Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli jana
tarehe 05 Machi, 2017 amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku 4 katika
mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara.
Kabla
ya kuondoka Mjini Mtwara na kurejea Jijini Dar es Salaam Mhe. Rais
Magufuli alifanya mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mashujaa Mjini
Mtwara ambapo alisema Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuhakikisha
inasukuma maendeleo ya Mtwara na Lindi kwa nguvu kubwa kwa manufaa ya
wananchi.
Alisema
Serikali imedhamiria kutilia mkazo juhudi za uendelezaji wa bandari ya
Mtwara, ujenzi wa barabara, uimarishaji wa miundombinu ya nishati ya
umeme, ujenzi wa viwanda vikubwa na usimamizi mzuri wa shughuli za
kilimo ambavyo vitasaidia kukuza uchumi, kuzalisha ajira na kuboresha
maisha ya watu.
Mhe.
Rais Magufuli aliwapongeza viongozi na wananchi wa Mkoa wa Mtwara kwa
mafanikio yaliyopatikana katika soko la korosho lililopita na ameagiza
wale wote waliohusika kufuja fedha za wakulima wachukuliwe hatua.
Aidha,
Mhe. Dkt. Magufuli alisema Tanzania itaendeleza uhusiano na ushirikiano
wake mzuri na nchi jirani ya Msumbiji na ametaka suala la wahamiaji
haramu wanaoondolewa nchini humo wakiwemo Watanzania lisikuzwe huku
akisisitiza kuwa Serikali haiwezi kuwatetea watu wanaoishi katika nchi nyingine bila kufuata sheria.
Kuhusu
Mkoa wa Mtwara kufanya vibaya kielimu, Mhe. Rais Magufuli amewataka
wananchi wa Mtwara kubadilika kwani juhudi za Serikali kuwapelekea
maendeleo hazitakuwa na maana kama wananchi watakuwa hawana elimu.
“Nimeambiwa hapa watu wanapenda sana disco na ngoma, watoto badala ya kusoma wanacheza disco, hapo tunakwenda pabaya” alisisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mkutano
wa Mhe. Rais Magufuli Mjini Mtwara ulidhuriwa na viongozi mbalimbali
wakiwemo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William
Lukuvi, Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo, Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, Waziri wa Fedha na
Mipango Dr. Philip Mpango, Wabunge na viongozi wa taasisi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni