Na Humphrey Polepole
Mabadiliko ya Katiba ya CCM 2017 yamegusa maeneo gani?
Hivi
karibuni kumekuwapo maneno ya upotoshwaji juu ya Mabadiliko ya Katiba
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yaliyofanyika tarehe 12 Machi 2017. Napenda
kufafanua kwa uchache maeneo ambayo yamefanyiwa Mabadiliko ili kuanzia
sasa ieleweke bayana kwamba msingi wa Mabadiliko haya ni Mageuzi Makubwa
ambayo yanafanywa na Chama chetu ili kuongeza tija, ufanisi,
uwajibikaji, kupunguza gharama za uendeshaji, kupiga vita rushwa na
ubadhirifu wa mali za umma.
Mageuzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
yanalenga kutizama Uongozi (Leadership), Muundo/Mfumo (Structure/System)
na Utawala (administration). Chama chetu kimetimiza miaka 40 mwaka huu
(2017) tangu kuanzishwa kwake na kipindi hiki tumeazimia kwa kauli moja
kukiimarisha, kukijenga na kukifanya madhubuti. Kazi hii ya Mageuzi ya
CCM ilianzishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM iliyokaa katika
Mkutano wake wa mwenzi Desemba 2016 na baadaye kupitishwa kwa sauti moja
na Mkutano Mkuu Maalum wa Machi 2017.
Ikumbukwe kwamba mabadiliko
haya ya Katiba yangaliweza kupendekezwa na kuanza kutumika pasina ya
kuitisha Mkutano Mkuu, lakini hekima ya Uongozi wa Chama chini ya
Mwenyekiti Ndugu Magufuli na Katibu Mkuu Ndugu Kinana ikatuongoza kwamba
Mabadiliko haya ambayo yanajenga msingi wa Mageuzi ya Chama chetu
lazima yashirikishe wanachama wetu.
CCM kama chama cha siasa ili
kifanye kazi yake vizuri na yenye matokeo makubwa chanya, ilikusudiwa
lazima kihuishwe ili kiweze kwenda na wakati na kutekeleza matakwa ya
wanachama, kwa kuzingatia ukweli kuwa lengo kuu la chama chochote cha
siasa ni kushika dola.
Mabadiliko ya Kikatiba ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) yana lengo la kukiimarisha chama chetu ili kuziteka
hisia, mioyo na fikra za watanzania wengi, kwa nia ya kukiunga mkono
katika lengo lake la kushika dola na kuleta maendeleo endelevu kwa
watanzania.
Katiba ya CCM imekuwa ikifanyiwa marekebisho mara kwa
mara tangu ilipotungwa mwaka 1977, kwa madhumuni ya kuiboresha ili
iendane na wakati uliopo. Kwasababu hiyo, yamekuwepo matoleo 12 ya
Katiba hii hadi mwaka 2012. Katiba ambayo imepitishwa na Mkutano Mkuu
Maalum tarehe 12 Machi 2017 jijini Dodoma, inakuwa toleo la 14.
Mabadiliko haya yanalenga kurekebisha Muundo, Mfumo, Uongozi, Utendaji na mengineyo.
Mambo muhimu ambayo yamezingatiwa katika marekebisho haya ni yafuatayo; –
MFUMO WA CHAMA
Mfumo
wa Chama, una sura ya serikali na utawala na kuwa na ngazi nyingi ya
vikao vya uamuzi. Hali hii inafanya gharama ya kukiendesha Chama kuwa
kubwa, vikao haviitishwi na maamuzi ya chama hayawafikii walengwa. Hivyo
basi yafuatayo yanazingatiwa,
Kupunguza wingi wa vikao vya
nadharia na badala yake kuwa na vikao vichache vinavyofanyika, vyenye
maamuzi yenye tija na kujenga uhai wa chama.
Kupunguza idadi ya
wajumbe au wawakilishi ili wawe wachache lakini wenye umakini na uwezo
wa kusimamia sera, itikadi, maamuzi ya chama pamoja na kuondoka urasimu
na kupunguza gharama za uendeshaji pasina kuathiri ubora wa uwakilishi.
Muundo wa Wilaya za Chama uendane na uundo wa sasa wa wilaya za Serikali
Uzito
mkubwa umewekwa katika kuimarisha chama katika ngazi ya shina, eneo
ambalo ndilo waliko wapiga kura. Kwa kufanya hivyo, chama kitakuwa
karibu na watu na watakiona kuwa ni chama chao.
Uendeshaji wa
shughuli zote za jumuia za chama na mali zake uwe chini ya usimamizi wa
Chama cha Mapinduzi na Baraza la Wadhamini la Chama cha Mapinduzi.
VIONGOZI
Viongozi
wachache wamekuwa na tabia ya kujilimbikizia nafasi nyingi za Uongozi,
utendaji na uwakilishi katika Chama na Serikali. Hali hii hushusha
ufanisi na kupunguza tija. Nafasi nyingi kwa mtu mmoja ni kushindwa
kuleta ufanisi katika vikao husika.
Hapa imezingatiwa kuwa;
ukiacha wale wanaolazimishwa kikatiba kuwa na nafasi zaidi ya moja kwa
mujibu wa mamlaka yao, kuanzia sasa nafasi za Uongozi katika chama
zitakuwa si zaidi ya moja.
KURA YA MAONI
Mfumo wa kura za
maoni hukusudia kuimarisha demokrasia ndani ya chama na kuashiria nafasi
ya mgombea anayeonekana kukubalika zaidi. Hata hivyo, eneo hili
limekuwa na matokeo mabaya ya kukithiri kwa rushwa na kupata viongozi
wasio na imani ya kweli ya chama wanaosaka maslahi, wafanyabiashara
wenye malengo binafsi na mamluki.
Mapendekezo ya kuimarisha udhibiti wa kura za maoni; –
Katiba ya
CCM ya Mwaka 1977 Toleo la 2012 Ibara ya 61A(1-3) inaelekeza kura za
maoni za ubunge na uwakilishi zitapigwa kwenye mikutano mikuu ya jimbo
na si kwa wanachama wote matawini kama ilivyofanyika mwaka 2015.
Imependekezwa
ili kudhibiti taratibu za kura za maoni jimboni, kuepusha migawanyiko,
kuziba mianya ya rushwa na kuepusha wapiga kura mamluki, inapendekezwa
kufanya mabadiliko ya upigaji kura za maoni za ubunge na uwakilishi
pamoja na kufuata utaratibu ufuatao wa kuwajadili wanaogombea;
Wagombea
ubunge/uwakilishi watachukua fomu na kurudisha kwa Katibu wa CCM wa
Wilaya inayohusika. Fomu zote za wagombea ubunge/uwakilishi zitajadiliwa
na kutolewa mapendekezo katika ngazi ya wilaya, mkoa na Taifa kabla ya
kupigiwa kura za maoni.
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa
itateua majina yasiyozidi matatu ambayo yatawasilishwa mbele ya Mkutano
Mkuu wa Jimbo kwa ajili ya kupigiwa kura za maoni. Mkutano Mkuu wa Jimbo
utapiga kura za maoni kumpendekeza mwanachama mmoja awe mgombea wa
ubunge/uwakilishi katika jimbo hilo.
Mara ya baada ya kura za
maoni, mapendekezo ya uteuzi yataanzia kwenye Kamati ya Siasa Jimbo (kwa
Zanzibar), Kamati ya Siasa ya Wilaya (Tanzania Bara), Mkoa, Kamati
Maalum (Kwa Zanzibar), Kamati Kuu na hatimaye Halmashauri Kuu ya Taifa
itafanya uteuzi wa mwisho.
Utaratibu huu hautawapa fursa wagombea
kutengeneza makundi na kutoa rushwa kwasababu hakuna anayejua kama
atakuwepo kwenye orodha ya wagombea. Wale wana CCM wenye tabia ya
kujiandaa na vyama zaidi ya kimoja, kwa utaratibu huu hawataweza
kujiandaa mapema kuhamia vyama vingine. Utaratibu huu pia utasaidia
kuondoa urasimu na migawanyiko isiyokuwa na sababu.
Aidha,
utaratibu huu utahakikisha anapatikana mgombea mwenye msimamo thabiti wa
Chama na ni utaratibu halisi kwa chama kuusimamia ipasavyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni