Rais Magufuli alitoa agizo hilo la siku saba jana wakati wa uzinduzi wa magari 580 ya kusafirishia saruji ya Kampuni ya Dangote uliofanyika kiwandani hapo. “Nia yangu nataka kiwanda hiki kifanye kweli ili ikiwezekana ujenge viwanda vingine…ujenge hata kumi,” amesema Rais Magufuli.
Amemruhusu Dangote auze makaa hayo kwa watu wengine ili Serikali ipate fedha na ameiagiza Wizara ya Nishati na Madini kukusanya mapato ya uchimbaji wa makaa hayo kwa Dangote mwenyewe. Rais amemhakikishia Dangote kuwa, ndani ya siku saba atakuwa amepata kibali cha kuchimba makaa ya mawe kwa ajili ya kiwanda hicho cha saruji.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango na Mmiliki wa kiwanda cha Dangote, Alhaji Aliko Dangote.
Pamoja na kuagiza kampuni ya Dangote ipatiwe eneo la kuchimba makaa ya mawe, Rais Magufuli ameitaka Wizara ya Nishati na Madini kuhakikisha inafikisha gesi katika kiwanda hicho haraka iwezekanavyo, lengo likiwa kuondoa vikwazo vya uhaba wa makaa ya mawe na ukosefu wa gesi, ambavyo vimekuwa vikisababisha uzalishaji wa saruji kusimama mara kwa mara.
Magufuli pia aliitaka kampuni ya saruji ya Dangote kuwasiliana moja kwa moja na Serikali pale inapohitaji huduma yoyote, badala ya kuwatumia watu wa kati ambao wamekuwa wakisababisha kuongezeka kwa gharama za uendeshaji na bidhaa na hivyo kuathiri uzalishaji wa saruji wa kiwanda hicho.
Kabla ya kuzindua rasmi magari hayo, Rais Magufuli alipokea kero za madereva ambao walifanya usaili wa kuomba kazi ya kuendesha magari hayo tangu miezi miwili iliyopita.
Madereva hao walimueleza kuwa menejimenti ya kiwanda hicho haijawaita kazini mpaka leo, licha ya kuwepo kwa malori mapya wanayopaswa kuendesha, huku Menejimenti ikiendelea kutumia malori ya watu binafsi kupitia kampuni za kati, ambazo ndizo zimekuwa zikitumika kutoa huduma nyingi kwa kiwanda.
Kutokana na malalamiko hayo, Rais Magufuli alimshauri mmiliki wa kiwanda hicho, Dangote kuiangalia vizuri menejimenti yake na kuitaka iachane na wafanyabiashara wa kati, ikiwemo kampuni moja iliyotaka kupewa zabuni ya kupokea gesi kutoka Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kisha kuzalisha umeme na kuiuzia Dangote.
“Ndugu Alhaji Aliko Dangote, iangalie vizuri menejimenti yako, inawatumia watu wa kati na ndio hao wanaosababisha matatizo, na mimi nimeshaiagiza wizara hakuna kuuza gesi kwa watu wa kati, tunataka tukuletee gesi wewe mwenyewe na uzalishe umeme wewe mwenyewe,” alisisitiza Rais Magufuli.
Kwa upande wake, Dangote alielezea kufurahishwa kwake na uwekezaji wa kiwanda hicho, uliogharimu Dola za Marekani milioni 650 na kwamba kiwanda hicho kitakachozalisha tani milioni mbili za saruji mwaka huu, kinatarajia kufikia uzalishaji wa tani milioni tatu mwaka ujao.
Alisema kutokana na uzalishaji huo, kiwanda kitazalisha ajira 20,000 huku kikiwa kimesaidia kupunguza bei ya saruji nchini kutoka Sh 15,000 kwa mfuko wa kilo 50 hadi kufikia Sh 10,000.
Dangote aliongeza kuwa tangu kampuni yake ianze kuuza saruji bei ya bidhaa hiyo sokoni, imeshuka kutoka Sh 15,000 kwa mfuko mmoja wa kilo 50 hadi kufikia Sh 10,000 na kwamba imeamua kununua magari ya kusafirisha saruji ili iweze kusambaza saruji hiyo nchi nzima kwa gharama nafuu, ambayo Watanzania wengi wataimudu.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema licha ya kuzalisha ajira, tangu kampuni hiyo ianze shughuli zake imeshalipa kodi kiasi cha Sh bilioni 46.139 na kodi inatarajiwa kuongezeka kadiri uzalishaji unavyopanda.
Magufuli aagiza mazungumzo na Dangote yaishe Aidha, Rais Magufuli ameagiza kwamba ikifika Jumatano wiki ijayo, mazungumzo kati ya Wizara ya Nishati na Madini na bilionea Aliko Dangote, yawe yamekwisha ili gesi ipatikane kwenye kiwanda cha saruji cha mfanyabiashara huyo.
Ameagiza kwamba, wizara hiyo ijadiliane na Dangote mwenyewe, badala ya kupitia kwa watu aliowaita kuwa ni matapeli. Aliwatuhumu baadhi ya wawakilishi wa mfanyabiashara huyo kuwa wanachelewesha uwekezaji na huenda wanashirikiana na viwanda vingine vya saruji kuihujumu Serikali.
“Inawezekana watu wako wanaokuwakilisha wana matatizo, hii ni meseji kwa mheshimiwa Dangote mwenyewe, ni lazima awe mwangalifu kwa watu wake,”amesema Rais Magufuli. Alisema mfanyabiashara huyo ni mwekezaji muhimu Tanzania, kwa kuwa amewezesha maelfu ya Watanzania kupata ajira na pia Serikali inapata mapato kupitia kodi.
Alimshukuru Dangote kwa kuwekeza Tanzania na pia amemshukuru Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kwa kusimamia mchakato uliowezesha kujengwa kwa kiwanda kikubwa cha saruji mkoani Mtwara.
“Mheshimiwa Kikwete popote ulipo asante sana na Mungu akubariki,” alisema Rais Magufuli. Desemba 10 mwaka jana, Rais Magufuli alizungumza na Dangote Ikulu jijini Dar es Salaam na kumhakikishia kuwa serikali ya Tanzania, itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji ili kutimiza lengo la kuwa na Tanzania ya viwanda.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, hakukuwa na tatizo kuhusu kiwanda cha kuzalisha Saruji cha Dangote mkoani Mtwara, ila kulikuwa na watu waliotaka kujinufaisha kwa kufanya biashara za ujanja.
“Iwapo unataka maelezo yoyote ama lolote linalokukwamisha uwasiliane na viongozi wa serikali badala ya kuwasiliana na watu ambao wako kwa ajili ya kufanya biashara ya ujanja ujanja kwa lengo la kupiga dili, “ Rais Magufuli alimweleza Dangote.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, Dangote alihitaji eneo dogo ambalo angelitumia kusafirishia saruji, wakajitokeza watu waliotaka kumuuzia kwa shilingi bilioni 43. Wakati wa mazungumzo hayo, Dangote alisema makaa ya mawe ya Tanzania ni rahisi na yana ubora kuliko ya nje.
Alisema, anafanya biashara nchini kupata faida na kuisaidia serikali ya Tanzania kuwawezesha wananchi kupata ajira. Alimhakikishia Rais Magufuli kuwa ataendelea kufanya kazi na Serikali ya Tanzania; na ana mpango wa kutafuta fursa nyingine za uwekezaji nchini, kwa kuwa kuna sera nzuri za uwekezaji.
Azindua kituo cha kupooza umeme cha Tanesco Wakati huo huo, Rais Magufuli amezindua kituo cha kupooza umeme cha Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kilichopo mjini Mtwara, ambacho kinajengwa kwa fedha na wataalamu wa Tanesco kwa gharama ya Sh bilioni 16.
Mradi huo utahusisha ujenzi wa njia ya umeme ya kilovoti 132 kutoka Mtwara hadi Lindi, hivyo kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme katika mji wa Lindi.
Magufuli alimpongeza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, menejimenti na wafanyakazi wa Tanesco kwa kazi nzuri wanayofanya iliyowezesha usambazaji wa umeme kuongezeka hadi kufikia asilimia 46 ya nchi nzima.
Lakini, aliiagiza Tanesco kuwakatia umeme wote wenye madeni, bila kujali kama ni taasisi ya umma ama binafsi. Mapema jana asubuhi, Rais Magufuli alisali ibada ya Dominika ya kwanza ya Kwaresma katika Kanisa la Watakatifu Wote Jimbo Katoliki la Mtwara, ambako amechangia Sh milioni moja na mifuko 200 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa uzio na ukarabati wa kanisa hilo.
Aliwataka wananchi wa Mtwara, kushikamana kuiombea nchi na kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo ya mkoa na Taifa zima.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni