadhi ya wabunge wa chama hicho na kuwakamata viongozi hao kwa maelezo kuwa wamekaidi amri ya Jeshi la Polisi ya kuzuia mikutano ya ndani na nje ya vyama vya siasa. 
Imeelezwa kuwa viongozi hao wa Chadema walikuwa na mkutano uliotanguliwa na kikao cha viongozi wakuu na kufuatiwa na cha viongozi hao kikijumuisha wabunge, mameya na wenyeviti wa halmashauri. 
Wakiwa katika kikao hicho, ilielezwa kuwa watu wanne waliingia wakiwa wamevalia kiraia na kuwaeleza kuwa viongozi wao wanahitajika kituo kikuu cha polisi kutokana na kufanya mkutano kinyume cha sheria. 
Mbunge wa Viti Maalumu, Upendo Peneza ambaye  alikuwa kwenye mkutano huo alisema pamoja na mambo mengine ya chama, walikuwa wakijadili suala la operesheni Ukuta la Septemba Mosi kama liendelee au lisiendelee kutokana na hali ilivyo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwao, alisema viongozi hao walikamatwa kwa kukukaidi amri ya polisi ya kuzuia mikusanyiko ya kisiasa na kuchochea wananchi kuandamana kinyume cha sheria Septemba Mosi. 

Alisema baada ya kuachiwa kwa dhamana, viongozi hao wametakiwa kuripoti kituoni hapo leo. 
Wiki iliyopita, Jeshi la Polisi kupitia kwa Kamishana wa Operesheni na Mafunzo, Nsato Marijani lilipiga marufuku mikutano ya ndani likisema inatumika kuhamasisha watu kuvunja sheria za nchi na kupambana na askari. 

Hatua hiyo ilikuja huku jeshi hilo likiwa limepiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano kufuatia uamuzi wa Rais John Magufuli kuzuia shughuli  za kisiasa hadi 2020. 

Wanafunzi hewa 4,445 wabainika Kahama

 Image result for kahama
Imeandikwa na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jaffo, amesema Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, ina wanafunzi hewa 4445 ambao wanasoma katika shule za sekondari za serikali kinyume na utaratibu.
Jaffo aliyasema hayo wakati akizungumza na Watumishi wa Halmashauri za Msalala na Mji, juzi, katika ziara ya kushitukiza, ambapo aliwaasa kufanya kazi kwa weledi kwa kufuata sheria na taratibu za kuwahudumia wananchi.
Alisema kuwepo kwa idadi hiyo kubwa ya wanafunzi hewa katika shule za sekondari kunatokana na maofisa elimu kutokujua takwimu za wanafunzi na kuongeza kuwa, muda mwingi wamekuwa wakikaa ofisini bila ya kutembelea maeneo ya kazi.
Naibu Waziri huyo alisema, takwimu za utengenezaji wa madawati, zimekuwa kinyume na ilivyotarajiwa, hali ambayo imesababisha kuchelewa kumalizika kama iliovyokuwa imepangwa na Rais John Magufuli.
Pamoja na mambo mengine, Naibu Waziri huyo aliwaonya watumishi hao kutotumia fedha vibaya zitakazotolewa na wizara hiyo, kwa ajili ya kutengeneza miundombinu ya barabara katika halmashauri ya mji wa Kahama.
Mbunge wa Jimbo la Kahama, Jumanne Kishimba alimweleza Naibu Waziri huyo kuwa Halmashauri ya Mji wa Kahama, ina changamoto nyingi zikiwamo za miundombinu ya barabara, kuzidiwa kwa wagonjwa wanaotoka katika wilaya 16 katika hospitali ya halmashauri ya mji pamoja na upungufu wa watumishi.
Alisema Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kahama, imezidiwa na wagonjwa ambao wanatoka katika sehemu mbalimbali zilizopo jirani, hali ambayo watumishi wake wanapata wakati mgumu katika kutoa huduma na wakati mwingine kushindwa kutoa huduma kwa wakati.

Ajira zinakuja mh Angella Kairuki asema :. Nawashauri vijana wasijiingize kwenye makundi yasiyofaa wasubiri ajira zinakuja


SERIKALI imeanza kuwashughulikia watumishi walionufaika na fedha za watumishi hewa ambapo hadi sasa watumishi 839 wapo katika hatua mbalimbali wakiwemo waliofikishwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na wengine wanaendelea kuhojiwa polisi kwa ajili ya kufikishwa mahakamani.
Sambamba na hilo, serikali inatarajia kutoa ajira mpya 71,496 kwa mwaka huu wa fedha baada ya kukamilisha uondoaji wa wafanyakazi hewa. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angella Kairuki aliyasema hayo wakati akizungumzia utekelezaji wa mipango na mikakati ya wizara yake katika kipindi cha ‘Tunatekeleza’ kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1). Kairuki alisema,
“Kwa sasa tayari wapo watumishi wameshahojiwa na kuchukuliwa maelezo yao polisi na upelelezi utakapokamilika watachukuliwa hatua mbalimbali za kisheria, ikiwemo kufikishwa mahakamani… Tunakamilisha ushahidi na tutawatangazia tutakapokamilisha,” alisema.
Alisema waligundua kwamba kuna maofisa utumishi na wahasibu ambao siyo waaminifu, badala yake walikuwa wakielekeza fedha kwa ndugu zao na miradi yao na wengine walishastaafu lakini bado majina yao yalikuwa yakiendelea kupokea mishahara wakati walitakiwa kuondolewa kwenye mfumo.
Alisema kwa kipindi cha Machi mosi hadi Agosti 20 mwaka huu, watumishi hewa waliogundulika ni zaidi ya 16,127 na kuisababishia serikali hasara ya mabilioni ya fedha. Kwa kipindi cha Agosti pekee watumishi hao hewa wangelipwa mishahara wangeisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 16.
“Uhakiki huu ni endelevu na tumegundua changamoto kubwa katika usimamizi wa mishahara ni uadilifu kwa watu waliokasimiwa madaraka. Maofisa Utumishi, Maofisa Utawala na Wahasibu wamepewa madaraka lakini wengi wao siyo waaminifu, hivyo kwa sasa tumeweka uwajibikaji kwa waajiri,” alisema.
Aidha alisema wanaufanyia mfumo wao maboresho zaidi ili uweze kuchakata taarifa nyingi zaidi ambapo pia sekta ya mishahara imeshushwa katika ngazi za chini zaidi hasa katika sekta za elimu na afya ambazo zimekutwa na watumishi hewa wengi zaidi ili waweze kuwa na taarifa za mtumishi mmoja mmoja.
Alisema upo muongozo ambao fedha za serikali zinaporejeshwa zinapitia hazina na kusisitiza kwamba wataendelea kuhakikisha wanasimamia fedha zote ambazo zilichukuliwa serikalini kinyume na utaratibu na isivyo halali zinarudishwa kwa mfumo sahihi.
Pia alisema wameongeza kasi ili kuhakikisha kunakuwa na nidhamu ya kazi na uwajibikaji kwa watumishi wa umma, hivyo wanaanda mkataba wa utendaji kazi kwa watumishi wa umma na ikiwezekana utaanza kutumika mwaka ujao wa fedha.
Alisema serikali imefanya maboresho makubwa katika mishahara na motisha kwa ajili ya maslahi ya watumishi wa umma, sambamba na kuhimiza taasisi mbalimbali kuweka vitendea kazi ili kuwawezesha wafanyakazi kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Akizungumzia ajira hizo mpya Kairuki aliwatoa hofu watanzania waliokuwa wanatarajia ajira serikalini na kusisitiza kwamba walichokuwa wanasubiri ni takwimu halisi kwa taasisi ili kujua ni watumishi wangapi wameondolewa.
“Baada ya kukamilisha mchakato huo, hatua nyingine zitaendelea… Hii ni neema kwa waliomaliza vyuo, cha msingi wavute subira maana tutatoa ajira 71,496 kwa mwaka huu wa fedha na hatukuzifuta ajira. Nawashauri vijana wasijiingize kwenye makundi yasiyofaa wasubiri ajira zinakuja,” alisema. Katika hatua nyingine, Kairuki alisema, wamepokea malalamiko zaidi ya 200 kutokana na ukiukwaji wa sheria ya maadili ya viongozi wa Utumishi wa Umma ambayo inamnyima mtumishi kutotumia madaraka yake vibaya.
“Katika malalamiko hayo 142 yanahusu sheria ya maadili. Sekretarieti ya Maadili imefanya uchunguzi wa awali na malalamiko 12 yataanza kufikishwa Baraza la Maadili na hatua mbalimbali zinaweza kuchukuliwa ikiwemo kushushwa vyeo au kuachishwa kazi,” alisema.
Pia aliwaagiza maofisa utumishi kuwahudumia watumishi na kuwapa haki zao ikiwemo kuwapandisha madaraja kwa wakati pale wanapostahili. Aidha Kairuki alikemea tabia ya baadhi ya watu kughushi taarifa za utumishi wa umma na kusisitiza kwamba jambo hilo ni kosa kubwa kwa yeyote anayefanya hivyo.
“Mtu yeyote ambaye anatoa nyaraka za serikali na siyo mlengwa au anayetoa nyaraka ambayo imewekewa zuio kwa mujibu wa sheria ni kosa la jinai na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. Tunawasisitiza watumishi wa umma kuhakikisha wanazingatia sheria hizo na mwongozo wa utoaji nyaraka na kumbukumbu za taarifa za serikali,” alisema.
 https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjPIRiuCu-pbeMneQbRw6xO4fK054P32No4NJciADd8tYSD2QmTI1047hLx3Q-zGgWxYOazVOcCJf0LSIthRjWY2PiXDf_vM3buIwd25Wf6YO-J5pZWiqY_cGKNE63-haqgWI7gjmobmAND/s640/IMG-20160815-WA0011.jpg

Magazeti ya Leo jumanne ya tarehe 30/08/2016